Rais Mwinyi apigwa kofi jukwaani
Rais Mstaafu Rais Ali Hassan Mwinyi jana alipigwa kofi la shavuni na muumini wa dini ya Kiislamu katika Baraza la Maulidi mara baada ya kuwataka Waislamu kujikinga na Ukimwi kwa kutumia kondomu kuliko kuwaambukiza watu gonjwa hilo hatari kwa jamii.
Mwinyi aliendelea kudai kuwa mtu akifanya zinaa, kwa kutumia mpira (kondomu), atakuwa amefanya dhambi moja, lakini akifanya bila kutumia mpira, mtu huyo ni dalali wa kutembeza zinaa na Ukimwi.
Baada ya hapo akauliza mashekhe, kwamba kufanya dhambi Mungu anaweza akasamehe, lakini yule ambaye atafanya dhambi bila kondomu, bora ni vipi?
Mwinyi akaendelea kusema: “Dharura ya mtu asiyeweza kujizuia na kufanya zinaa, mashekh na maulamaa tufanyeje hapo?”
Baada ya kusema hivyo, akatoka muumini mmoja akapanda jukwaani na kumpiga Rais Mwinyi kofi upande wa shavu la kuume, akapepesuka almanusra aanguke na kuokolewa na maafisa usalama.
Baada ya kumdhibiti mtu huyo ambaye alitia dosari sherehe hizo zilizokuwa zimeandaliwa vizuri, wanausalama hao walimpakia kwenye gari na kuondoka naye.
Baadhi ya waumini walitaka kukimbia, wengine wakaenda kuwasaidia maafisa usalama kumkabili mtu huyo aliyempiga Rais Mwinyi maarufu kama Mzee Ruksa.