Bongo5 Makala

Makala: Kala Jeremiah ni yule yule kwa kasi ya 4G

Ukiachilia mbali wimbo wa Taifa la Tanzania tunaoufahamu, rapper Kala Jeremiah aliwashawi kuandika ngoma yake na kuipa jina la Wimbo wa Taifa. Hii ni kutokana na maudhui mapana ya ngoma hiyo ambayo kwa namna moja au nyingine kila mwananchi kuna mtari unamgusa.

Baada ya Kala kulijenga jina lake vilivyo kupitia ngoma hiyo kilichofuata ni kuwa daraja kati ya wananchi na serikali. Kazi ya daraja hili ni kupitisha hoja kutoka kwenye kijamii kwenda serikalini, pia kupitisha elimu kwenda kwenye jamii.

Nisikuchoshe

October 10 mwaka huu Kala Jeremiah alitoa ngoma mpya ‘Vijana’ baada ya ukimya wa zaidi ya mwaka mmoja tangu atoe ngoma ‘Wanandoto’. Binafsi nimesikiliza kwa makini kile alichokileta kwa sasa na kulinganisha na kazi kubwa aliyokwisha kuifanya huko nyuma nikagundua Kala ni yule yule.

Twende pole pole, narudia tena; Kala ni yule yule na kwa msisitizo naongeza ni yule yule kwa kasi ya 4G. Ngoma ya Vijana amezunguzia mambo mengi ila tuyachambue haya manne (4G).

  1. Ukosefu wa ajira kwa vijana

Katika verse zote Kala kazunguza mambo mengi kwa mistari mingi yenye kila aina ya ufundi katika uwasilishaji wake, licha ya uwezo kutiririka na vina na kunata na beat bado tatizo la ukosefu wa ajira ni kitu kisichoweza kuufunga mdomo wake. Anasema hivi;

Je upo mtaani na unataka utajiri, je unasubiria mpaka waje wakuajiri/

Kwanini usijiajiri, kwanini usianzishe hata kibanda cha asali/

Kwanini msianzishe kikundi cha kushona, kikundi cha kuvyatua tofali za kuchoma/

Kuna fursa nyingi mbona, kama upo shule ongeza bidii kusoma/

Mwaka 2014 katika Jiji la Lagos nchini Nigeria walifariki vijana 20 katika mkanyagano, vijana hao ni miongozi mwa vijana 120,000 waliohudhuria usahili wa nafasi za kazi 4, 000 zilizotangazwa na uhamiaji wa nchini hiyo.

Tukio hilo lilidhihirisha kuwa tatito la ukosefu ajiri ni kubwa katika nchi hiyo, hata hivyo si kwa Nigeria pekee bali hata Tanzania. August mwaka huu tumeshuhudia hapa nchini vijana 56,000 wakijitokeza katika ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuwania nafasi 400 za ajira zilizotangazwa hapo awali.

Hivyo basi msanii akiwa kama kioo cha jamii ni wajibu wake kuwa sehemu ya utatuzi wa changamoto hiyo, aidha kwa kutoa ajira, kushauri na kutoa elimu. Hadi kufikia hapo Kala kwa kiasi kikubwa ametekeleza wajibu wake.

      2. Vijana na uongozi

Rapper wa kundi la Weusi, Nikki wa Pili hivi karibuni kupitia mtandao wa twitter aliandika, ‘watu wenye mawazo tofauti hawana nafasi pahali ambako watu hawapendi kufikiri tofauti’

Katika makundi matatu yaliyopo katika jamii, yaani watoto, vijana na wazee, ni kundi lipi linafikiri tofauti zaidi?, bila shaka ni vijana. Hata hivyo ni vijana wachache sana ambao wapo katika mfumo wa kutoa mawazo yao na kuweza kufanyiwa kazi na serikali, Kala Jeremiah analigusia hilo katika ngoma yake.

Na nyie viongozi wape nafasi vijana, siyo mpaka uzoefu au za kujuana/

Kala anamaanisha vijana wapewa nafasi za uongozi katika ngazi yoyote ile kwani kufanya hivyo ni mwanzo wa kuleta mawazo mapya yatakayoibua hoja, sera, utekelezaji na hatimaye maendeleo kwa kila mmoja.

Rais anayemaliza muda wake sasa nchini Liberia, Ellen Johnson-Sirleaf ambaye amekuwa Rais wa kwanza mwanamke barani Afrika toka mwaka 2005, inaelezwa katika uongozi wake aliwatumia sana vijana akiamini kuwa kufanya hivyo kutaisaidia nchi hiyo kuendelea baada vita vya muda mrefu.

       3. Dawa za kulevya na vijana

Mwaka 2012 ulimwengu ulipata mshtuko mkubwa kufuatia kifo cha msanii mashuhuri, mrembo na mwenye sauti ya kipekee, Whitney Houston wa Marekani. Hit songs kama I will Always Love You, Save All My Love for You, I have Nothing, My Love Your Love na nyinginezo kibao zilitoka wake.

Kwa mujibu wa madaktari nyota ya muimbaji huyo ilizimwa na matumizi ya dawa za kulevya. Si wasanii wa Marekani pekee wanakumbana na hili hata wa Bongo Flava pia na wale wasiyo wasanii. Kala ameliona hilo katika ngoma yake.

Usibebeshwe unga na bosi utaitwa punda, na dili zikadunda/ hamia kwenye siasa mbona fursa zimejaa/

Hivyo Kala anekuwa sehemu ya utatuzi wa tatizo hilo, nakumbuka February 12 mwaka huu wakati Rais Dkt. John Magufuli akimwapisha Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, Rogers William Siyanga alisema takwimu zinaonyesha Watanzania 1,007 wamekamatwa na kufungwa katika nchi mbalimbali kutokana na kujihusisha na biashara hiyo haramu.

      4. Dear God bado yupo na Kala/vijana

Dear God ni hit song iliyompa Kala mafanikio makubwa ikiwemo kushinda tuzo tatu za KTMA, katika ngoma hiyo alizungumzia uhusiano wake na Mungu kitu ambacho amekuwa akikirudia mara nyingi katika ngoma zake.

Albamu yake Pasaka inajimbanua vya kutosha katika hilo, katika ngoma hii vijana amegusia tena hilo.

Usisahau kusali maana bila maombi hutavuka mstari, dunia ina mengi/

Katika kitabu kitwacho How to deal with stubborn habits, sura ya sita ya kitabu hicho inazunguzmia mada ‘gratitude and prayer’, kwa tafsiri ya lugha ya Kiswahili, ‘Shukrani anazopewa Mungu (kwa ajili ya uumbaji, watu wengine, wewe mwenyewe) pamoja na kuomba.

Kitabu hiki ambacho kinazungumzia saikolijia kinaelezea kuwa kuna faida kadhaa anazopata mwanadamu kwa kumjua Mungu ambaye ni Muumba wake.

Nitamatishe: Vitu vinne nilivyoangazia ni vichache sana, ukizingatia wimbo wenyewe una dakika 5: 17, hivyo alivyozungumza ni elimu pana kwa wale aliowakusudia kuwafikishia ujumbe huo.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents