Habari

Wanaapolo wapora madini ya mamilioni CCM

KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, kundi la watu wanaodhaniwa kuwa ni wachimbaji wadogo wa madini, juzi walivamia gari lililobeba mchanga wenye madini mali ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) wilayani Simanjiro na kuiba kiasi kikubwa cha madini ya tanzanite yenye thamani ya mamilioni ya shilingi.

na Mwandishi Wa Tanzania Daima, Simanjiro

 

KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, kundi la watu wanaodhaniwa kuwa ni wachimbaji wadogo wa madini, juzi walivamia gari lililobeba mchanga wenye madini mali ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) wilayani Simanjiro na kuiba kiasi kikubwa cha madini ya tanzanite yenye thamani ya mamilioni ya shilingi.

 

Imeelezwa kwamba, waporaji walifanikisha wizi huo kwa kutumia silaha za jadi.

 

Habari zilizolifikia Tanzania Daima Jumapili kutoka Mirerani, wilayani Simanjiro zinasema kwamba, madini hayo yaliporwa juzi, majira ya saa tisa alasiri katika Kijiji cha Naisinyai na kundi la watu wanaosadikiwa kuwa wachimbaji wadogo wa madini, maarufu kwa jina la Wanaapolo.

 

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Luther Mbutu, jana alithibitisha kutokea tukio hilo na kueleza kuwa waporaji walioonekana kuzinasa mapema habari kuhusu mchanga wa madini hayo, walilivizia gari lililobeba mchanga na lilipokaribia mahali walipokuwa, walitanda haraka katikati ya barabara.

 

Kwamba, baada ya kuona gari hilo linakuja bila kupunguza mwendo, waliamua kulala chini katikati ya barabara, jambo lililomlazimu dereva kusimama, pengine bila kutambua kwamba huo ulikuwa sawa na ushindi kwa waporaji hao.

 

Taarifa za awali za kipolisi zilieleza kuwa, kundi hilo la watu, wakiwa na silaha mbalimbali za jadi waliliteka gari aina Isuzu Canter, lenye namba za usajili T 443 AAR, mali ya mtu binafsi lililokuwa likiendeshwa na dereva aliyetambuliwa kwa jina la Davis Japhet (27).

 

Watekaji hao wakiwa wamelala chini, walilishambulia kwa mawe gari hilo na kupasua kioo chake cha mbele na baada ya kumteka dereva, walimjeruhi kwa sime, kisha wakaanza kuyasaka madini hayo kwenye mchanga.

 

Taarifa hizo za kipolisi zilieleza zaidi kuwa, mchanga huo ambao ndani yake kulikuwa na madini ya tanzanite, ulitolewa na Kampuni ya Tanzanite One kwa UVCCM, Wilaya ya Simanjiro.

 

“Inashangaza kweli, watu wameteka gari, wamemjeruhi dereva kwa sime, wameiba madini yenye thamani kubwa! Dereva huyu amelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru, anakopatiwa matibabu zaidi.

 

“Madini hayo ya tanzanite yalikuwa yamechanganyika kwenye mchanga ambao imegundulika kuwa ulitolewa na Kampuni ya kuchimba madini ya Tanzanite One kwa Jumuiya ya Vijana ya Chama Cha Mapinduzi, Wilaya ya Simanjiro.

 

“Kinachoshangaza hapa, ni hawa watu kuamua kusafirisha mchanga wenye mchanganyiko wa madini yenye thamani kubwa bila ya kuomba msaada wa ulinzi wa Jeshi la Polisi, msaada ambao unatolewa bure, haulipiwi!” alisema kwa mshangao Kamanda Mbutu.

 

Alisema pamoja na masako mkali unaofanywa na jeshi hilo, bado halijafanikiwa kuwanasa waporaji hao na kwamba, dalili za awali zinaonyesha kuwa hawatakuwa tena eneo hilo.

 

Hata hivyo, alieleza kuwa jitihada za polisi kuwasaka zinaendelea na watakapopatikana watafikishwa mahakamani kwa mujibu wa sheria.

 

Alisema katika tukio hilo la kupora madini hayo, hakuna uharibifu mkubwa wa mali uliosababishwa na waporaji, lakini taarifa za awali zinadai kuwa, madini hayo yanaweza kuwa na thamani ya mamilioni ya shilingi.

 

Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents