Habari

Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson akalia kuti kavu, ni baada ya kusitisha shughuli za bunge

Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson amepuuza wiito wa kujiuzulu, baada ya uamuzi wa mahakama ya juu kwamba hatua yake ya kuahirisha bunge ilikuwa kinyume na sheria. Vikao vya bunge vimeitishwa tena leo siku ya Jumatano.

UN-Vollversammlung in New York | Boris Johnson, Premierminister Großbritannien (picture-alliance/dpa/S. Rousseau)

Uamuzi huo wa mahakama ya juu zaidi nchini Uingereza umeungwa mkono kwa kauli moja na majaji wake wote 11, hali ambayo inazidisha uzito wa uamuzi huo, na matatizo kwa waziri mkuu Boris Johnson.

Rais wa mahakama hiyo, Lady Hale amesema hatua ya serikali ilikuwa na malengo ya kulitatiza bunge kufanya majukumu yake.

”Kwa hiyo mahakama imehitimisha kwamba uamuzi wa kumshauri Malkia kusitisha shughuli za bunge ulikuwa kinyume na sheria, kwa sababu matokeo yake yalilitatiza bunge, au yalilizuia bunge kufanya majukumu yake ya kikatiba, bila sababu yoyote ya msingi.” Amesema rais huyo wa mahakama ya juu ya Uingereza.

Großbritannien Supreme Court | Lady Brenda Hale, Richterin (Reuters/Supreme Court/Parliament TV)Rais wa Mahakama ya Juu ya Uingereza Lady Brenda Hale

Johnson ajikaza kisabuni

Akizungumza kwa mara ya kwanza baada ya uamuzi huo wa mahakama mjini London, Boris Johnson ambaye yuko mjini New York akihudhuria Hadhara Kuu ya Umoja wa Mataifa, amepuuza miito iliyotolewa na wanasiasa mbali mbali wakimtaka ajiuzulu, akisema kuwa kwa maoni yake, uamuzi wa mahakama ya juu haukuwa sahihi.

Amesema, ”Inabidi niseme kwamba napingana vikali na uamuzi wa majaji. Sidhani kama ni sahihi, lakini bila shaka tutasonga mbele, na vikao vya bunge vitafanyika tena.”

Kwa mujibu wa shirika la habari la Deutsche Welle, Katika hukumu yake, mahakama ya juu imesema hivi sasa ni wajibu wa viongozi wa bunge kuamua muda wa kuanza tena vikao vyao, na tayari spika wa baraza la chini John Bercow, amesema milango ya bunge huko Westminster itafunguliwa leo Jumatano.

Großbritannien Debatte zum Brexit im Unterhaus in London | John Bercow, Speaker (picture-alliance/empics/House of Commons)Spika wa bunge la Uingereza John Bercow

Spika huyo amesema uamuzi wa mahakama ya juu ni wa kihistoria, na kwamba raia wanayo haki ya kuona wawakilishi wao wakitimiza majukumu yao ya kikatiba, ya kuishinikiza serikali kuwajibika.

Miito ya kumtaka ajiuzulu yahanikiza

Miongoni mwa wanasiasa waliomtaka waziri mkuu Boris Johnson kujiuzulu ni kiongozi wa chama kikuu cha upinzani cha Labour, Jeremy Corbyn, ambaye amemtuhumu Johnson kuidharau misingi ya demokrasia na utawala wa sheria.

Waziri kiongozi wa Scotland, sehemu ya Uingereza yenye mamlaka ya ndani Nicola Sturgeon amekwenda mbali, na kusema ikiwa Johnson hatokuwa na ujasiri wa kujiuzulu mwenyewe, basi wabunge waungane na kumtimua madarakani.

Mratibu wa masuala ya Brexit katika bunge la Umoja wa Ulaya Guy Verhofstadt, amesema hatimaye, katika mvurugano wa Brexit, imedhihirika kuwa utawala wa sheria nchini Uingereza bado uko hai na wenye nguvu.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents