Michezo

Niliahidi siku mwalimu akinipa nafasi lazima nimwonyeshe – Kimwaga

 

Winga wa Azam FC, Joseph Kimwaga ameweka wazi kuwa atahakikisha anakuwa vizuri zaidi hii ni kufuatia kufunga mabao mawili kwenye mechi yake ya kwanza msimu huu.

Kimwaga  amekuwa nje ya uwanja tangu Agosti 24 mwaka jana kufuatia kupata majeraha ya goti kwenye Uwanja wa Chuo cha Ualimu cha TTC mkoani Mtwara, wakati timu yake ya Azam FC ikijiandaa na mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Ndanda uliomalizika kwa ushindi wa bao 1 – 0.

Mabao hayo mawili Kimwaga alifunga juzi wakati Azam FC ikiichapa Friends Ranger mabao 5-0 kwenye mchezo wa kirafiki, mengine yakifungwa na kiungo Salmin Hoza, mshambuliaji Mbaraka Yusuph na winga Enock Atta kwa njia ya mkwaju wa penalti.

Winga huyo ameuambia mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz kuwa wachezaji anaogombania nao namba wako fiti kuliko yeye hivyo atahakikisha anajiweka vizuri zaidi.

“Kwanza kabisa namshukuru Mwenyezi Mungu amenijalia nimepona vizuri, pili nashukuru benchi la ufundi kwa kunipa nafasi leo (juzi) tatu nashukuru wachezaji wenzangu kwa sababu tumeshirikiana vizuri tumefanikisha timu imeshinda,” alisema.

Akizungumzia mabao yake mawili aliyofunga, Kimwaga alisema kuwa: “Kwangu ni jambo jema kwa sababu ni kitu ambacho nilikuwa siku zote nawaza, siku mwalimu akinipa nafasi lazima nimwonyeshe.”

Aidha kabla Kimwaga hajaumia mwaka jana, alikuwa kwenye kiwango kizuri na hivi sasa amerejea na moto jambo ambalo linaashiria dalili njema za kuendelea kufanya vizuri katika mechi nyingine zijazo atakazopewa.

Kikosi cha Azam FC, kitarejea mazoezini leo saa 12 jioni kuanza maandalizi ya mchezo ujao wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) dhidi ya Mtibwa Sugar utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex Jumamosi hii saa 1.00 usiku.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents