Habari

Wananchi waomba Bunge kumuongezea muda Rais Magufuli madarakani

Wananchi wa vijiji vya Bulangwa na Katente mkoani Geita wameliomba Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufanya marekebisho ya muda wa ukomo wa urais kutoka miaka 10 ya sasa hadi miaka 20 ili kumuwezesha Rais Dk. John Pombe Magufuli kuendelea kubakia madarakani kunusuru rasilimali za taifa.

Wananchi hao wametoa ushauri huo katika mkutano wa hadhara ulioitishwa na mbunge wa jimbo la Bukombe Mh. Dotto Biteko kwa ajili ya kumpongeza Rais Dk. John Pombe Magufuli kwa namna anavyosimamia rasilimali za nchi.

Akiwahutubia wananchi Mbunge wa jimbo la Bukombe ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati ya Nishati na Madini Mh. Dotto Biteko amesema kazi ya kupigania rasilimali za taifa inayofanywa na Rais Dk. John Pombe Magufuli sio ya lelemama.

Ripoti ya kamati ya pili ya mchanga wa madini (Makinikia) iliyowasilishwa Juni 12 mwaka huu kwa Rais Magufuli na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Prof. Nehemiah Osoro ilibaini taifa linapoteza shilingi Trilioni 168 kupitia usafirishaji wa mchanga wa madini ya makinikia nje ya nchi kuanzia mwaka 1998 hadi kufikia Marchi mwaka huu.

Ripoti hiyo ya pili ilihusisha baadhi ya Mawaziri wa zamani wa nishati na madini kuhusika na mikataba mibovu iliyopelekea taifa kupoteza rasilimali.

Chanzo:ITV

By Godfrey Mgallah

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents