Siasa

Aliyeanika wizi wa kura Kenya atimkia Ulaya

MMOJA wa maofisa wa Tume ya Uchaguzi ya Kenya (ECK) ambaye aliamua kuweka wazi wizi wa kura na upendeleo uliofanywa kwa Rais Mwai Kibaki amekimbilia katika nchi za Ulaya na kuomba hifadhi kukimbia vitisho dhidi ya maisha yake.

Waandishi Wa Mwananchi na Mashirika ya Habari


MMOJA wa maofisa wa Tume ya Uchaguzi ya Kenya (ECK) ambaye aliamua kuweka wazi wizi wa kura na upendeleo uliofanywa kwa Rais Mwai Kibaki amekimbilia katika nchi za Ulaya na kuomba hifadhi kukimbia vitisho dhidi ya maisha yake.


Rais huyo wa Kenya ni Kipkemoi arap Kirui, ambaye alikuwa mfanyakazi wa Ofisi ya Bunge la nchi hiyo na kupelekwa ECK kwa muda wakati wa uchaguzi.


Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana kupitia barua pepe aliyowaandikia ndugu na jamaa zake siku chache baada ya kutimua, Kirui alisema kuwa ameamua kuchukua hatua hiyo, baada ya watu wasiofahamika kuendelea kumtishia maisha yake.


Taarifa za kuondoka kwake alizitoa kwa ndugu zake kupitia barua pepe baada ya ndugu hao kumkosa kupitia simu yake ya mkononi.


�Hii ni kuwajulisha rasmi kuwa nipo Ulaya kwa sababu muhimu, hasa ni kutokana na baadhi ya watu kutishia usalama wa maisha yangu,� alisema Kiruip bila kutaja nchi aliyokimbilia na kupata hifadhi, siku aliyoondoka, wala watu anaodai kuwa wamekuwa wakitishia usalama wa maisha yake.


Mara baada ya utata kutokea kwenye matokeo ya uchaguzi, Kirui alijitokeza kupitia runinga na kueleza uamuzi wake wa kujitoa katika Tume hiyo ya Uchaguzi muda mfupi kabla ya kutangazwa kwa matokeo, kutokana na utashi wake kutoruhusu mambo yasiyo ya kawaida yaliyokuwa yakifanyika ndani ya ECK kwa nia ya kuharibu matokeo hayo.


�Ninazungumza wazi kwa watu wa Kenya kuwa utashi wangu hauniruhusu kuendelea kuona kile ninachokishuhudia kikifanyika halafu nikae kimya, � alisema Kirui alipoamua kujitoa Desemba 31 mwaka jana, katika Mkutano wa Chama cha Orange Democratic Movement (ODM).


Katika hatua nyingine, taarifa kutoka mashirika mbalimbali yanayotoa misaada Kenya zinaeleza kuwa, zaidi ya watu 500,000 wataendelea kuhitaji msaada wa kibinadamu katika wiki zijazo kufuatia hali iliyopo sasa, na kama machafuko zaidi yataendelea.


Shirika la Umoja wa Mataifa (UN) lilieleza kuwa, utapiamlo kwa watoto umeongezeka na pia matukio ya ubakaji yanaongezeka kadri siku zinavyokwenda, huku kukionekana kutokuwepo na suluhu ya haraka.


Afisa wa UN anayeshughulikia masuala ya kibinadamu alikaririwa na shirika moja la habari akieleza kuwa, zaidi ya watu 255,000 wanaendelea kukimbia makazi yao na hali ya chakula kwa watu hao inaendelea kuwa mbaya.


Idadi hiyo ni zaidi ya asilimia 100 ukilinganisha na ile iliyokuwepo wiki iliyopita. Taarifa za wiki iliyopita zilionyesha kuwepo kwa wananchi wapatao 100,000 waliokuwa wakikimbia makazi yao huku wengine wakiripotiwa kwenda katika nchi za Tanzania na Uganda.


Wakati huo huo, kutoka wilayani Tarime, mkoani Mara, Samsoni Chacha anaripoti kuwa, mahindi na maharage yaliyoporwa maeneo ya Migori nchini Kenya na kuingizwa katika vijiji vya Kogaja, Ikoma na Shirati yanasadikiwa kuwa na sumu yenye madhara kwa binadamu.


Waporaji wanaelezwa kuwa, waliiba magunia zaidi ya 30,000 ya mahindi na maharage kutoka katika bohari la chakula katika Manispaa ya Migori, mkoani Nyanza kilomita 20 kutoka mpaka wa Tanzania.


Inaelezwa kuwa nafaka hizo zilikuwa zimewekwa sumu ya kuulia wadudu Novemba mwaka jana na kuwa ilihitajika kupita miezi sita kabla ya kutumika kwa chakula.


Baadhi ya wakazi wa miji ya Migori na Isabenia nchini Kenya, Kimani Kamau, James Onyango, Alice Paulo na Mwenyekiti wa Haki za Binadamu Wilaya ya Kurya, Peter Masante, walisema asilimia kubwa ya magunia yaliyoibwa yameingia Tanzania.


Vijiji vinavyoelezwa kuwa shehena hiyo ilipitia ni; Kogaja, Ikoma na Shirati. Kwa upande wa Kenya tayari tahadhali imeshatolewa kwa wananchi na wameelezwa kuwa, wanatakiwa kuyaosha kwanza kabla ya matumizi na kwa Tanzania, tahadhali kama hiyo imetolewa na


Mkuu wa wilaya za Tarime na Rorya, Stanley Kolimba.


Katika hatua nyingine Andrew Msechu na Sophia Mlenda


Wanaripoti kuwa wasomi nchini wamelaani machafuko yanayoendelea Kenya na kumtaka Rais Mwai Kibaki kuachia madaraka na kutaka hatua za haraka zichukuliwe kuitisha uchaguzi mpya wa Rais wa nchi hiyo.


Msimamo huo ulitolewa jana na viongozi wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya Juu nchini (Tahiliso) na Umoja wa Wahadhiri wa Vyuo Vikuu kupitia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDASA) mara baada ya maandamano yaliyoanzia Ubungo hadi viwanja vya Jangwani.


Wasomi hao wameitaka serikali ya Tanzania kusitisha mchakato wowote wa Shirikisho la Afrika Mashariki kwa kuwa tayari Rais Mwai Kibaki ameshaonyesha nia mbaya ya udikteta na mbaya zaidi Rais Yoweri Museveni ameitambua serikali yake.


Akitoa tamko la Udasa, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Azaveli Lwaitama alitoa wito kwa serikali ya Tanzania kutoitambua Serikali ya Kenya chini ya Rais Mwai Kibaki hadi mgogoro huo utakapomalizika.


“Tunaiomba serikali yetu isithubutu kuitambua serikali ya Kenya inayoongozwa na Mwai Kibaki, hadi pale utatuzi wa mgogoro huo utakapofikiwa kwa kulenga na kuheshimu maoni ya wapiga kura wa Kenya, pia tunapendekeza Tume huru za Uchaguzi na sheria za uchaguzi ziwe za kidemokrasia kwa nchi zetu zote,” alisema Dk Lwaitama.


Aliongeza kuwa Tanzania inatakiwa kubeba jukumu kubwa kwa kushirikiana na wanachama wenzake wa EAC na Umoja wa Afrika (AU) katika mgogoro huu kuliko ilivyo kwa Marekani na Uingereza kwa kuwa nchi hizo ndizo zinazoathirika zaidi kisiasa na kiuchumi kutokana na mgogoro huo, kwa kuishinikiza serikali ya Kenya kujali uamuzi na haki za wananchi wake kupitia matokeo sahihi ya kura.


Alisema kuwa UDASA haikubaliani na mtazamo kuwa chimbuko la mgogoro wa kisiasa ni ukabila, bali ni kielelezo cha mapambano ya kitabaka baina ya kundi dogo la wanyonyaji dhidi ya kundi kubwa la wananchi wanaoendelea kupuuzwa, kunyonywa na kudharauliwa, pia mbinu za wanasiasa wahafidhina na mafisadi wenye kutafuta kuungwa mkono kwa kuibua hisia za ukabila.


“Katika hili, sisi pia tunasikitishwa na tabia za ukabila hasa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kupitia vyama vya wanafunzi vya kikabila, tunawashauri wanafunzi kuanzisha vyama vyenye sura ya kitaifa na kizalendo, vyuo vikuu vinatakiwa kuwa vituo mkakati vya mapambano dhidi ya ukabila, ubeberu na ufisadi, visiwe makambi ya maovu hayo,” alisisitiza Dk Lwaitama.


Naye Katibu Mkuu wa TAHLISO Julius Mtatiro alisema msimamo wa Umoja huo unaungana na matakwa ya ODM na kumtaka Rais Kibaki aondoke madarakani, pia iundwe serikali ya mpito na kuhakikisha inasimamia kurudiwa kwa Uchaguzi Mkuu wa Rais ndani ya miezi isiyozidi mitatu.


Alisema ni vyema Jumuiya ya kimataifa akamuwekea vikwazo kwa kutomtambua kama Rais wa Kenya, kwa kumzuia kwenda nje ya nchi hiyo kwa kutumia wadhifa huo, ili kuonyesha gharama ya Demokrasia kwa viongozi wenye uchu wa madaraka.


“Tunaungana na juhudi za Rais Kikwete kwa kuwa tunatambua kuwa hana uhusiano wowote na Odinga wala Kibaki, lakini ni wazi kuwa ana uhusiano na wananchi wa Kenya, tunamuomba aendelee kuwa na msimamo usioyumba na amueleze Kibaki kuwa haki haipimiki mezani, ni kitu cha lazima,” alisema.


Aliongeza kuwa ni vyema Rais Museveni wa Uganda na George Bush wa Marekani wakajitokeza na kuwaomba Wakenya na Afrika msamaha kwa kutambua na kumtumia Rais Kibaki salamu za pongezi, pia Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Kenya Samuel Kivuitu akamatwe na kufikishwa mahakamani.


Tena, Joyce Mmasi anaripoti kutoka jijini hapa kwamba; nia ya wasomi wa UDSM kutaka Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Kenya, Samwel Kivuitu anyang�anywe shahada yake ya sheria aliyoipata chuoni hapo, inakumbana na ugumu kufuatia taratibu za chuo hicho kutokuwa na utaratibu wa kufuta shahada za wahitimu kutokana na matendo yao baada ya kuhitimu.


Wasomi wa UDSM mwishoni mwa wiki iliyopita walimtaka Mkuu wa Chuo hicho aifute shahada ya Kivuitu kwa sababu kwamba amewadhalilisha kwa kutangaza matokeo ambayo hakuna anayeelewa jambo lililozua machafuko nchini Kenya.


Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Rwekaza Mukandara aliliambia gazeti hili kwa njia ya simu jana kuwa, chuo kikishamtunukia mtu shahada, hakina uwezo wa kumnyang�anya kwa sababu zozote isipokuwa za kitaaluma.


Profesa Mukandara alisema, chuo kinaweza kumnyang�anya mtu shahada yake endapo atakuwa amegundulika kughushi vyeti na kama hakuwa na sifa ya kujiunga na chuo kikuu.


Alisema sababu nyingine ambazo chuo kinapata haki ya kumnyang�anya mtu shahada kilichomtunukia ni endapo itagundulika kuwa mtu huyo aliibia mitihani, au alifanya udanganyifu wa aina yoyote katika suala la kitaaluma na si vinginevyo.


�Katika hili la Kivuitu hatuna uwezo wa kumnyang�anya shahada yake, maana sio academic issue, ingekuwa amefanya moja ya hayo niliyoyataja tungekuwa na uwezo wa kumnyang�anya lakini hana kosa lolote linaloturuhusu kumnyang�anya shahada yake� alisema.


Mwishoni mwa wiki iliyopita wasomi kadhaa walitaka mwenyekiti huyo wa Tume ya uchaguzi anyang�anywe shahada yake kutokana na kutajwa kuvuruga katika suala zima la kutangaza matokeo ya uchaguzi wa Kenya hali iliyopelekea nchi hiyo kuingia katika machafuko ya kisiasa na kupelekea watu zaidi ya 300 kupoteza maisha na wengine zaidi ya laki tano kukosa mahali pa kuishi.


Kivuitu hata hivyo baada ya kutangaza matokeo alinukuliwa akisema hana uhakika kama matokeo aliyoyatangaza yalikuwa sahihi na hivyo hana uhakika kama Rais Kibaki aliyemtangaza mshindi alishinda katika uchaguzi ule.


Alisema alishinikizwa kutangaza matokeo yale hali iliyoonyesha ni msomi asiyezingatia maadili ya kazi yake na kupoteza sifa ya kuwa msomi tena wa masuala ya kisheria.


Source: Mwananchi

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents