Habari

‘Diana alitaka kuwasaidia watoto wa Tanzania’

WAKATI Waingereza wakiwa katika wiki ya maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 10 tangu alipofariki dunia aliyekuwa mke wa mrithi wa kiti cha ufalme wa Uingereza, Diana Spencer’Princess Diana’, imebainika kuwa Tanzania inafaidika na miradi iliyoanzishwa baada ya kifo chake

Na Hassan Abbas, London


WAKATI Waingereza wakiwa katika wiki ya maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 10 tangu alipofariki dunia aliyekuwa mke wa mrithi wa kiti cha ufalme wa Uingereza, Diana Spencer’Princess Diana’, imebainika kuwa Tanzania inafaidika na miradi iliyoanzishwa baada ya kifo chake na endapo angekuwa hai alikuwa na kiu ya kuwatembelea watoto wa Tanzania wanaoishi katika mazingira magumu.


Siri hiyo ilibainishwa jijini hapa na Mkuu wa Masuala ya Mawasiliano na Miradi katika Mfuko Maalumu wa Kumbukumbu ya Princess Diana (Diana Memorial Fund), Bw. Paul Hensby, alipofanya mahojiano maalumu na mwandishi wa habari hizi mwishoni mwa wiki iliyopita.


Bw. Hensby alitoboa siri kuwa marehemu Princess Diana si tu alitaka kutembelea Tanzania na kutoa misaada, bali pia tayari nia yake hiyo ambayo ilikatishwa na kifo akiwa Paris Agosti 31, 1997, sasa malengo yake yametimizwa kwa Mfuko huo kutumia kiasi cha pauni 150,790 kuanzia mwaka 2004 katika miradi ya afya wilayani Muheza, Tanga.


“Diana kama angekuwa hai leo, angependa kutembelea Tanzania na hasa Muheza ambako tayari kuna miradi yake ya kusaidia afya ya jamii. Angependa kukutana na watoto wa huko na kuangalia wanaendeleaje kiafya, kuwapa upendo wake, kuwapa moyo na kutumia ushahiwshi wake katika kuhakikisha wanapata misaada ya afya,” alisema.


Akaongeza: “Angependa pia kutumia ushawishi wake kuhakikisha kuwa huduma za elimu na afya katika maeneo ya Tanzania vinaimarishwa.”


Kwa mujibu wa takwimu za Mfuko huo, mradi wa afya wa Muheza unahudumia watu wapatao 60-70 kwa wiki na pia kuna klabu ya watoto kwa ajili ya kupewa stadi za maisha na namna ya kujikinga na ugonjwa wa UKIMWI.


Pia mradi huo unahusisha huduma za ushauri wa majumbani ambapo wataalamu wa masuala ya tiba wanazungumza na wanafamilia nyumba kwa nyuma kuhamasisha watu kupima virusi vya UKIMWI.


Bw. Hensby alisema Princess Diana atakumbukwa daima kwa sababu nyingi, lakini ukiwamo ushujaa wake wa kujitokeza mstari wa mbele kusaidia maskini na watoto waishio katika mazingira magumu.


Kwa wiki nzima sasa, tangu Ijumaa iliyopita, Jiji la London na maeneo mengine ya hapa, limekuwa katika shughuli mbalimbali zinazoashiria kuwa hata baada ya miaka 10 sasa, Diana bado anakumbukwa.


Mbali ya misa takatifu iliyofanyika wiki iliyopita na kuhudhuriwa na Malkia Elizabeth II, watoto wa Diana, William na Harry na watu wengine mashuhuri, picha za Diana zimekuwa zikionekana katika baadhi ya maeneo na kupamba magazeti.


Source: Majira

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents