Michezo

Tupo tayari kutwaa ubingwa wa SportPesa Super Cup – Kamusoko

Nahodha wa klabu ya Yanga, Thaban Kamusoko anaamini kuwa timu yao ipo tayari kwa ajili ya michuano ya SportPesa Super Cup inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi siku ya Jumapili ya Juni 3 jijini Nakuru.

Akizungumza baada ya kumalizika kwa mazoezi ya jioni yaliyofanyika kwenye viwanja vya Nakuru Athletic Club, Kamusoko amethibitisha kuwa kikosi cha Yanga kina morali ya kutosha kwa ajili ya kuwavaa wapinzani wao Kakamega Homeboys kwenye mechi ya ufunguzi.

“Timu ipo vizuri na ina morali ya hali ya juu kuelekea kwenye mchezo wetu wa kwanza na
hakika tumedhamiria kufanya makubwa kwenye michuano hii kwani ukweli ni kuwa Yanga
ni timu kubwa na inacheza ili kushinda mataji.

Wanatujua
Nahodha huyo anayekaimu nafasi ya nahodha mkuu, Nadir Haroub amesema wataingia kwenye mchezo wao wa ufunguzi kwa kujiamini licha ya kutowajua wapinzani wao vyema.

Kamusoko

“Hatuwajui sana wapinzani wetu lakini naamini wao wanatujua kwasababu Yanga ni klabu kubwa na tunacheza mashindano ya kimataifa kila mwaka lakini sisi hatuwafahamu wao kiundani kwasababu hatujawahi kuwasikia”, alisema.

Akizungumzia michuano iliyopita ambayo Yanga ilitolewa kwenye hatua ya nusu fainali na AFC Leopards ya Kenya, Kamusoko amesema safari hii Yanga imeenda Kenya wakiwa kamiliili waweze kurekebisha makosa yao.

“Mwaka jana hatukutilia maanani michuano hii lakini tulikuja kujua umuhimu wake baada ya Gor Mahia kucheza na Everton kwa hiyo mwaka huu tumejipanga kuhakikisha haturudii makosa yaliyojitokeza”, alisisitiza Kamusoko.

Faraja

Naye kocha msaidizi wa kikosi hicho cha mabingwa mara 27 wa Tanzania Bara, Noel Mwandila amesema watafanya kila liwezekanalo kuhakikisha wanatwaa kombe hilo ili waweze kupata faraja baada ya kushindwa kufurukuta kwenye ligi ya ndani.

“Tuna kila sababu ya kufanya vyema kwenye michuano hii ili tuweze kuwapa faraja mashabiki wetu ambao wamekuwa wakituunga mkono tangu mwanzo wa msimu”,alihitimisha.

Yanga itakata utepe wa michuano ya SportPesa Super Cup siku ya Jumapili kwenye dimba la Afraha majira ya saa 7 kamili mchana kwa kuwavaa Kakamega Homeboys ambao wanashika nafasi ya tisa kwenye msimamo wa Ligi Kuu nchini Kenya.

Timu itakayofanikiwa kushinda kwenye mchezo huo wa ufunguzi itakutana na mshindi wa mechi kati ya Simba na Kariobangi Sharks kwenye hatua ya nusu fainali.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents