Habari

Wakili aigeuzia kibao TAKUKURU

UPANDE wa utetezi katika kesi ya kuhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Costa Ricky Mahalu na Grace Martin, umeiambia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, kwamba Taasisi Kupapambana na Kuzuia Rushwa Tanzania (TAKUKURU) haikuwa na mamlaka ya kisheria ya kuendesha kesi hiyo.

na Happiness Katabazi


UPANDE wa utetezi katika kesi ya kuhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Costa Ricky Mahalu na Grace Martin, umeiambia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, kwamba Taasisi Kupapambana na Kuzuia Rushwa Tanzania (TAKUKURU) haikuwa na mamlaka ya kisheria ya kuendesha kesi hiyo.


Hoja hiyo ilitolewa na wakili wa utetezi, Cuthbert Tenga wakati akijibu hoja za upande wa mwanasheria wa Takukuru, Tabu Mzee, ambaye jana aliwasilisha kielelezo ambacho ni Gazeti la Serikali.


Mzee alidai kuwa kielelezi hicho ndicho kinaruhusu taasisi hiyo kuendesha kesi hiyo na kuongeza kuwa, upande wa mashtaka una mamlaka ya kuendesha kesi hiyo dhidi ya washtakiwa tangu ilipofunguliwa mahakamani Januari 11, mwaka huu.


Akijibu hoja za wakili wa Takukuru, wakili Tenga alisema anashangazwa na taasisi hiyo kuendesha kesi hiyo inayowakabili wateja wake wakati haina mamlaka ya kisheria ya kuiendesha.


Tenga ambaye alianza kupangua hoja za upande wa mashtaka baada ya kupitia kielelezo chao, alisema kupitia kielelezo hicho upande wa utetezi umebaini kwamba mamlaka waliyopewa ya kuendesha kesi za kuhujumu uchumi yameanza rasmi Agosti mwaka huu na yametokana na mabadiliko ya sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya mwaka 2007.


Alisema Januari mwaka huu, wakati Takukuru ilianza kuendesha kesi hiyo, ilikuwa inafahamu fika kwamba haina mamlaka hayo, lakini kwa sababu inazozijua, iliamua kukaidi sheria za nchi na kuamua kuiendesha.


“Aliyepaswa kufungua na kuendesha kesi hii ni DPP siyo nyie Takukuru… ebu tuwaulize ni nani aliwatuma kufungua kesi hii na huku mkijua wazi hamna mamlaka ya kuendesha kesi hii? Ielezeni mahakama au mna maslahi yenu binafsi katika kesi hii?” alihoji Tenga na kusababisha mawakili wa upande wa mashtaka wakijiinamia huku wananchi walioudhuria katika kesi hiyo kuangua vicheko.


“Na kwa jinsi hii, ndipo ninapokubaliana na maelezo ya Mkurugenzi wa Takukuru, Dk. Edward Hosea, aliyoyatoa kwenye vyombo vya habari hivi karibuni, kwamba ofisi yake inakabiliwa na matatizo katika uendeshaji wa mashtaka,” alisema na kusababisha tena watu kuangua vicheko.


Tenga alisema kwa sababu Takukuru haikuwa na mamlaka ya kufungua kesi hiyo, akaiomba mahakama hiyo ifute kesi ya msingi inayowakabili wateja wake.


Naye wakili mwingine wa utetezi, Alex Mgongolwa, aliieleza mahakama kwamba hati ya maelezo ya mlalamikaji kwanza aibainishi kosa na wala haiwataji washtakiwa kama wamefanya kosa lolote.


Baada ya kusikiliza hoja hizo za pande mbili na kupokea vielelezo toka upande wa mashtaka, Hakimu Mkuu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Sivangilwa Mwangesi, aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 22, mwakani, na siku hiyo ndiyo atatoa uamuzi kuhusu hoja zilizotolewa na pande hizo mbili.


Mahalu na Grace, Januari 11 mwaka huu, walifikishwa katika mahakama hiyo wakikabiliwa na kosa la kuhujumu uchumi, ambapo inadaiwa kwamba wakiwa watumishi wa serikali katika Ubalozi wa Tanzania nchini Italia, mwaka juzi, waliibia sh bilioni 3 mali ya serikali.


Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents