Habari

MWANZA: Maambukizi ya VVU yapanda, yadaiwa kundi la vijana liko kwenye hatari zaidi 

MAAMBUKIZI ya virusi vya Ukimwi kwa Mkoa wa Mwanza yamepanda kutoka asilimia 4.2 mwaka 2012 hadi 7.2 mwaka 2017.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella, alisema hayo wakati akifungua maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani yaliyofanyika katika Uwanja wa Rock City Mall jijini Mwanza, jana.

“Kiwango cha maambukizi kwa sasa kimekua kwa kasi sana kutoka asilimia 4.2 hadi 7.2, si jambo jema,” alisema.

Alisema taarifa zinaonyesha kundi la vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 24 ndiyo liko kwenye hatari zaidi.

Kwa mujibu wa Nipashe, Mongella alisema maeneo ya visiwani ni hatarishi kutokana na asili na shughuli inayofanyika na kuwataka Watanzania kuungana kupiga vita kwa kuchangia mfuko wa udhamini wa kudhibiti Ukimwi.

“Ukimwi sio mwisho wa maisha, hakuna sababu ya wewe kujinyanyapaa, kwanza wewe mwenyewe na pili jamii, tuondokane na huu ushamba, tuende kwenye hatua inayofuata,” alisema Mongella.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi, Dk. Leornad Maboko, alisema mfuko huo umewezesha kupatikana kwa Sh. bilioni 12 kwa ajili ya shughuli ya kudhibiti Ukimwi kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa kazi ambayo inatarajiwa kuanza mwanzoni mwa mwaka ujao.

Alitaja namba ya kuchangia mfuko huo kwa ajili ya shughuli ya kusaidia kupunguza maabukizi ya virusi vya Ukimwi kwa mtu yeyote mwenye moyo wa kuchangia kuwa ni 0684909090.

Amewasihi wananchi wa Mkoa wa Mwanza kufika kwenye mabanda kwa ajili ya kupima saratani ya shingo ya kizazi, ya matiti, na kisukari.

Alisema maambukizi ya virusi vya Ukimwi kitaifa yanazidi kupungua kwa mwaka kutoka zaidi ya watu 100,000 miaka 10 iliyopita na kufikia maambukizi 72,000 kwa mwaka.

Mwenyekiti wa Baraza la watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi nchini (NACOPHA), Letisia Morris, aliiomba serikali kuelekeza mapambano dhidi ya ununuzi wa vifaa tiba, na utoaji wa elimu ya matumizi ya dawa za kufubaza virusi hivyo (ARV) na wanaume kujitokeza kupima kujua kama wanaishi na virusi hivyo.

“Unyanyapaa ni tishio kubwa kuliko hata VVU na Ukimwi, tupige vita unyanyapaa, hakuna sababu ya kumnyanyapaa mtu anayeishi na virusi vya Ukimwi…kwa jamii tupige vita unyanyapaa dhidi ya watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi na utakapopima ukaonekana una maambukizi anza tiba mapema, sisi huwa tunasema ‘ongeza salio ili mawasiliano yawepo’,” alisema Letisia.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kivulini, Yasin Ally, alisema hofu ya vijana wa sasa sio Ukimwi wala magonjwa ya zinaa bali ni mimba.

“Wengi wamediriki kujifungia njiti shuleni kwa ajili ya kukwepa mimba kuliko Ukimwi na magonjwa ya zinaa, takwimu inaonyesha maambukizi mapya kwa vijana wa miaka 15 hadi 24 ni asilimia 40, hapa wadau wa ukatili na Ukimwi ni lazima tutafakari tunabadilishaje mbinu kwanini hofu ya vijana hawa ambayo ni waathirika wakubwa ni mimba na sio Ukimwi na sio magonjwa ya zinaa,” alihoji Ally.

Kaulimbiu ya maadhimisho hayo ni ‘Jamii ni chachu ya mabadiliko tuungane kupunguza maambukizi mapya ya VVU”

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents