Habari

Watanzania watakiwa kuacha kutumia vipodozi visivyokuwa na viwango

Naibu Waziri wa Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile amewaasa Watanzania hasa wanawake kuacha kutumia vipodozi visivyo na kiwango kutokana na vipodozi hivyo kusababisha magonjwa kama vile kansa pamoja na magonjwa mengine ya ngozi.

Dkt. Ndugulile ameyasema hayo leo, Bungeni mjini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mhe. Mattar Ali Salum, Mbunge wa Shaurimoyo juu ya adhabu inayotolewa kwa yeyote anayekamatwa akiingiza nchini vipodozi visivyofaa kwa matumizi ya binadamu.

“Kifungu cha 91(b) cha sheria ya chakula, dawa na vipodozi sura ya 219 kinatoa adhabu ya kifungo kisichopungua miezi mitatu au kulipa faini isiyopungua shilingi laki tano au adhabu zote mbili kwa matumizi ya binadamu,” alisema Dkt. Ndugulile.

Aidha amesema kuwa, sambamba na adhabu hiyo, mtuhumiwa anapaswa kugharamia uteketezaji wa vipodozi vyote vilivyokamatwa na wakaguzi.

Vilevile amesema, Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kudhibiti uingizwaji na utumiaji wa vipodozi hivyo ambavyo hutakiwa kusajiliwa kabla ya kibali cha kuingiza nchini kutolewa. Aidha mpaka sasa TFDA imesajili jumla ya vipodozi 3,179 ambavyo ndivyo vinaruhusiwa kuingizwa na kutumika nchini.

Dkt. Ndugulile amesema wakaguzi wa TFD wamewekwa katika vituo vya forodha kwenye mipaka ya Namanga, Holili, Horohoro, Tunduma, Sirari, Kasumulu, Mutukula, Rusumo, Bandari ya Dar es Salaam, Bandari ya Mwanza, Uwanja wa wa Kimataifa wa J.K. Nyerere na vituo vingine vya forodha vilivyopo katika mkoa wa Dar es Salaam kwa ajili ya kufanya ukaguzi wa bidhaa ikiwa ni pamoja na vipodozi vinavyoingizwa nchini.

Hata hivyo TFDA ilitenga na kutumia jumla ya Shilingi 154,800,000 kwa ajili ya operesheni maalum za ukaguzi wa bidhaa ikiwa ni pamoja na vipodozi. Aidha, kwa mwaka 2017/2018 Mamlaka imetenga jumla ya shilingi 132,160,000 ambazo zimekuwa zikitumika katika operesheni za kubaini na kukamata vipodozi.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents