Habari

TRC yawatoa hofu watanzania kuhusu Treni ya umeme

Yasema haitatumia umeme mwingi

MKURUGENZI Mkuu Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa amewatoa hofu Watanzania kwa kusema umeme wa kuendeshea treni hiyo siyo mwingi kama watu wanavyofikiria hivyo amewataka Watanzania kutokuwa na wasiwasi juu ya jambo hilo.

Aidha,Kadogosa amewaondoa wasiwasi watu juu ya nauli za usafiri huo wa treni ambapo amesema kwamba zitakuwa ni zile ambazo kila mtanzania ataweza kumudu.

Kadogosa ameyasema hayo Februari 26,2024 wakati wa kufanya majaribio ya Treni ya Kisasa ya umeme yenye mabehewa manne yaliyotoka Korea Kusini kwa ajili ya mradi wa Reli ya Kisasa (SGR).

Majaribio hayo ambayo yamefanyika kuanzia stesheni ya Dar es Salaam hadi mjini Morogoro yanaanza ikiwa imepita miezi michache tangu Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kuagiza treni hiyo kuanza safari zake kati ya Dar es Salaam na Dodoma.

Amesema majaribio hayo ni muhimu kwa sababu kwa mara ya kwanza wamefunga mabehewa ya abiria na yamesafirisha watu kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro.

“Kwenye majaribio ya leo treni hii imetumia saa mbili kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro ni matarajio yetu kuwa hadi kufika Julai kama alivyoagiza Rais safari kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma ziwe zimeshaanza,” amesema na kuongeza

“Tulianza na wazo kisha tukakata miti na kutengeneza mazingira na leo hii tumefikia hapa, hakika tunamshukuru Mungu, pili tunamshukuru Rais Samia kwa dhamira yake ya dhati ya kuendeleza mradi huu kwa kuhakikisha anatoa fedha za kukamilisha jambo hili, mpaka sasa vipande vyote hadi kufikia Mwanza vinajengwa,” amesema

Amesema sehemu kubwa ya matengenezo ya njia ya treni hiyo yamekamilika na wamebakiza maeneo machache hasa ujenzi wa madaraja ya juu eneo la Vingunguti, Banana pamoja na Njiapanda ya Segerea.

Naye Msemaji wa Serikali, Mobhare Matinyi amesema kuwa majaribio hao ni uthibitisho kwamba kile kilichoahidiwa na serikali kuwa kabla ya Julai treni hiyo itaanza kufanyakazi inatekelezwa.

“Hii ndiyo Tanzania inavyokwenda ahadi zilizopo zinatekelezwa hivyo watanzania wana kila sababu ya kujivunia mafanikio haya,” amehitimisha

Written by Janeth Jovin

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents