Habari

Ridhiwani aeleza alichoteta na Lowassa Dar

Picha inayomuonyesha waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa akiteta jambo na Ridhiwani, mtoto wa Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete imemfanya mbunge huyo wa Chalinze kujitokeza na kuizungumzia.

Lakini yapo matukio mengi yanayoonyesha “siasa si uhasama” kama alivyosema Ridhiwani, Mwananchi imezungumza na Ridhiwani kuhusu walichoteta na Lowassa na pia inakurejeshea kumbukumbu za wanasiasa walionekana kuwa na uadui, lakini nje ya jukwaa wanaelewana.

Picha ya Ridhiwani na Lowassa ilipigwa wakati wa mechi ya watani wa jadi katika soka nchini, Simba na Yanga iliyofanyika Uwanja wa Taifa Jumamosi iliyopita na kuhudhuriwa na maelfu ya watu, wakiwamo wanasiasa ambao walikaa jukwaa kuu na kubadilishana mawazo bila kujali tofauti zao.

Katika picha hiyo, Ridhiwani, akiwa amevalia fulana ya njano anaonekana akiwa amemuinamia Lowassa ambaye amekaa, wakionekana kuteta jambo huku wameshikana mkono. Wote wawili wanaonekana kutabasamu.

Wawili hao walionekana kuwa na uadui mkubwa kabla ya kuanza kwa mchakato wa kutafuta mgombea urais wa CCM, huku Ridhiwani akionekana kutomkubali mbunge huyo wa zamani wa Monduli, ingawa hakuwahi kusema hadharani.

Wakati fulani mitandao ilidai kuwa Ridhiwani amesema nchi haiwezi kuongozwa na mtu kutoka Kaskazini, tuhuma alizozikanusha. Katika mahojiano na Mwananchi yaliyofanyika kipindi hicho, Ridhiwani alitaja makada watano waliofungiwa kwa miezi 12 na CCM kujishughulisha na kampeni, kuwa walikuwa na sifa ya kugombea urais.

Lowassa alikuwa mmoja wa makada hao. Lowassa hakujitokeza kupambana na Ridhiwani, ingawa ilikuwa inasemekana kuwa wana uadui mkubwa.Lakini hali hiyo haikuonekana wakati wanasiasa hao walipokutana Uwanja wa Taifa Jumamosi.

Faragha ya Lowassa na Ridhiwani

“Unajua ni siku nyingi (sikuwa nimekutana na Lowassa) na nilikuwa nimemkumbuka sana. Mkutano wa Dodoma (wa mwaka 2015), alikuwa amekaa na (aliyekuwa mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Shinyanga, Hamis Mgeja. Kwenye Uwanja wa Taifa Jumamosi nikamsalimia ‘mzee shikamoo’. Akanijibu ‘marahaba mwanangu, hujambo?’ Nikamwambia ‘sijambo’,” alisema Ridhiwani akirejea mazungumzo yake na Lowassa katika Uwanja wa Taifa.

Ridhiwani alisema baada ya salamu ile, alihitaji kufahamu zaidi kuhusu Kikwete.

“Akaniuliza pale kwamba ‘baba yako yuko wapi?’ Nikamwambia ‘yupo anaendelea vizuri, lakini kwa sasa amesafiri kikazi yuko Ethiopia’. Basi akaniambia akirudi nimsalimie sana, na mie nikamjibu nitamfikishia salamu huku tunafurahi pale.”

“Akasema ‘unajua sisi watu wa mpira ila shughuli tu ndiyo zinatubana’. Tukafurahi pale, akasema asante sana basi nikarudi kukaa kwenye nafasi yangu,” alisema Ridhiwani.

Katika ujumbe wake aliouandika katika akaunti yake ya instagram, Ridhiwani anaonekana kujifunza jambo baada ya kumalizika kwa siasa za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

By: Emmy Mwaipopo

Chanzo: Mwananchi

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents