Siasa

Serikali yanufaika na ukaguzi wa dhahabu

TANZANIA inaokoa wastani wa Sh bilioni moja kila mwezi baada ya kuachana na Mkaguzi wa dhahabu kutoka nje, Alex Stewart na kazi hiyo kufanywa na Watanzania, imefahamika

Faraja Mgwabati

TANZANIA inaokoa wastani wa Sh bilioni moja kila mwezi baada ya kuachana na Mkaguzi wa dhahabu kutoka nje, Alex Stewart na kazi hiyo kufanywa na Watanzania, imefahamika.

Serikali ilimwajiri Alex Stewart kutoka Marekani mwaka 2003 kwa ajili ya kukagua kiasi na thamani ya dhahabu inayochimbwa na migodi mbalimbali ya dhahabu nchini na kulipwa fedha nyingi, lakini kazi hiyo ilifanywa na Watanzania huku yeye akisimamia tu.

Stewart alikuwa akilipwa asilimia 1.9 ya mauzo ya dhahabu na mchanga unaopelekwa Japan, kiasi ambacho ni wastani wa Sh bilioni moja kwa mwezi. Kiasi hicho ni zaidi ya nusu ya asilimia tatu ya mrabaha ambao wenye migodi walikuwa wakiilipa serikali.

Wakati migodi ya dhahabu ya Bulyanhulu, Tulawaka, North Mara, Geita Gold Mine na Golden Pride, inailipa serikali asilimia tatu ya mauzo yao kama mrabaha, serikali ilikuwa inamlipa Stewart asilimia 1.9, hivyo kufanya serikali kuambulia asilimia 1.1 tu ya mapato ya dhahabu.

Hadi mkataba huo unasitishwa Agosti mwaka jana, serikali ilikuwa imemlipa Stewart Dola za Marekani milioni 50 (zaidi ya Sh bilioni 50). Hata hivyo, kufikia Agosti mwaka jana, serikali iliamua kuachana naye na hivi sasa kazi hiyo inafanywa na Watanzania chini ya Kitengo cha Ukaguzi wa Madini (GAP) ambacho kipo chini ya Wizara ya Nishati na Madini.

Akizungumza na HabariLeo katika mahojiano maalumu, Mkaguzi wa GAP, Jumanne Mohamed alisema kiasi kinachookolewa hivi sasa kinaweza kujenga madarasa zaidi ya 50 kwa mwezi. “Stewart alikuwa akilipwa fedha nyingi, lakini kazi tulikuwa tunaifanya sisi wenyewe Watanzania ndiyo maana serikali mwaka jana ikaamua tufanye wenyewe,” alisema.

Alisema kazi ya kukagua dhahabu inaendelea vizuri na sasa wana mpango wa kuanza kukagua madini aina nyingine kama vile almasi na tanzanite. Alisema GAP inakagua dhahabu tu sasa, kwa sababu ndiyo madini ambayo yalikuwa na malalamiko kwamba yanaibwa.

Hata hivyo, Mohamed alikanusha kwamba kumekuwa na wizi wa dhahabu unaofanywa na wenye migodi kwa sababu GAP inafuatilia kila hatua ya uzalishaji na uuzaji. Alisema wakaguzi wa GAP wapo katika migodi yote mitano wanayoikagua ya Bulyanhulu, Tulawaka, North Mara, Geita na Golden Pride kuhakikisha kwamba hakuna wizi.

“Mbali ya kupoteza fedha kwa kumlipa Stewart fedha nyingi, serikali haijapoteza mapato kwa kuibiwa hata wakati wa Stewart yupo, kwa sababu ni sisi wenyewe tulifanya kazi ya kudhibiti,” alisema. Alisema kwa kawaida kila mgodi unakuwa na mkaguzi mmoja isipokuwa mgodi wa Bulyanhulu ambao una wakaguzi wawili kutokana na kusafirisha mchanga Japan au China.

Kwa mujibu wa Mohamed, wakati wa kukagua dhahabu kuna kuwa na mwakilishi kutoka Ofisi ya Madini ya Mkoa husika, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), GAP na mwenye kiwanda ambao wote hushuhudia uzalishaji, uchukuaji sampuli wakilishi.

“Pia tunashuhudia uyeyushaji wa dhahabu na miche yote ya dhahabu hugongwa mihuri na kila mche una namba zinazofuatana (serial number) halafu kila mche unapimwa uzito na kurekodiwa mbele ya wote,” alisema Mohamed.

Alisema baada ya kupimwa uzito, miche hufungwa na kuwekwa kwenye boksi na kufungwa nembo (seal) na watu wa TRA na ofisi ya madini na wakati wa kupakia kwenye gari maboksi hayo hupimwa tena tayari kwa kwenda kwenye ndege kuuzwa. Kuhusu mchanga unaopelekwa Japan au China kuchambuliwa, Mohamed alisema wao wanatambua kiasi cha dhahabu kilichomo kwenye mchanga kabla ya kusafirishwa na wenye mgodi huilipa Serikali mrabaha wake kabla hata mchanga haujaondoka.

Alisema mchanga ukishajazwa kwenye kontena sampuli 18 wakilishi huchukuliwa na kupimwa na kisha hubaini kiasi gani cha dhahabu kipo ndani ya mchanga uliopo kwenye kontena na Bulyanhulu hulipa mrabaha asilimia tatu ndipo mchanga husafirishwa.

“Kwa ukaguzi kama huu mwenye mgodi hawezi kuiba chochote,” alisema Mohamed na kuongeza kuwa kitengo hicho kitahakikisha kinadhibiti upotevu wowote wa madini. Hadi sasa kampuni za madini hazijaanza kulipa kodi ya kampuni ya asilimia 30 ambayo zinatakiwa kulipa Serikali kwa madai kwamba hazijaanza kupata faida na kwa hiyo zinalipa mrabaha tu wa asilmia 3.

Kwa mujibu wa mikataba kati ya wenye migodi na serikali, wachimbaji hao wataanza kulipa kodi hiyo wakianza kupata faida. Hata hivyo, baadhi ya migodi kama vile Buhemba mpaka umemaliza dhahabu na kufungwa bila kulipia kodi hiyo. Kwa kutambua upungufu huo, Rais Jakaya Kikwete alianza mazungumzo na wenye migodi mara tu alipoingia madarakani ili waweze kulipa kodi hiyo kwa sababu huwezi kujua lini watapata faida na madini yataisha lini na mwelekeo ni mzuri.

Source: Habari Leo

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents