Habari

Wanaume watatu waiba maparachichi yenye thamani ya Tsh Milioni 600

Wanaume watatu katika jimbo la California nchini Marekani wamekamatwa na kuzuiliwa, wakituhumiwa kuiba maparachichi yenye thamani ya dola 300,000 ambayo ni sawa na zaidi ya Tsh milioni 600.

Kuongezeka kwa hitaji la matunda hayo duniani mwezi Mei kulisababisha bei ya maparachichi kupanda sana.

Polisi wanasema hilo huenda liliwafanya wanaume hao kushawishika kuiba matunda hayo kutoka kwa kampuni ya matunda ya Oxnard walipokuwa wanafanya kazi.

Afisi ya liwali wa wilaya ya Ventura imesema Carlos Chavez, Rahim Leblanc, na Joseph Valenzuela walikamatwa Jumatano.

Walikuwa wamefanya kazi katika Mission Produce, moja ya kampuni zinazoongoza duniani kwa usambazaji wa maparachichi, kwa miaka kadha.

Polisi wanaamini watatu hao wamekuwa wakiiba matunda hayo, kwa miezi kadha, na kuwauzia wateja ambao hawakuwa na ufahamu kwamba yalikuwa ya wizi.

Rais wa kampuni hiyo, Steve Barnard, anasema sanduku moja ya maparachichi kawaida huuzwa $50, lakini wanaume hao walikuwa wanauza nusu ya bei hiyo.

“Hitaji la matunda hayo limeongezeka. Kila mtu anapenda maparachichi,” Sajenti John Franchi wa afisi hiyo ya liwali aliambia gazeti la LA Times.

“Tunachukulia visa kama hivi vya wizi kwa uzito sana. Ni zao muhimu sana hapa na California.”

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents