Bongo5 Makala

Makala: Saini ya Mbosso na vyuma kukaza WCB (+Audio)

Ukichilia mbali uzinduzi wa albamu ya A Boy From Tandale, kitu kingine kikubwa ambacho kilikuwa kinasubiriwa kutoka kwa Diamond Platnumz kwa mwaka huu ni utambulisho wa msanii Mbosso ambaye kwa kipindi kirefu ilikuwa ikielezwa kuwa yupo chini ya usimamizi wa WCB.

Sekunde zikapuputika, dakika zikayoyoma, siku zikasonga na hatimaye usiku wa January 28, 2018 label ya WCB inayomilikiwa na Diamond Platnumz ikatangaza rasmi kuwa Mbosso ni msanii wao.

Ni kabla hata albamu ya A Boy From Tandale haijaingia sokoni, WCB wakaongeza idadi ya wasanii ndani ya label yao na kufika saba mara baada ya hapo awali kuwasaini wasanii kama Harmonize, Rayvanny, Queen Darleen, Rich Mavoko na Lava Lava.

Hatua hii ni kitu ambacho kiliweka alama nyingine kubwa katika maisha ya kimuziki ya Mbosso katika maeneo makuu mawili;.

Mosi; kutoka Yamoto Band hadi WCB, utakumbuka Mbosso ni miongoni mwa wasanii waliokuwa wakiunda kundi la Yamoto akishirikiana na kina Aslay, Beka Flavour na Enock Bella. Baada ya kundi hilo ‘kuvunjika’ kila mmoja alianza kufanya kazi pekee yake (solo artist).

Katika wasanii wale wanne Mbosso pekee ndiye aliyeonekana kupata shavu zaidi kwa upande wa usimamizi kwani WCB ni label kubwa ambayo wasanii wengi wangetamani kuwepo hapo.

Sababu ya pili; Ni kutoka Maromboso hadi Mbosso, alipokuwa Yamoto Band alikuwa akifahamika kama Maromboso ila alipokubali kuwa chini ya WCB alibadili jina na kuwa Mbosso. Ni wasanii wachache wenye uthubutu huo na ukizingatia jina lilikuwa brand tayari.

Mbosso anaweza kuja kusahau idadi ya nyimbo alizonazo, anaweza kusahau hata baadhi ya mashairi ya nyimbo zake ila hawezi kusahau hatua ya kutoka Yamoto Band hadi WCB na kitendo cha kubadili jina lake.

Kabla Vyuma Kukaza

Miezi kadhaa iliyopitia kuliibuka maneno (misimu) ‘Vyuma Vimekaza’ yakimaanisha kukosekana kwa fedha mifukoni mwa watu au watu kupitia hali ngumu kimaisha, hata hivyo Rais John Magufuli alikemea kuenezwa kwa ‘mtazamo’ huo kwa kueleza uchumi wa nchi bado upo katika hali nzuri. Tuachane na hilo.

September 3, 2017 kupitia mtandao huu niliandika makala yenye kichwa, ‘Kupitia ‘Zilipendwa’ huenda Diamond kamalizana na Lava Lava, Queen Darleen‘. Nilieleza jinsi kila msanii anayesainiwa WCB anavyopata fursa au urahisi wa kufanya kolabo na Diamond.

Utakumbuka Harmonize baada ya kusaini WCB wimbo wake wa pili kutoa ‘Bado’ alimshirikisha Diamond baada ya kutoka na ngoma ‘Iyola’. Baada ya Harmonize msanii mwingine kusainiwa katika lable hiyo alikuwa Rayvanny ambaye ngoma yake kwanza kutoa ilikwenda kwa jina la Kwetu.

Baada ya Kwetu ngoma iliyofuata ilikwenda kwa jina la Natafuta Kiki, kisha kufuata kolabo na Diamond Platnumz ‘Salome’.

Hata Rich Mavoko aliposaini WCB akiwa kama msanii wa tatu ngoma yake pili kutoa ni ‘Kokoro’ aliyomshirikisha Diamond, hivyo utaona kila aliyesaini alikuwa na bahati katika kolabo na Diamond, kama ni vyuma kukaza basi vilipata grisi kwa wakati huo.

Vyuma kukaza

Hata hivyo hali ikawa tofauti kidogo kwa Lava Lava na Queen Darleen waliofuata hapo baadaye. Kupitia ngoma ‘Zilipendwa’ iliyokutanisha wasanii wote wa WCB akiwemo Mbosso ambaye alikuwa bado hajatambulishwa rasmi ni wazi ilikuja kuondoa uwezekana wa wasanii hao kuja kufanya kazi na Diamond.

Ndicho nakiona kwa Mbosso kwa sasa, huwenda safari yake ikawa ngumu (vyuma kukaza) ukilinganisha na walivyoanza Harmonize, Rayvanny na Rich Mavoko.

Ngoma ya kwanza kutoa ni Watakubali ambayo aliitoa usiku wa January 28, 2018 mara baada ya kusaini WCB. Baada ya hapo alifanya media tour ya kibabe zaidi mikoani, nafikiri kuliko wasanii wote wa mwanzo kusaini WCB, hii ni kutokana na kile kilichotokea. Nitakieleza hapo mbeleni.

February 9, 2018 Mbosso alitoa ngoma ya pili ‘Nimekuzoea’ kisha kufuatia ngoma nyingine kama Picha Yake na Alele. Hadi hapa alipofikia Mbosso ingekuwa kipindi cha kina Harmonize, Rayvanny na Rich Mavoko, tungekuwa tunasikiliza kolabo yake na Diamond Platnumz.

Baada ya Mbosso kutoa ngoma ‘Watakubali’ alifanya media tour ya nguvu mikoani kwa kusukuma muziki wake. Hii ni baada ya baadhi ya vyombo vya habari Dar es Salaam kuacha kucheza kazi za Diamond na wasanii wote waliochini ya WCB.

Msanii anategemea media kama sehemu ambayo itamsaidia kufikisha bidhaa yake (muziki) kwa wanunuzi ambao ndio mashabiki wake, hivyo Mbosso alijaribu kuzikifikia media nyingi za mikoani ili kuweza kuwafiki mashabiki wake kitu ambacho amefanikiwa kwa kiasi kikubwa.

Vyuma vimepata Grisi

Kipindi ambacho Mbosso anafanya media tour mikoani boss wake, Diamond Platnumz anatangaza kufungua media yake (Wasafi TV & Radio), hazikupita siku nyingi Wasafi TV ikaanza kurusha matangazo yake.

Sasa ngoma za Mbosso zinachezwa Wasafi TV, tunaweza kusema inapunguza kwa kiasi fulani tatizo kama lilikuwepo baada ya kile kilichotokea mwanzo. Ninaposema vyuma vimepata grisi kwa upande wa Mbosso ni kweli vimepata.

Miezi miwili iyopita, yaani March 05 2018 Diamond Platnumz aliachia kipande cha wimbo mtandaoni ambao amemshirikisha Mbosso, bado haijajulikana ni lini hasa ngoma hiyo itatoka rasmi. Ngoma hiyo kutoka kutamfanya Mbosso kuwa sawa na kina Harmonize, Rayvanny na Rich Mavoko kama nilivyoeleza hapo mwanzo ingawa hadi sasa inaonekana kuchelewa ukilinganisha na hao watatu.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents