Michezo

Mabadiliko ya Yanga na Simba yapigwa stop na serikali

Serikali imezipiga stop klabu za Yanga na Simba kuendelea na michakato yao ya kubadili umiliki wake hadi pale yatakapofanyika marekebisho ya katiba zao.
YangaSimba

Hayo yalitangazwa jana na Kaimu Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Mohamed Kiganja alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Hivi karibuni klabu hizo kongwe ziliazimia kuingia kwenye mabadiliko, Yanga ikikodishwa na mwenyekiti wake Yusuf Manji na Simba ikitaka kuuza hisa asilimia 51 kwa mfanyabiashara Mohamed Dewji ‘Mo’.

Kiganja alisema Serikali haikatai mabadiliko ya uendeshaji katika klabu hizo pamoja na nyingine za wanachama, ila inachotaka kwanza kufanyike marekebisho ya katiba zao kwani za sasa haziruhusu mabadiliko hayo.

Alisema kuwa BMT inapenda kuona wahusika wanafuata sheria na taratibu za nchi katika kufikia malengo yao, ambapo alisisitiza kuwa kuendelea na michakato hiyo kabla ya kurekebisha katiba zao ni kosa na hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.

“Hivi karibuni kumeibuka michakato ya watu wakitaka kubadilisha umiliki wa klabu za wanachama na kuzielekeza katika utaratibu wa hisa na ukodishwaji, vitendo vimesababisha migogoro mikubwa ambayo inaashiria uvunjifu wa amani…,” alisema.

Kiganja alisema tayari mezani kwake kuna barua nyingi za wanachama wa Yanga wanaopinga vikali kuendelea kwa mchakato huo wa kubadilisha umiliki.

Kwa mujibu wa katiba ya Yanga iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2010 Ibara ya 56 inaeleza kuhusu kampuni ya umma: Inaeleza kuwa kutakuwa na kampuni itakayojulikana kama Young African Sports Corporation Limited ambayo itasajiliwa chini ya sheria ya makampuni kama kampuni ya umma yenye hisa.

Sehemu ya pili ya ibara hiyo inasema wanachama wote katika klabu ambao katika tarehe ya marekebisho ya Katiba ya mwaka 2007 wako hai kwa nguvu ya uanachama wao watakuwa wanahisa katika kampuni kwa kiwango cha idadi ya hisa watakapopata kwa mujibu wa muafaka wa Yanga uliofikiwa na wana Yanga Juni 22, 2006.

Klabu itamiliki hisa zilizosawa na asilimia 51 ya hisa zote zilizomo katika klabu hiyo. Mkutano Mkuu wa Uchaguzi utachagua wanachama wawili, ambao sio miongoni mwa viongozi wa klabu kuwa wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa kampuni kwa ajili ya kuwakilisha maslahi ya klabu kwenye kampuni.

Tayari Yanga iko chini ya Kampuni ya Yanga Yetu ambayo ni mali ya mwenyekiti wa klabu hiyo Manji, ikiwa ni kinyume na katiba yao wenyewe.

Kiganja alisisitiza kuwa klabu zisitishe mipango ya kubadilisha uendeshaji na ziendelee kuwa mali ya wanachama. Wakati Yanga walikuwa tayari wameishaingia mkataba wa miaka 10 wa
kuikodisha klabu yao, wenzao wa Simba walijipa miezi sita kukamilisha taratibu za kuuza hiza.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents