Habari

YST yaeleza ongezeko la gunduzi, tafiti za kisayansi kwa mfumo wa akili bandia

SHRIKSHO la Wanasayansi Chipukizi (YST) limesema kuwa mwaka huu katika maonesho ya kitaifa ya kazi za ugunduzi na tafiti zinazofanywa na wanafunzi kutoka vyuo mbalimbal nchini kumekuwa na ongezeko kubwa la idadi ya gunduzi na tafiti za kisayansi ambazo ziko katika mfumo wa akili bandia.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwanzilishi mwenza wa YST, Dkt Gozibert Kamugisha alisema maonesho hayo ambayo yatafanyika Desemba 5, mwaka huu yatakuwa ni ya tofauti na miaka iliyopita, mwaka huu kuna ongezeko kubwa la idadi ya gunduzi ambazo ziko katika mfumo wa akili bandia.

Kamugisha alisema hiyo ni ishara kuwa vijana sasa wanaenda na kasi ya dunia ambayo inashuhudia ongezeko kubwa la gunduzi zenye kutumia akili bandia na matumizi yake.

Aidha alisema katika maonesho hayo yanatarajia kujumuisha takribani wanafunzi 90 kutoka mikoa yote ya Tanzania na kwamba kwa miaka 13 YST imekuwa ikitoka fursa kwa vijana kupatiwa mafunzo ya mbinu za kiutafiti wa sayansi, kufanya utafiti wa kisayansi na kufanya maonesho ya gunduzi zao baada ya kufanya mchakato mrefu wa kiutafiti.

“Mwamko unazidi kuwa mkubwa kwa wanafunzi wa Sekondari nchini katika kutuma kazi zao kwani mwaka huu waliotuma maombi ya gunduzi ni takribani wanafunzi 979 ambao wameiomba fursa ya kushiriki katika program hiyo,”alisema na kuongeza

“Baada ya kufanya mchujo tumepata maombi 361 ambayo yalichaguliwa na wanafunzi walipatiwa mafunzo ya namna ya kuendeleza kazi zao za kisayansi, hivyo yataonyeshwa huku mgeni rasmi katika maonesho anatarajiwa kuwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda,” alisema

Kwa upande wake Ofisa Mtendaji wa Taasisi ya Karimjee Jivanjee, Caren Rowland alisema kuwa taasisi hiyo imeendelea kuboresha programu mbalimbali zinazolenga kuwawezesha vijana kufikia ndoto zao ambapo mpaka sasa imeshadhamini wanafunzi 41 katika mikopo ya elimu ya juu na wanatarajia kudhamini wengine wanne na hivyo kufikia wanafunzi 45.

“YST wamekuwa wakifanya tukio la kipekee kwa kutoa jukwaa kwa vijana kutoka mikoa mbalimbali Tanzania ili kuonyesha ubunifu,ugunduzi,utafiti pamoja na tarata zao za kisayansi,tunawapongeza YST waandaaji wa mashindano hayo ambayo yanahamasisha na kulea akili za vijana wote nchini, hii ndio sababu ya Karimjee Jivanjee kutoa mkono wa hisani,” alisema

Naye Mmoja wa Wanufaikaji wa mashindano hayo, Alfred Ngulo alisema mafunzo hayo yaliwawezesha kuendeleza tafiti zao na hivyo kufikia malengo na kwamba anaipongeza YST kwa kushirikiana na Taasisi ya Karimjee kwa namna wanavyoibua na kuwasaidia wanafunzi katika kuhakikisha masomo ya sayansi yanazidi kukua nchini kwa lengo la kupata wataalamu wengi.

Written by Janeth Jovin

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents