Tragedy

Auawa akigombea dumu tupu la lita 40

WATU wawili wameuawa katika matukio mawili tofauti mkoani Mara huku raia wawili kutoka Ethiopia na Mtanzania aliyekuwa anawavusha kutoka Kenya, wamekamatwa na Polisi wa Wilaya ya Tarime.

Makubo Haruni, Tarime

 

WATU wawili wameuawa katika matukio mawili tofauti mkoani Mara huku raia wawili kutoka Ethiopia na Mtanzania aliyekuwa anawavusha kutoka Kenya, wamekamatwa na Polisi wa Wilaya ya Tarime.

 

Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Mara, Nonosius Komba amewataja waliokufa kuwa ni Kosam Marwa (32), mkazi wa Mgango Musoma ambaye alipigwa na kuchomwa moto, mwingine ni Jackson Makorere mkazi wa Kewanja aliyeuawa kwa kupigwa jiwe kichwani na Kichuchura Marwa (18), anayeshikiliwa na Polisi wakigombea dumu tupu la ujazo wa lita 40.

 

Alisema kwa njia ya simu kuwa katika tukio la kwanza, Kosam Marwa aliuawa na wananchi wa Kijiji cha Ruhu katika wilaya mpya ya Rorya kwa kupigwa mawe na kuchomwa moto kwa tuhuma za kuvunja kibanda cha Veronica Beatus na kupora mashine tatu za kunyolea nywele, nguo, cherehani, vitenge, shuka na kanda za radio mbili.

 

Komba alisema baada ya wizi huo uliotokea Septemba mosi mwaka huu, Kosam alikutwa anaviuza mnadani na alipoulizwa na wananchi kwamba alivipata wapi, alikiri kuwa aliviiba kibandani hapo ndipo walipompiga hadi kufa.

 

Tukio hilo la watuhumiwa wa wizi kuuawa limetokea mara ya pili kwa muda usiozidi wiki moja kutokana na watuhumiwa watatu wa wizi wa mifugo waliouawa na wakazi wa Kijiji cha Deti Kata ya Nyathorogo katika Wilaya ya Rorya baada ya kukutwa na ng’ombe wanne mali ya Thobias Okuge wa kijiji cha Deti.

 

Katika tukio la pili, Kaimu Kamanda Komba alisema lilimhusu Makorere ambaye alikufa baada ya kupigwa kwa jiwe kichwani wakati akigombea dumu tupu lililodaiwa kutumika kufanyia jaribio la kuibia dizeli katika mgodi wa North Mara.

 

Kamanda Komba alisema baada ya kupigwa jiwe kichwani, alikimbizwa hadi Hospitali ya Nyangoto ambako alikufa wakati anapata huduma ya matibabu na mtuhumiwa Kichuchura amekamatwa na atafikishwa mahakamani muda wowote.

 

Wakati huo huo, Komba alisema Polisi wilayani Tarime jana alfajiri majira ya saa 11 iliwakamata Waethiopia wawili na Mtanzania mmoja wa Kijiji cha Nkongole wilayani humo katika kizuizi kilichopo Kijiji cha Gamasara, wakivushwa kwa miguu.

 

Aliwataja waliokamatwa kuwa ni Asefa Bera (20), Abaynes Lerago (39) ambao ni Waethiopia na Mtanzania aliyekuwa amewavusha aitwaye Nicodemas Joseph.

 

Kamanda Komba alisema atawapeleka Uhamiaji kwa maandalizi ya kushitakiwa kuingia nchini kinyume cha sheria.

 

Source: Habari Leo

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents