Habari

Mbeya: Akutwa akifukua kaburi la albino

Mkazi wa kijiji cha Chapakazi, Mbalizi mkoani Mbeya, Jonas John (28) anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani hapo, baada ya kukamatwa akifukua kaburi la mtu mwenye ualbino, aliyefariki a kuzikwa kijijini Mumba mwaka 2010.


Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Mbeya, Dhahir Kidavashari.

Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Mbeya, Dhahir Kidavashari, alisema John alikamatwa katika kijiji Mumba kata ya Ilembo, Tarafa ya Isangati Wilaya ya Kipolisi Mbalizi, mkoani humo saa 7 usiku jana.

Kijana huyo alikamatwa na askari akiwa na wenzake wawili, wakifukua kaburi la mtu aliyefahamika kwa jina la Sister Osisara, aliyekuwa mlemavu wa ngozi (albino) kwa lengo la kuchukua viungo vyake.

Kamanda alisema mtuhumiwa alikutwa na majembe na koleo, ambayo walikuwa wakiyatumia kufukulia kaburi hilo usiku huo, kabla ya wakazi wa maeneo ya jirani na makaburi hayo kubaini kilichokuwa kikiendelea na kutoa taarifa.

Alisema baada ya mtuhumiwa kukamatwa na kuhojiwa na polisi, aliwataja washirika wenzake wawili, ambao walikimbia baada ya kuwaona askari. Kamanda Kidavashari alisema msako unaendelea, kuwatafuta watuhumiwa wawili waliokimbia.

“Wenzie wawili walikimbia kwa kuwa ilikuwa rahisi kwao kuwaona polisi kwani walikuwa nje, huyu mwenzao aliyekamatwa akiwa ndani ya kaburi,” alisema Kamanda Kidavashari. Aliwataka watu au mtu yeyote aliye na taarifa, juu ya walipo watu hao, kutoa taarifa kwa vyombo vya ulinzi na usalama ili hatua zichukuliwe dhidi yao.

Taarifa zaidi kutoka kwa baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo, zinaeleza kuwa mtuhumiwa alikutwa ndani ya kaburi akiwa amemaliza kazi ya kutoa udongo.

BY: EMMY MWAIPOPO

CHANZO: HABARILEO

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents