Burudani

Nuru The Light: Kipaji kilichokuzwa na James Dandu na kuweka historia nchini Sweden (Audio)

Nuru the Light, ni msanii wa Tanzania ambaye kama lilivyo jina lake, mwanga wa kipaji chake cha muziki uliimulika jamii ya Watanzania na kuitangaza vizuri ughaibuni, hususan nchini Sweden alipokuwa akiishi na familia yake kwa miaka mingi.

Nuru The Light2

Msanii huyo ambaye Tanzania inamfahamu zaidi kwa nyimbo zake za RnB na Bongo Flava zikiwemo Walimwengu, ‘Muhogo Andazi’ aliomshirikisha Bob Junior, na Nsubiri Usilale aliouachia mwaka juzi, kipaji chake kiligunduliwa na moja kati ya ‘Icon’ wa muziki wa Kiswahili Tanzania, Marehemu James Dandu aka Cool James Massive au Mtoto wa Dandu miaka takriban 15 iliyopita nchini Sweden.

Nuru the Light ambaye wiki hii ameachia wimbo wake mpya na mkali alioupa jina la ‘L’ ambao video yake itazinduliwa hivi karibuni, ana kila sababu za kumkumbuka kwa heshima marehemu James Dandu.

Anakumbuka akiwa na umri wa miaka 16 ambapo alikutana na James Dandu nchini humo. Dandu aligeuka kuwa baraka iliyokuza kipaji chake na kwa muda mfupi alivunja rekodi kwa kuwa msanii wa kwanza mwenye umri mdogo zaidi Tanzania kusaini mkataba wa kufanya kazi na kampuni kubwa ya muziki ya Stockholm Records iliyoko jijini Stockholm, Sweden.

“I think mimi ni msanii mdogo zaidi wa Tanzania ambaye nilikuwa signed kwenye lebel rasmi ya muziki ever in history,” anasema Nuru The Light kwenye kipindi cha Chill na Sky.

Kwa mujibu wa Nuru, kaka yake ndiye aliyekuwa mtu wa kwanza kushawishiwa na James Dandu afanye muziki kwa kuwa alikuwa ana nia ya kutengeneza kundi la wasanii kadhaa nchini Sweden na alipenda mmoja kati ya wasanii hao awe Mtanzania.

Kwakuwa kaka yake Nuru hakuwa na kipaji cha Muziki, alimtaka Dandu ajaribu kuongea na Nuru ambaye alionekana kuwa na mapenzi na muziki ingawa alikuwa na umri mdogo wa miaka 16 tu.

Kwa jinsi alivyokuwa smart, mrembo huyo alicheza karata yake kwa usahihi baada ya marehemu James Dandu kumpa nafasi ya kujaribu. Jaribio hilo la kwanza lilizaa matunda bora moja kwa moja na kuandika historia kubwa iliyofungua njia ya muziki wake.

“So Mtoto wa Dandu akanifuata, nikabook kufanya ‘demo’. Baada ya kufanya ile demo kwenye record label ambayo ilikuwa inaitwa Stockholm Records ya nchini Sweden, walinipenda sana. Kwa wakati huo nilikuwa na umri wa miaka kati ya 15 na 16,” anasimulia.

“Kwahiyo wakasema hawawezi kunisaini kwa sababu niko underage (umri wangu hautoshi kisheria) kwa hiyo inabidi uongee na mzazi wangu. So wakaongea na mama yangu, kikao cha kwanza tumekaa wakampa mkataba asaini, akawaambia ‘no, kwa kuwa huyu ni mwanangu inabidi niende niusome vizuri kwa umakini’,” anaendelea.

Mama yake alipata wasiwasi kuhusu uamuzi wa kumruhusu afanye muziki kwa kuwa alitaka kumuona mwanae akitumia muda wake wote katika masomo. Hata hivyo, Nuru alifanikiwa kumshawishi waliporudi nyumbani baada ya kujiridhisha na mkataba waliopewa.

“Mimi nikamwambia nakuahidi, ukisaini huu mkataba, nitafanya vizuri zaidi shuleni,” anaendelea kusimulia. “Mama akasita sana, kama anaona ni mbinu ya kumshawishi tu, lakini kwa sababu alikuwa anafahamu mimi najitahidi na ni mtu napenda sana kusoma…kwa hiyo akasema basi atakuwa atakuwa poa, tukaenda kama vikao vitatu na uongozi wa ile recording label mwisho akasaini.”

Nuru alianza kufanya muziki chini ya label hiyo ya Sweden kwa makubalino maalum, wakati huo akiwa anatumia jina la ‘Danuma’. Anasema jina hilo lilitoholewa kutoka kwenye ya mwanzo ya sentensi ‘Dada Nuru Magram’.

“‘Da’ ilikuwa na maana ya dada kwa kuwa nilikuwa msichana pekee kwenye kundi, ‘Nu’ ilitoka kwenye jina langu halisi ‘Nuru’ na ‘Ma’ lilitoka kwenye jina langu la baba ambalo ni ‘Magram’.

Miaka michache baadaye Nuru alirudi nchini Tanzania na kuanza kufanya muziki wa Bongo Flava na video kali ambazo takribani zote ziliongozwa na ‘Adam Juma’ wa Visual Lab.

Baadhi ya nyimbo za RnB na Bongo Flava alizofanya ni Muhogo Andazi aliomshirikisha Bob Junior, Chapa Lapa aliomshirikisha Vedasto, Nisubiri Usilale, Wewe, Kwanini, Walimwengu na wiki iliyopita aliachia wimbo mpya unaoitwa ‘L’.

Nje ya muziki, Nuru The Light ni msomi na mtaaluma wa masuala ya Kisaikolojia aliyoyasomea kwa muda wa mika 7 nchini Sweden, na ameajiriwa kama mtoa huduma za ushauri nasaha wa masuala ya kisaikolojia nchini Sweden ambako ameishi takribani miaka 20.

Hivi sasa yuko nchini kwa muda wa mapumziko ambapo ameutumia kutambulisha wimbo wake mpya na hivi karibuni anatarajia kuzindua video ya wimbo huo aliyofanya na Adam Juma.

“Utakuwa uzinduzi wa kipekee, na nawaahidi mashabiki wangu nilichokifanya ni bora kama kawaida na nitaendelea kufanya bora kila siku. Nafanya kazi Sweden lakini kila wakati napakumbuka nyumbani na ndio maana naanzisha hata projects za kusaidia jamii kadri navyoweza,” alisema.

Nuru amekuwa akijihusisha pia na miradi mbalimbali ya kusaidia jamii ya watanzania. Moja kati ya miradi hiyo ni ule aliouanzisha na kuutekeleza mwaka jana kuwasaidia wanawake wajasiriamali ambapo hadi sasa amefanikisha kuwaendeleza wanawake zaidi ya 7 wanaofanya biashara kwa msaada wake.

Sikiliza zaidi kipindi hicho hapo chini.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents