Burudani

Babu Seya akimbilia mahakama ya haki za binadamu ya Arusha

Mwanamuziki mkongwe nchini, Nguza Viking maarufu kama Babu Seya na mwanae, Johnson Nguza aka Papii Kocha, ameamua kwenda kutafuta msaada kwenye Mahakama ya Haki za Binadamu Afrika (AFCPHR) ya Arusha.

babu+seya+px

Wanamuziki hao wamekata rufaa dhidi ya adhabu waliyohukumiwa mwaka 2004 ya kutumikia kifungo cha maisha gerezani. Kupitia shauri lao lililowasilishwa mahakamani na kupewa namba 006/ 2015, wanaiomba Mahakama ya Afrika kutoa uamuzi kuwa haki zao zilivunjwa.

Kwa sababu hiyo wanaomba waachiwe huru na kulipwa fidia. Katika shauri hilo pia wameomba wawezeshwe kupata msaada wa sheria na. Pia wanataka Mahakama hiyo iteue wataalamu watakaotoa ufafanuzi wa hoja za kesi yao na kuisaidia kufikia wajibu wake.

Miongoni mwa hoja za walalamikaji hao zilizowasilishwa mahakamani hapo ni pamoja na kwamba mwenendo wa shauri lao haukufanyika kwa kuzingatia haki,.

Vilevile wanadai hati ya mashtaka dhidi yao ilikosewa kuandikwa tarehe ambayo tuhuma za makosa yao zilidaiwa kufanywa hivyo wakashindwa kutayarisha utetezi wao.

Pia wanadai mahakama iliyowatia hatiani ilijielekeza katika ushahidi wa upande wa mashtaka pekee usioshirikisha ushahidi mwingine.

Wanadai kwamba Serikali ya Tanzania kupitia maofisa wake, ilivunja misingi ya haki za binadamu na sheria za kimataifa. Wanadai pia kwamba mlalamikiwa alivunja Ibara 1,2, 3, 5, 7(1)b), 13 na 18(1) ya Mkataba wa Afrika kuhusu Ubindamu na Haki za Binadamu.

Malalamiko mingine ni kuwa baada ya kukamatwa hawakuelezwa mapema kuhusu mashtaka waliyokuwa wakituhumiwa nayo. Wanadai kwa sababu hiyo waliwekwa chini ya ulinzi kwa siku nne bila kuwa na mawasiliano na kupata fursa ya kuonana na mwanasheria au mtu mwingine ye yote.

Wanadai wakiwa chini ya ulinzi polisi waliwatesa na kuwatukana na baadaye ofisa mmoja wa polisi aliwaeleza kuwa wanatuhumiwa kwa ubakaji. Walalamikaji hao raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), walikuwa wakiishi na kufanya kazi ya muziki Dar es Salaam.

Wanadai kwamba mashtaka dhidi yao yalitungwa na hivyo hukumu iliyotolewa haikujikita katika ushahidi wenye nguvu katika sheria.

Nguza na wanawae watatu walikamatwa Oktoba 12, mwaka 2003 na kufikishwa kituo cha Polisi cha Magomeni Dar es Salaam.
Baadaye walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Oktoba 16 mwaka 2003.

Watuhumiwa hao pamoja na mwingine aliyejulikana kwa jina la Mwalimu walishtakiwa kwa tuhuma 10 za ubakaji.

Pia walikabiliwa na mashtaka 11 ya kunajisi watoto 10 wenye umri wa miaka sita na nane. Watuhumiwa wote walikana mashitaka yao. Baada ya kusikilizwa kesi hiyo, Mahakama ya Kisutu Dar es Salaam ilitoa hukumu Juni 25, mwaka 2004.

Iliwatia hatiani kwa kifungo cha maisha jela huku mtuhumiwa wa tano, Mwalimu akiachiwa huru. Walikata rufaa Mahakama ya Rufaa Tanzania Oktoba 30 mwaka juzi ambako wafungwa wawili Francis Nguza na Nguza Mbango walishinda rufaa yao.

Hata hivyo, Babu Seya na Papii Kocha walijigonga mwamba na kurudishwa jela kwa kuhukumiwa kifungo cha maisha.

Source:Mtanzania

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents