Habari

Video: Daraja refu kuliko yote duniani laanza kutumika rasmi, lajengwa kwa miaka tisa lina urefu wa maili 34

Rais wa China, Xi Jinping amefungua rasmi daraja refu zaidi duniani, ambalo limekuwa likijengwa kwa miaka tisa. Daraja hilo, ukijumuisha pia barabara zinazolinganisha pamoja, lina urefu wa 55km (maili 34) ana linaunganisha Hong Kong na Macau na jiji la China bara la Zhuhai.

Kwa mujibu wa chombo cha habari cha BBC, Ujenzi wa daraja hilo umegharimu $20bn (£15.3bn) na umecheleweshwa mara kadha. Ukatumia mwendo wa kawaida wa kutembea wa 5km kwa saa, basi itakuchukua saa 11 kulivuka daraja hilo ukaamua kutembea.

Ujenzi wake ulikumbwa na wasiwasi mara kadha kuhusu usalama wake.

Maafisa wanasema watu zaidi ya 18 walifariki wakati wa kujengwa kwa daraja hilo.

Rais Xi alihudhuria sherehe ya kuzindua daraja hilo ambayo imefanyika jijini Zhuhai, akiwa pamoja na viongozi wa Hong Kong na Macau.

Aerial view of Hong Kong-Zhuhai-Macau Bridge West Artificial Island

Moja kati ya visiwa bandia vilivyojengwa 

Magari yataruhusiwa kuanza kulitumia Jumatano. Linaunganisha miji mitatu muhimu kusini mwa China – Hong Kong, Macau na Zhuhai.

Daraja hilo, ambalo limejengwa kuhimili mitetemeko ya ardhi na vimbunga, ilijengwa kwa kutumia tani 400,000 za chuma, chuma zinazotosha kujenga minara 60 sawa na mnara maarufu wa Eiffel jijini Paris.

Takriban 30km ya urefu wake umepitia baharini kwenye mlango wa Mto Pearl.

Ili kuwezesha meli kupita chini ya daraja hilo, kuna sehemu ya urefu wa 6.7km ambapo daraja hilo linaingia chini ya bahari na kupitia kati ya visiwa viwili vya kujengwa na binadamu na hivyo kuwa kama njia ya chini kwa chini baharini.

Maeneo yaliyosalia yanaunganishwa kwa barabara, njia za kuondosha maji na barabara za chini kwa chini kukamilisha kuunganisha kikamilifu miji ya Zhuhai na Hong Kong na daraja hilo.

Ni sehemu ya mpango wa China wa kujenga kinachoitwa Greater Bay Area (Eneo Kubwa la Ghuba), ambalo litajumuisha Hong Kong, Macau na miji mingine tisa kusini mwa China.

Eneo hilo kwa sasa lina wakazi 68 milioni, zaidi ya raia wote wa Tanzania au Kenya pia.

Zamani, mtu kusafiri kati ya Zhuhai na Hong Kong angechukua saa nne kukamilisha safari hiyo. Lakini sasa daraja hilo litapunguza hilo hadi kuwa dakika 30 pekee.

Graphic: Bridge and tunnel cross-section and location map

Unaruhusiwa kuendesha gari darajani?

La hasa. Ndipo uweze kuendesha gari lako kwenye daraja hilo, unahitaji kibali maalum, ambacho kitakuwa vinatolewa kwa watu kwa vipimo.

Aidha, magari yote yatalipa ada kuruhusiwa kutumia daraja hilo.

Katika hilo halijafunguliwa kutumiw ana magari ya uchukuzi wa umma, hivyo ni mabasi ya kibinafsi ambayo yatakuwa yanawasafirisha watu

Aidha, hakuna reli inayopitia kwenye daraja hilo.

Maafisa awali walikuwa wamekadiria kwamba magari 9,200 yangekuwa yanalitumia daraja hilo kila siku.

Baadaye walishusha makadirio yao baada ya barabara mpya na miundo mbinu ya usafiri kujengwa eneo hilo.

Watu wanasema nini?

Kumekuwa na ukosoaji mkubwa wa mradi huo.

Daraja hilo lilikuwa limeelezwa na baadhi ya vyombo vya habari kama ‘daraja la mauti’.

Watu zaidi ya tisa walikuwa wamefariki upande wa Hong Kong wakati wa kujengwa kwa daraja hilo, na maafisa waliambia idhaa ya Kichina ya BBC kwamba watu tisa walifariki upande wa China.

Mamia ya wafanyakazi walijeruhiwa pia wakati wa ujenzi wa daraja hilo.

Kumekuwa pia na wasiwasi kuhusu athari zake kwa mazingira.

Makundi ya kutetea uhifadhi wa mazingira yanasema mradi huo huenda umeathiri sana viumbe wa baharini, ikiwa ni pamoja na pomboo weupe wa China ambao huwa nadra sana kupatikana.

Idadi ya pomboo wanaoonekana katika bahari ya Hong Kong wamepungua kutoka 148 hadi 47 katika miaka 10 iliyopita, na kwa mujibu wa tawi la Hong Kong la shirika la World Wide Fund for Nature (WWF) hakuna pomboo aliyeonekana karibu na daraja hilo.

“Mradi huu umefanya madhara makubwa sana kwa bahari,” alisema Samantha Lee, Mkurugenzi msaidizi wa Uhifadhi wa Bahari katika WWF.

“Nina wasiwasi kwamba idadi hii haitaongezeka tena.”

Kwa pamoja, daraja hilo na barabara zinazoliunganisha na miundo mbinu mingine, pamoja na visiwa bandia vilivyojengwa baharini viligharimu $20bn. Daraja kuu lenyewe liligharimu $6.92bn.

Maafisa wa serikali nchini China wanasema daraja hilo litachangia kuuzalishia uchumi wa China yuan trilioni 10 ($1.44tn; £1tn), lakini mmoja wa wabunge Hong Kong ametilia shaka hilo.

“Sina uhakika kwamba daraja hilo linaweza kujiendeleza kwa gharama iwapo si magari mengi yatakuwa yanalitumia, alisema Tanya Chana alipozungumza na BBC.

“Nina uhakika kwamba hakuna vile tutaweza kupata tena gharama iliyotumiwa kwa ujenzi.”

Kwa mujibu wa makadirio ya Idhaa ya Kichina ya BBC, daraja hilo litakusanya ada ya jumla ya $86m kwa kuwatoza wanaolitumia.

Lakini gharama ya kulisimamia na kufanya ukarabati inatarajiwa kuchukua karibu theluthi moja ya mapato yatakayokusanywa kupitia tozo hiyo.

Wakosoaji wanasema daraja hilo halitakuwa na mafao yoyote kwa uchumi, na wengine wanasema lengo muhimu ni kuhakikisha Hong Kong inaunganishwa na China bara.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents