Burudani

Tidal ya Jay Z ni mradi uliowalenga matajiri na unaovunja connection ya muziki wa Marekani na maskini?

Huwezi tena kuangalia video ya muziki ya Beyonce, Nicki Minaj au Jay Z kwa haraka kupitia Youtube kama ulivyokuwa ukifaidi zamani. Ili kuangalia video mpya za wasanii hao ni lazima uwe mteja wa Tidal – huduma ya kusikiliza/kuangalia muziki mtandaoni inayomilikiwa na Jay Z.

jay-z-58

Tangu kuanzishwa kwa huduma hiyo, yametokea malalamiko mengi kutoka kwa wapenzi wa muziki duniani, wanaohisi kuwa Tidal ni mradi ulianzishwa kwa tamaa ya Jay Z na wasanii wenye ubia na mtandao huo kuendeleza kuzichuma fedha za mashabiki wa muziki na kutunisha zaidi mifuko yao iliyojaa zaidi.

Hadi March 2015, huduma hiyo ilikuwa imefikisha watumiaji zaidi ya 580,000 na ipo kwenye nchi 31 duniani hadi sasa. Ili kuweza kusikiliza nyimbo kwenye Tidai inakulazimu kulipa $20 kila mwezi – kiwango kinachoonekana kuwa ni kikubwa mno ukilinganisha na huduma zingine kama hizo ikiwemo Spotify.

Tangu kuanzishwa kwa Tidal, mashabiki wengi wa muziki duniani wamekuwa na wakati mgumu kupata nyimbo za wasanii wawapendao walioko kwenye huduma hiyo wakiwemo Jay Z, Beyonce na Nicki Minaj.
Hiyo ina maana kuwa mashabiki wao wengi si wa Afrika tu ambao ni ngumu kuweza kuwa wateja wa Tidal, bali hata mashabiki wao wa Marekani.

Kwa mfano Nicki Minaj ameachia video ya wimbo wake ‘Feeling Myself’ aliomshirikisha Beyonce ambayo unaweza kuiona kupitia Tidal peke yake. Tidal haipo Tanzania na hivyo ili kuweza kuitazama video hii ni labda upate msamaria mwema atakayeiweka Youtube.

Nimejaribu kuiangalia Youtube lakini sijafanikiwa kuipata. Kama shabiki wa wasanii hao, unaweza kuona ni kiasi gani Tidal inatengeneza ukuta kati ya wasanii wakubwa wa Marekani na mashabiki wao maskani na hasa sisi tuliopo katika nchi maskini.

Wamarekani wenyewe walalamika kuwa Tidal ni ngumu kuitumia. Wanasema hawafurahii kutazama video huko. Video ambazo tumekuwa tukiziona kwenye runinga bure na kuzitazama Youtube bila malipo, leo tuzione kwa kulipia Tidal? Ni vipi Jay Z na wenzake watazikwepa lawama za kuwa mapebari wanaotaka kujilimbikizia mali tu?

Muimbaji wa kundi la Death Cab for Cutie, Ben Gibbard aliiponda huduma hiyo kwa kusema kuwa alichokifanya Jay Z ni “kuwaleta mamilionea na mabilionea na kuwaweka kwenye jukwaa na kuwafanya wote walalamike kuhusu kutolipwa.” “Hii ndio maana kitu hiki kitakuja kufeli.”

Badala yake, Gibbard alisema Jay Z alitakiwa kutumia njia nyingine.

“Kama ningekuwa Jay Z, ningewaleta wasanii 10 underground au ambao hawapo kwenye label na kusema, ‘Hawa ni watu wanaohangaika kutengeneza maisha kwenye kiwanda cha muziki. Hata hivyo mshindani wangu anamlipa mtu huyu asilimia 15 ya kiwango kadhaa cha muziki wake kusikilizwa, lakini kiwango hicho hicho cha streams kwenye Tidal, itamlipa msanii huyu kiasi hiki.”

Hata hivyo afisa mkuu wa uwekezaji wa Tidal, Vania Schlogel, alipinga kauli hiyo na kuliambia Business Insider: “Wasanii wanaojitegemea hulipwa chini zaidi ya wenzao waliopo kwenye label – imekuwa hivi kwenye muziki kwa miaka. Wanalipwa asilimia 55 ya mrahaba dhidi ya wasanii wa label kubwa wanaolipwa 60%. Tunawalipa wasanii wote si tu katika kiwango sawa, lakini kiwango cha juu zaidi – kiwango kikubwa kwenye industry kwa 62.5%.”

Naye muimbaji Lily Allen aliwahi kuelezea kwenye mtandao wa Twitter kile anachoona kuwa Tidal ina gharama kubwa mno.

“Ninampenda Jay Z sana, lakini TIDAL ni aghali mno ukilinganisha na huduma zingine nzuri kabisa na streaming services. Amewachukua wasanii wakubwa & kuwafanya wapatikane kwenye TIDAL peke yake, watu watakimbilia kwenye mitandao ya wizi na kupeleka traffic kwenye site za torrent. Wasanii wachanga (ambao bado si mamilionea) watapata shida sana kwa matokeo yake.. mashaka yangu ni kuwa Tidal itawakwamisha wasanii wanaochipukia.”

Mmoja wa wasomaji wa mtandao wa Rap-Up wa Marekani ametoa maoni yake na kusema: Nafahamu kuwa muziki wa msanii si bure na wana haki ya kupata mapato kutokana na kusikilizwa mtandaoni na kuuzwa. Ninanunua single na album na sina shida kabisa na hilo lakini pointi yangu ni kuwa sijawahi kununua video ya msanii (isipokuwa kama ikija kwenye album kama Beyoncé). Kwanini nitoe hela kuangalia video ya muziki? Kwangu mimi video za muziki zimekuwa ni njia ya kupromote singles. Nimenunua single hivyo kwanini ninunue video?

Tidal haitakiwi kuwa Spotify na YouTube kwa pamoja. Tidal wanaweza kuwa na video za behind the scenes kwasababu wanatakiwa kuwapa subscribers wao kitu cha ziada, lakini sio kwa kuachia video kwa umma kama wanavyofanya sababu itawarudisha nyuma. Kwasababu kama mimi, wengine pia hawaweza kununua subscription ili tu kuangalia video ya muziki, hata kama ni ya wasanii wawili niwapendao.”

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents