Habari

Rais Magufuli ampa makavu RPC Muroto “Nikwambie ukweli, hujanifurahisha”

Rais wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli Ijumaa hii ameweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa nyumba 118 za makazi ya Askari wa Jeshi la Polisi katika eneo la Nzuguni jijini Dodoma, ambapo ujenzi huu utagharimu shilingi Bilioni 2.728 na utakamilika Desemba 31, 2019.

Akizungumza wakati wa mkutano huo, Magufuli amemwita na kumhiji Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, RPC Gires Muroto kuhusu pesa kiasi cha Tsh milioni tano ambazo alimpatia kwa ajili ujenzi wa Kituo cha Polisi.

RPC Muroto amesema tayari tofali 7239 mifuko ya sementi 40 na bati 65 tayari zipo na wiki kesho ataanza kwa kasi kubwa.

“Nimepita pale na kukagua mwenyewe, nimakuta mchanga tu, nataka nikwambie ukweli, hujanifurahisha, nataka kuanzia wiki ijayo ujenzi huu uende haraka na ukamilike mapema.

“Nawashukuru IGP na Waziri wa Mambo ya Ndani kwa kunialika kwenye shughuli hii ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa nyumba 118 za askari wa Jeshi la Polisi hapa Dodoma. Nitoe wito kwa wanaotekeleza mradi wa ujenzi huu wafanye haraka na mmeniahidi kuwa utakamilika kwa wakati na iwe hivyo ili askari wangu wapate sehemu nzuri ya kukaa.

“Ndugu zangu Askari endeleeni kuchapa kazi, ili Tanzania na watu wake waendelee kukaa kwa amani, mimi nipo pamoja na ninyi, endeleeni kufanya kazi kwa bidii, uadilifu na uaminifu mkubwa, Watanzania wanawategemea ninyi.

Rais Dk. John Magufuli ameagiza jengo lililokuwa linatumiwa na Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) lililopo jijini Dodoma kuwa Makao Makuu ya Jeshi la Polisi; “Ni matumaini yangu leo nitaona kibao kikubwa pale kimeandikwa Jeshi la Polisi.
“Kwa kuwa mmetekeleza wito wa kuhamia Dodoma, nimeamua kuwapa jengo la ghorofa nne lililokuwa linatumiwa na RUWASA, sasa yatakuwa makao makuu ya Jeshi la Polisi, nimewapa jengo hili kwa kutambua uchapakazi wenu.

“Jiji la Dodoma ndilo makao makuu hilo halina mbadala na tangu tuanze kuhamia hapa pamebadilika sana na panapendeza na nataka niwahakikishie miaka michache ijayo jiji hili litaifikia au hata kuizidi Dar es Salaam.

“Taifa hili linawategemea ninyi vyombo vya ulinzi na usalama, bila ninyi hakuna taifa, bila ninyi hakuna maisha, bila ninyi hakuna uwekezaji, bila ninyi hakuna viwanda,” amesema Magufuli.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents