Habari

Watu 15 wauwawa katika shambulio dhidi ya Kanisa katoliki

Watu 15 wameuawa na wengine wawili kujeruhiwa kufuatia shambulizi dhidi ya kanisa katoliki kaskazini mashariki mwa Burkina Faso siku ya Jumapili.

Tukio hilo lilitokea wakati wa ibada ya Jumapili katika kijiji cha Essakane katika jimbo la Oudalan – karibu na mpaka na Mali.

Maelezo machache yametolewa kuhusiana na kisa hicho.

Afisa mmoja wa kanisa hilo alidokeza kuwa watu hao wenye silaha wanashukiwa kuwa wanamgambo wa kijihadi.

Mamlaka katika mji mkuu wa nchi hiyo ya Afrika Magharibi, Ouagadougou haijatoa tamko lolote kuhusiana na shambulio hilo.

Taarifa ya mkuu wa Dayosisi ya eneo hilo, Abate Jean-Pierre Sawadogo, ilisema watu 12 waliuawa papo hapo, huku wengine watatu wakifariki hospitalini.

“Katika hali hii chungu, tunakuomba kuwaombea waliokufa kwa imani, ufueni ya haraka kwa waliojeruhiwa, na uimarishaji wa mioyo ya huzuni,” ilisema taarifa hiyo.

Huo ni ukatili wa hivi punde zaidi nchini humo kuhusishwa na wapiganaji wa wenye itikadi kali.

Zaidi ya theluthi moja ya Burkina Faso kwa sasa iko chini ya udhibiti wa waasi.

Mamlaka zimekuwa zikipambana na makundi ya kijihadi yenye mafungamano na al-Qaeda na Islamic State, ambayo yamechukua maeneo makubwa ya ardhi na kuwakosesha makazi mamilioni ya watu katika eneo la Sahel.

Katika miaka mitatu iliyopita, makanisa yamekuwa yakilengwa na waumini wengi kuuawa.

Burkina Faso, ambayo inatawaliwa kijeshi, hivi karibuni ilijiondoa katika jumuiya ya kisiasa na kiuchumi ya kikanda, Ecowas, pamoja na majirani zake wa Sahel, Mali na Niger.

Walitaja ukosefu wa uungwaji mkono kutoka kwa Ecowas katika vita dhidi ya ugaidi kuwa mojawapo ya sababu za kutaka kujiondoa katika muungano huo

Nchi tatu zinazoongozwa na jeshi tayari zilikuwa zimesimamishwa kutoka kwa umoja huo, ambao umekuwa ukizitaka kurejea katika utawala wa kidemokrasia.

Mapema mwezi huu, rais wa Burkina Faso anayeungwa mkono na jeshi Ibrahim Traoré alisema kuwa wanajeshi wa Urusi wanaweza kutumwa kupambana na wanajihadi katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

Imeandikwa na Mbanga B.

Chanzo; BBC Swahili

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents