Siasa

Wapigakura wamuibulia fitna nzito Waziri wa JK

WAPIGAKURA wa Jimbo la Manyoni M a s h a r i k i wamemuibulia fitna nzito Mbunge wao, John Chiligati kwa kile wanachodai ‘kawatapeli’ kwa kuwapelekea gari dogo kwa ajili ya huduma za wagonjwa.

Mwandishi Wa Habari Leo


WAPIGAKURA wa Jimbo la Manyoni M a s h a r i k i wamemuibulia fitna nzito Mbunge wao, John Chiligati kwa kile wanachodai ‘kawatapeli’ kwa kuwapelekea gari dogo kwa ajili ya huduma za wagonjwa.


Wapigakura hao wamemrushia tuhuma hizo Chiligati ambaye ni Waziri wa Ajira, Kazi na Maendeleo ya Vijana, anayeonekana ni mmoja ya mawaziri bora wa Rais Jakaya Kikwete.


Chiligati, ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Manyoni Mashariki (CCM), anatuhumiwa kuwadanganya wapigakura wake kwa kuwapelekea wananchi wa tarafa ya Kintinku gari
ya wagonjwa aina ya Toyota Mark II (maarufu kama baluni) badala ya Toyota Land Cruiser kwa ajili ya wagonjwa wa kituo cha afya cha tarafa hiyo.


Tuhuma dhidi ya Waziri Chiligati ziliwekwa bayana siku chache baada ya Waziri Mkuu, Edward Lowassa kumaliza ziara mkoani Singida, kwa kuwa wananchi wa tarafa hiyo walihoji ni kwa nini gari hilo pamoja na udogo wake likae makao makuu ya halmashauri badala ya kituoni hapo.


Chanzo cha habari hizi kimebainisha kuwa mmoja wa wananchi hao aliyetajwa kwa jina la Jumanne Abdallah, aliuliza swali hilo wakati wa ziara ya Waziri Mkuu Lowassa ambaye aliutaka
uongozi wa wilaya ujibu hoja hiyo papo hapo.


Inadaiwa Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Agnes Kitundu alimwambia Waziri Mkuu kuwa gari
lipo makao makuu ya halmashauri kwa kuwa kuna uhaba wa magari, hivyo litakuwa inahudumia maeneo mengine kwenye halmashauri hiyo.


Taarifa kutoka Singida zimebainisha kuwa, baada ya gari hilo kufikishwa Singida, Waziri Chiligati alizungumza na uongozi wa halmashauri ili libaki makao makuu ya halmashauri, gari jingine lililokuwapo hapo, Toyota Land Cruiser Hardtop lipelekwe kuhudumia wagonjwa katika
kituo hicho.


Tuhuma kuhusu gari hilo dogo ni miongoni mwa hoja 15 zilizojadiliwa katika kikao maalumu cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo kwa kuwa ilikuwa ni sehemu ya kasoro zilizobainishwa katika ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali iliyoishia Juni 30 mwaka jana.


Oktoba 31, mwaka juzi, Ofisa Afya wa Wilaya ya Manyoni aliyetajwa kwa jina la Erondola alimkabidhi Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni, Toyota Mark II
(GX81) yenye rangi nyeupe ikiwa na namba za usajili SM 4340, badala ya Toyota Land Cruiser kama wananchi walivyokuwa wakihitaji.


Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Singida, Parseko Kone, Mbunge huyo amekanusha tuhuma kwa nini alete ‘baluni’ badala ya Land Cruiser, kwa kile alichosema kwamba alishindwa
kukataa kupokea gari hilo, kwa kuwa wafadhili wasingemuelewa.


Gazeti hili lina taarifa kwamba Kone na Chiligati walikutana Mei 21, wakati wa ziara ya Waziri Mkuu Lowassa. Chiligati alimweleza Mkuu huyo wa Mkoa kuwa wafadhili waliahidi kuleta Toyota Land Cruiser Hardtop, lakini baadaye walibadili na kuleta Toyota Mark II, hivyo yeye alishindwa kulikataa.


Kwa mujibu wa Kone, Waziri Chiligati ndiye aliyeagiza gari hilo nchini Japan, lakini aina ya gari lililoletwa si lile aliloomba kwa wafadhili.


Maelezo ya Kone yamethibitisha madai kuwa halmashauri hiyo iliingiza fedha kwenye akaunti ya Waziri Chiligati ili kusafirisha gari kutoka Japan, uongozi wa halmashauri ukaenda
bandari ya Dar es Salaam kulichukua.


HabariLeo ina habari kuwa Mei 17 mwaka huu, Kone aliiamuru Taasisi ya Kuzuia Rushwa PCB) wilaya Manyoni, kuchunguza tuhuma hizo na kuwasilisha majibu kwake Mei 30 mwaka huu.


Hata hivyo, gazeti hili lilipozungumza na Kone juzi saa 3.00 asubuhi, PCB walikuwa awajawasilisha ripoti ya uchunguzi wao.


Alitoa agizo hilo katika kikao maalumu cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya wilaya hiyo, kilichojadili mambo kadhaa, ikiwamo taarifa ya Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali (CAG).


Sehemu ya barua hiyo ya Novemba 03, mwaka 2004 inasomeka: “Naomba suala hili tulizungumze katika Halmashauri ili iwapo tutakubaliana, basi Halmashauri ilipe Sh milioni 3.5 kwa ajili ya kusafirisha gari hilo ambalo ni Land Cruiser, japo sio jipya kabisa, lakini
ni reconditioned, hivyo ni gari imara kukabili barabara zetu.”


Vyanzo vya habari hizi vimedai kuwa, wafadhili wa Nagoya nchini Japan waliahidi kupeleka gari aina ya Toyota Land Cruiser na kwamba halmashauri hiyo ilimpatia Waziri Chiligati
Sh 5,900,500 kwa ajili ya kufanikisha kuletwa kwa gari hilo kwa ajili ya wagonjwa.


Kwa mujibu wa barua ya Katibu Mkuu Hazina ya Juni 06, 2005, Wizara ya Fedha ilitoa msamaha wa ushuru wa forodha, ushuru wa bidhaa na Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa ajili ya gari husika.


“ Hebu Mkurugenzi nieleze, katika hoja hii ya gari, Land Cruiser halikupokelewa kutoka Nagoya Japan na badala yake likaletwa gari aina ya Toyota GX Mark II,” Kone aliuliza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manyoni (Jane Kitundu).


Inadaiwa kuwa, baada ya Kitundu kushindwa kutoa maelezo, alimwomba Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Charles Mongo awaeleze wajumbe kwa nini gari halikuwa kwenye mamlaka ya wilaya hiyo, na yeye alisema Mbunge wa Manyoni Mashariki, Waziri Chiligati,
ndiye aliyekuwa akishughulikia taratibu za ununuzi wa gari hilo.


Akizungumza kwa simu ya mkononi jana kuhusu tuhuma hizo, Waziri Chiligati alikiri kuingiza nchini gari dogo kwa ajili ya wagonjwa badala ya Land Cruiser (Hard Topmaarufu kama mkonga).


Alisema uingizaji wa gari hilo ulitokana na juhudi zake binafsi kama Mbunge kutaka kuokoa maisha ya wakazi wa Kintinku na ndipo alipowasiliana na Shirika la Transport Aid la Japan ili kupata msaada wa gari.


“Barua yangu ilikuwa ni kuomba Land Cruiser maarufu kama mkonga (Hard Top) na tukakubaliana kuwa wangenitumia gari hilo ndipo nilioomba fedha ambazo zilikuwa zikitumwa
moja kwa moja Japan.


“Lakini wakati tukiendelea na mawasiliano ndipo waliniambia tayari wameshatuma gari aina ya Toyota Mark II na lipo tayari bandarini kwa ajili ya kulisafirisha na niliwasiliana na Mkurugenzi wa Halmashauri akanishauri tulichukue hatuwezi kukataa msaada, nikafanya hivyo, lakini naona kuna watu hawanielewi kabisa,” alisema Waziri Chiligati.


Source: Daily News

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents