Bongo5 Makala

Utata wa KTMA: Ni nani alistahili kuwa producer bora wa muziki mwaka jana?

Mwaka huu tuzo za muziki za Kilimanjaro hazijawa na malalamiko kwenye vipengele vingi kama ilivyokuwa miaka iliyopita. Pamoja na Diamond kuzoa tuzo zote saba alizotajwa, ni ushindi wa Fid Q pekee ndio ulioshangiliwa na tu wengi zaidi.

page

Sababu ni kwamba pamoja na rapper huyo ambaye jina lake ni Fareed Kubanda kuaminika kwa wengi kuwa ndio mwandishi hatari zaidi wa mashairi ya Hip Hop, alikaa miaka 7 bila kupata tuzo yoyote.

Ndio maana katika mahojiano niliyofanya naye, Fid alisema ushindi wake mwaka huu ni sawa na saa iliyopoteza majira kupatia muda na kwamba kitu kizuri katika kushinda tuzo ni pale kila mtu anapofurahi, na ndivyo ilivyokuwa kwake.

Hata hivyo, ni katika kipengele kimoja tu, watu wengi wanaonesha kutoridhika na mshindi, nacho ni kile cha mtayarishaji bora wa muziki wa kizazi kipya ambacho kilienda kwa Man Walter. Wengi wanasema producer huyo hakustahili.

Na kama ulikuwepo ukumbini siku ya utoaji wa tuzo hizo, utakubaliana name kuwa baada ya jina lake kutajwa, ni watu wachache mno walioshangalia tofauti na ilivyokuwa kwa washindi wengine. Mbaya zaidi, kutokana na furaha nyingi kumjaa, producer huyo alijikuta akifunguka maneno mengi ya furaha hadi ukumbi ukaanza kumzomea na akazimiwa kipaza sauti.

Ushindi huo, ulimuumiza producer wa wimbo wa Diamond, My Number One, Sheddy Clever aliyeandika:

“Ndugu zangu hivi nitashindwa vp kuchukua tuzo ya producer bora wa mwaka wakati nimetayarisha wimbo uliochukua tuzo ya wimbo bora wa mwaka na ni wimbo ambao umemfanya Msanii @diamondplatnumz aweze kuchukua tuzo zaidi ya 5 #ktma hii inaonesha kua muziki we2 watanzania bado unahitaji elimu ya kutosha ila cna maana mbaya hapana bt nawashukuru saaana #ktma kwa kazi walio fanya pia.”

Kilio chake kiliungwa mkono na producer mkongwe nchini, Master J aliyesema;

“Sijaelewa Diamond kupata tuzo 7 halafu produza wake kutoka na 0.”

Wengi wanaomuunga mkono Sheddy, wanaamini kuwa ili hesabu ikamilike vizuri, ushindi wa tuzo saba wa Diamond ulikuwa ni tiketi ya moja kwa moja kwa producer wake kuchukua tuzo ya mtayarishaji bora wa muziki. Hata hivyo producer wa Transorfmax, Lucci alidai kuwa, hit moja pekee isingetosha kumfanya Sheddy achukue tuzo hiyo.

“Kama producer mwenzako wacha nikuelimishe kidogo mdogo wangu,”
Lucci alisema.

“Kwanza, kamwe hujawahi kunisikia mimi nikilalamika kwamba sijapata hata nomination moja kwenye kili awards pamoja na kufanya hits zote kubwa za Cpwaa..Kwanini? kwasabubu it takes more than just a hit song…its takes consistency brother. Watu waone hujabahatisha…kama ningefanya hits zote za Cpwaa ndani ya mwaka moja halafu nisiingie kwenye category hapo sawa, ila kwa nyimbo moja tu au mbili kwa mwaka bado haitoshi. I did Jikubali ambayo ilikua ni kama anthem (ukiacha Ngololo) lakini hata nomination haijapata but hatujapiga kelele. Kwanza shukuru Mungu sana you were even a nominee. Yes production matters kwenye ubora wa wimbo tena sana sana sana lakini, tafakari mwenyewe moyoni mwako je; what made “Number one” a huge hit…was it your production zaidi au Diamond’s establishment as an artist and the love kila mtu aliyonayo kwake? Jibu ni lako wewe na Mungu wako…anyway…hongera walao kwa nomination uliyopata pamoja na kua mpya kwenye game..big up Sheddy.”

Naye mtangazaji wa Magic FM, Salma Msangi ‏alidai kuwa yaliyomtokea Sheddy ndiyo yaliyowahi kumtokea Man Walter kipindi 20 Percent aliponyakua tuzo tano kwa mpigo.

“Hata kipindi alichopata tuzo 5 20% Man water hakupata. . So producer wa wakati huo hakustahili #Historia Imejirudia,” alitweet mtangazaji huyo.

Pamoja na Sheddy Clever na Man Walter, wengine waliokuwa wakishindania kipengele hicho ni pamoja na Nahreel, Marco Chali na C9. Ni nani sasa alistahili kuwa mtayarishaji bora mwaka huu?

Kwa mtazamo wangu (ambao sio lazima uwe sahihi) ukiangalia sababu kama idadi ya hits alizofanya, ubora wa nyimbo zenyewe kwa maana ya kiufundi zaidi, Nahreel alistahili kushinda mwaka huu.

Nahreel ni producer wa miaka mingi na aliyetengeneza hits nyingi sana lakini ni mwaka jana ndipo alipokuwa amesettle zaidi kufanya kazi hiyo baada ya kuwa huru kutokana na kumaliza masomo yake nchini India.

Nahreel ni producer aliyekamilika na mwenye uwezo mkubwa wa kutengeneza nyimbo za aina mbalimbali. Wengi walikuwa wakimfahamu kwa beat zake za Hip Hop zaidi, zikiwemo zile alizomtengeneza Joh Makini miaka kadhaa iliyopita mfano ‘Copy My Motion’.

Kwa mwaka jana, Nahreel alitengeneza hits zikiwemo za ‘Nje ya Box’ na ‘Bei ya Mkaa’ za Weusi, nyimbo za kundi lake la Navy Kenzo ukiwemo ‘Chelewa’ na ‘Hold Me Back’, ‘Come Over’ ya Vanessa Mdee, ‘Ball Player’ ya Izzo B aliyowashirikisha Ngwair na Quick Rocka na ‘Love Me’ ya Izzo aliowashirikisha Barnaba na Shaa.

Hizo ni baadhi tu ya nyimbo alizozitengeneza mwaka jana mkali huyo ambazo hakuna anayeweza kubisha kuwa zilihit ile mbaya. Mkusanyiko wa nyimbo hizo ndio unaozalisha sifa ya kuwa ‘consistency’ aliyoisema Lucci kwenye mtazamo hapo juu.

Pengine ili kuona ukali wa Nahreel, ni bora kuzifahamu pia hits alizozifanya mwaka huu ambazo ni pamoja na ‘Gere’ ya Weusi, ‘Mfalme’ ya Mwana FA f/ G-Nako, My Papa ya Feza Kessy.

Hivyo pamoja na kwamba kura nyingi zilimwendea zaidi Man Walter, kwa mtazamo wangu ni Nahreel ndiye aliyekuwa anastahili kushinda mwaka huu. Nyimbo pekee za Man Walter zilizofanya vizuri mwaka jana ni ‘Yahaya’ na ‘Joto Hasira’ za Lady Jaydee na ‘Tupogo’ ya Ommy Dimpoz’ (ambayo aliitengeneza kwa kushirikiana na Marco Chali).

Kwahiyo kwa idadi ya hits zilizofanyika mwaka jana, Nahreel alikuwa nazo nyingi zaidi kumzidi Man Walter. Hata hivyo katika masuala ya tuzo hasa yanayohusisha upigaji kura, hilo linaweza lisiwe kigezo na kura za wananchi ni muhimu ziheshimiwe. Wananchi ndio walioona Man Walter ni producer bora wa mwaka jana.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents