Wasanii 10 wapya wa Tanzania wa kuwaangalia mwaka 2015
Kila mwanzoni mwa mwaka mpya tumekuwa na desturi ya kutaja orodha ya wasanii 10 wapya wenye uwezo mkubwa wa kuwaangalia zaidi. Katika orodha hii, tunajumuisha wasanii ambao wanaweza kuwa wapo kwenye game kwa miaka kadhaa nyuma na wamesharekodi ngoma kibao lakini bado hawajapata nafasi ya kufahamika zaidi kwa watu wengi.
Lengo la kuwataja ni kuwashawishi wadau wa vyombo vya habari nchini kuwapa nafasi ya kipekee wasanii hawa kwakuwa wana potential ya kuja kuwa wasanii wakubwa baadaye. Hawa ni wasanii 10 ambao tunahisi mwaka 2015 wanapaswa kuangaliwa kwa jicho pana zaidi.
P The MC
P ni rapper mwenye umbo ndogo na zao la Tamaduni Muzik. Kwa watu waliowahi kuhudhuria kilinge cha Msasani Club uwezo wake watakuwa wanaufahamu. Ni rapper mwenye uandishi wa kipekee na style kali.
Rapper huyu amesharekodi ngoma kibao ambazo kwa bahati mbaya nyingi hazijaweza kusikika kwa wengi. Pia amekuwa akishirikishwa kwenye collabo kadhaa alizozitendea haki. Akipewa nafasi anayostahili, ni rahisi sana uwezo wake kudhihirika.
Nyimbo alizowahi kurekodi ni pamoja na Baba Msaliti, Penzi la Siri, Wanangu, Fadhili ni Utumwa, Nafunga Mtaa na zingine.
Ingia hapa kusikiliza nyimbo zake zaidi.
Zaiid
Zaiid (kulia) akiwa na Majani
Zaiid ni mshkaji wake wa karibu na P The MC na kwa mujibu wa mtangazaji wa Times FM, Jabir Saleh, rappers hawa wawili wanamkumbusha Redman na Method Man.
Kwa wanaofuatilia hip hop ya mtaa, jina la Zaiid si geni. Ni rapper mwenye uandishi hatari kama jambia lililonoolewa vikali. Akiwa ni zao jingine la Tamaduni Muzik, Zaiid alijinyakulia sifa nyingine pale alipotumia beat ya ngoma iliyomtambulisha J.Cole, Who Dat na kufanya version yake mwenyewe ambayo pia aliitolea video.
Tangu hapo Zaiid amekuwa akiachia video kadhaa zenye utambulisho wa hip hop ya kweli ikiwemo freestyle ya hivi karibuni kwenye beat ya Lose Yourself ya Eminem.
https://www.youtube.com/watch?v=ggVsdYfegYE
Yeye na P the MC wanatarajia kuachia mixtape yao ya pamoja iitwayo Mwenge Kiwalani.
Rossie M
Rosemary Mpangala aka Rossie M aliingia kwenye 20 bora ya shindano la Bongo Star Search mwaka 2012. Ni mhitimu wa chuo kikuu cha Dodoma ambako alikuwa akisoma kozi ya Maliasili na Utalii.
Ni muimbaji mkali wa R&B lakini uimbaji wake ‘aggressive’ unamfanya uweze kumfananisha na ule uimbaji wa Mary J Brige wa hip hop soul.
Ngoma mpya aliyoachia hivi karibuni inaitwa Wivu.
Kiche Legend
Kiche ni lead rapper kwa kundi liitwalo 909 linalojumuisha members wengine kama Ronny, Agogo, Icy, Mswati na Rockhard. Kiche ni rapper mkali wa Kiingereza na Kiswahili. Hata hivyo akichana Kiingereza huwezi kumtofautisha na rappers wa Marekani.
Pamoja na kurap, Kiche pia ni muimbaji mzuri wa R&B na kwa qualities hizo si kosa kumfananisha na Drake. Unaweza kusikia uwezo wake katika kurap na kuimba kwenye nyimbo za hivi karibuni za 909, Njoo Hapa na Sikubali Kushindwa.
Slim Sal
Slim ni rapper kutoka Dodoma na huenda ndiye rapper mwenye uwezo wa kurap haraka zaidi kuliko wote Tanzania kwa sasa na unaweza kumfananisha na Twista kwa uwezo huo. Ngoma yake aliyoitoa hivi karibuni inaitwa Mistaripedia.
Malaika
Diana Malaika ni muimbaji mrembo ambaye sauti yake ilisikika kwa mara ya kwanza kwenye wimbo wa Chege ‘Uswazi Take Away’.
“Uswazi Take Away’ndio ulikuwa wimbo wangu wa kwanza. Baada ya hapo ndIo nikatoa wimbo wangu mwenyewe unaitwa ‘Nenda’ video alifanya Adam Juma. Kuanzia hapo ndo nikaona sasa nifanye muziki serious na nitimize ndoto zangu maana nilikuwa napenda muziki tokea zamani ila kwakuwa wazazi waliniambia nimalize kwanza masomo ndio nianze muziki,” aliiambia Bongo5 hivi karibuni.
https://www.youtube.com/watch?v=ibEWjb8dNKQ
Sasa hivi mrembo huyo ana wimbo mpya uitwao ‘Mwantumu’.
Edu Boy
Edu Boy ni mshindi wa shindano la Fiesta Super Nyota 2013 akitokea Mwanza. Hivi karibuni aliachia video ya wimbo wake ‘Yes or No’ aliomshirikisha Belle 9.
Okelo
Okelo ni msanii mpya kabisa kwenye scene ya Bongo Flava lakini video yake ya kwanza ya wimbo ‘Okelo wa Show’ inadhihirisha wazi kuwa akipewa nafasi mwaka huu atapeta. Yupo chini ya studio za Classic Sounds za Mona Gangster.
Wiista
Wiista ni rapper aliyekuwa kwenye kundi la Navy Kenzo lakini kutokana na sababu kadhaa aliondolewa kwenye kundi. Kwa sasa ni solo artist na ameachia video ya wimbo wake Naiye.
Rubby
Hellen George aka Rubby ni mshindi wa Fiesta Super Nyota 2014. Kwa sasa ameachia wimbo wake wa kwanza uitwao Na Yule.