Gari Dar lazama

Mvua za masika zinazoendelea kunyesha nchini zimeendelea kuleta maafa katika sehemu mbalimbali nchini ambapo Jijini Dar, dereva mmoja amenusurika kufa baada ya gari lake kusombwa na maji na kisha kuzama kwenye Mto Msimbazi

Na Mwandishi wa Alasiri, Ukonga


 


Mvua za masika zinazoendelea kunyesha nchini zimeendelea kuleta maafa katika sehemu mbalimbali nchini ambapo Jijini Dar, dereva mmoja amenusurika kufa baada ya gari lake kusombwa na maji na kisha kuzama kwenye Mto Msimbazi.


Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia leo katika eneo la Vingunguti wakati gari aina ya Nisan Patrol almaarufu kama `shangingi` liliposombwa na maji baada ya kutumbukia kwenye mto huo wa Msimbazi wakati likijaribu kuvuka .


Watu walioshuhudia tukio hilo, wanasema baada ya gari hilo kusombwa na maji hadi kwenye kina kirefu, dereva huyo aliweza kufungua mlango na kupanda juu ya boneti la gari ili kujiokoa.


Shuhuda mmoja ameiambia Alasiri kuwa baada ya dereva huyo kupanda juu ya boneti la gari lake, hakuweza kutoka mtoni kwa vile maji ya mto yalikuwa yakienda kwa kasi na nguvu ambayo ingeweza kuhatarisha maisha yake.


Akasema kuwa baada ya wananchi kuona hivyo wakawapigia simu Polisi, ambao walifika mara moja kutoa msaada kwa dereva huyo.


Msimuliaji huyo akasema polisi pia iliwabidi kuomba msaada kwa kikosi cha Zimamoto na uokoaji, waliofika wakiwa na winchi iliyotumika kumuopoa dreva huyo kutoka mtoni.


Alipoulizwa na Alasiri, Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, Faustine Shilogile amethibitisha kuokea kwa tukio hilo, na kumtaja mmiliki wa gari hilo ambaye pia alikuwa akiliendesha kuwa ni Bw. Antony Dibayuka mkazi wa Chang`ombe.


Pia Kamanda Shilogile akalitaja gari hilo kuwa ni lenye namba za usajili T 331 ACP aina ya Nisan Patrol.


Akisimulia zaidi tukio hilo, Kamanda Shilogire amesema Bw. Dibayuka alikuwa akitokea mjini kwenda nyumbani kwake kupitia njia ya Vingunguti na kuwa alipofika mtoni hapo alikuta maji machache na kuamua kupitisha gari.


Akasema gari hilo likanasa kwenye tope na kushindwa kuondoka, ndipo maji yalipoongezeka na kulisomba, kabla ya Bw. Dibayuka kupanda juu ya boneti na kuomba msaada wa polisi.


Kamanda Shirogile akasema Polisi kwa kushirikiana na kikosi cha Zimamoto walifanikiwa kumwokoa Bw. Dibayuka akiwa salama na tayari gari lake pia limeshatolewa mtoni.


Kamanda Shilogile ametoa wito kwa wananchi kutoudharau mto huo kwani unaweza kuwaletea madhara hata unapokuwa na maji yasiyoonekana kuwa mengi.


 


Source: Alasiri

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents