Habari

Waziri Majaliwa awakaribisha Cuba kujenga viwanda Tanzania

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Cuba nchini Tanzania, Balozi Lucas Domingo Polledo, ambapo amewakaribisha wafanyabiashara wa Cuba kuja kuwekeza katika ujenzi wa viwanda vya dawa.

Waziri Mkuu aliyasema hayo wakati akizungumza na Balozi Polledo mjini Havana. Waziri Mkuu yuko nchini Cuba kwa ajili ya ziara ya kikazi yenye lengo la kudumisha ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.

Majaliwa alisema serikali imedhamiria kuendeleza sekta ya viwanda nchini kama mkakati wa kukuza uchumi na kufikia uchumi wa kati, hivyo wafanyabiashara kutoka nchini Cuba wanakaribishwa kuja kuwekeza nchini, hususani katika viwanda vya dawa na sukari.

Waziri Mkuu alisema licha ya Tanzania kuwa ni nchi ya amani na yenye utulivu wa kisiasa, pia imeweka mazingira mazuri ya uwekezaji jambo ambalo litawawezesha watakaokuja kuwekeza nchini kupata tija.

Pia alitumia fursa hiyo kuishukuru Serikali ya Cuba kwa ushirikiano mzuri na Serikali ya Tanzania kwa sababu Cuba ni mojawapo kati ya nchi zenye ushirikano wa muda mrefu na Tanzania hususani katika masuala ya Kisiasa, Kijamii, Kielimu na Kiuchumi.

“Tanzania na Cuba zina historia ya kutosha. Tunatambua mahusiano mazuri yaliyopo kati nchi zote mbili, ambayo yalikuwepo kuanzia Serikali ya Awamu ya kwanza chini ya uongozi wa Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Nyerere.”

Kwa upande wake, Balozi Polledo alisema Serikali ya Cuba itahakikisha uhusiano wake na Serikali ya Tanzania unaendelea kuimarishwa. Pia alipongeza jitihada zinazofanywa na Serikali katika kuboresha maendeleo pamoja na kukuza uchumi.

Na Emmy Mwaipopo

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents