Michezo

Azam FC yamaliza rasmi na Stewart Hall

Klabu ya Azam FC, imeachana rasmi na aliyekuwa Kocha Mkuu wake, Stewart Hall, baada ya kufanyika makubaliano ya pande zote mbili.

hall-stewart-kocha-wa-azam-fc

Uongozi wa Azam FC umechukua hatua hiyo kufuatia hivi karibuni Hall kutangaza uamuzi wa kuachia ngazi akiweka wazi kuwa amechoka kufundisha soka Tanzania na sasa anataka kwenda kutafuta changamoto nyingine mpya ya kufundisha soka nje ya nchi.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu ya azamfc.co.tz Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba, alisema mara baada ya kukaa meza moja na Hall wamekubaliana kwa pamoja juu ya ombi lake hilo huku akieleza kuwa kwa sasa kikosi hicho kitakuwa chini ya Kocha Msaidizi Dennis Kitambi.

Alisema Kitambi atakinoa kikosi hicho katika mechi mbili zilizobakia msimu huu, ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Mgambo JKT itakayofanyika Jumapili hii (Mei 22) pamoja na ile ya fainali ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) watakayokipiga na Yanga Juni 11 mwaka huu.

“Leo tumeachana na Hall kwa makubaliano ya pande zote mbili baada ya kutuomba kuachia ngazi kwa lengo la kutafuta changamoto nyingine nje ya nchi, wakati tukijipanga kuunda benchi jipya la ufundi kwa sasa timu itakuwa chini ya Kocha Msaidizi Dennis Kitambi hadi kumalizika kwa msimu huu,” alisema.

Kawemba pia alichukua fursa hiyo kumpongeza Hall kwa mafanikio aliyoipa timu hiyo kwa muda mchache aliofanya kazi ndani ya Azam FC huku akimtakia kila la kheri katika timu nyingine atakayokwenda kuifundisha.

“Tunamshukuru Hall kwa mafanikio aliyotupa msimu huu, kwanza kutupa ubingwa wa Kombe la Kagame, kuingia fainali ya Kombe la FA na sasa tukiwa nafasi ya pili kwenye ligi, hii ni rekodi nzuri na tunamshukuru sana kwa hilo na tunapenda kumtakia kila la kheri katika timu nyingine atakayokwenda kufundisha,” alisema.

Rekodi ya Hall Azam FC
MECHI 62
SHINDA 41
SARE 16
POTEZA 5
Hii ni tokea alipotua Azam FC Juni, 2015.

MABAO YA KUFUNGA 111
MABAO YA KUFUNGWA 41
BILA KUFUNGWA (Mechi 31)

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents