Michezo

Video: Oscar Pistorius atoa ushahidi kwa kilio na kutetemeka, ‘nikiamka nanusa harufu ya damu’

Mwanariadha mlemavu wa miguu wa nchini Afrika Kusini, Oscar Pistorius jana alitoa ushahidi wake kwa mara ya kwanza. Akiongea kwa uchungu, majonzi na sauti ya kutetemeka, mwanariadha huyo alidai kuwa hajawahi kuisahau familia ya aliyekuwa mpenzi wake Reeva Steenkamp tangu amuue kwa risasi February 14 mwaka jana.

Pistorius aliiomba radhi familia ya Steenkamp kwa kitendo alichokifanya. “Kila siku wao ni watu wa kwanza huwa nawaombea,” aliiambia mahakama kuu mjini Pretoria, baada ya kumuomba jaji Thokozile Masipa ruhusa ya kuongea na familia ya Steenkamp iliyokuwa imekaa mahamakani.

Alisema akiwa mdogo, alimshuhudia mama yake ambaye ni marehemu akilala na bunduki chini ya mto na akiwa mtu mzima alianza kulala na bunduki yake, ile ile iliyomuua mpenzi wake Steenkamp. Ulikuwa ni uoga huo wa matukio ya kihalifu uliomjengea hofu yake. Magari yaliwahi kumfuata katika nyakati mbalimbali na kuwaliwahi kufanyika jaribio la kumteka kaka yake.

Alisema kwa sasa si uhalifu unaomweka macho usiku kucha bali ni harufu ya damu na kwamba kwa sasa ameapa kutoshika tena bunduki na amekuwa akitegemea dawa za usingizi ili kulala. Aliongeza kuwa usiku huota ndoto za ajabu zinazomkumbusha siku ya tukio hilo kiasi ambacho kuna wakati alishindwa kulala kabisa na kumuita dada yake aje kwake.

Mwanariadha huyo alisema kukutana na Steenkamp, kulikuwa ni baraka kwake. “Nimeweka imani nyingi kwa Mungu kufika nilipotaka kuwa na nilipokutana na Reeva, nadhani ilikuwa ni baraka. Siku zote nilikuwa nataka kuwa na mwenza ambaye ni mkristo. Alikuwa mkristo imara. Alikuwa akiniombea usiku na alikuwa akiombea mazoezi yangu- vitu vyote vidogo. Dini yake ndio iliyonivukisha mwaka wote uliopita,” alisema Pistorius aliyekuwa akiongea kwa sauti ya kulia.

Leo ataendelea kutoa ushahidi wake baada ya jana kuomba apumzike kutokana na uchovu.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents