Burudani

Adam Shafi: Serikali imewatelekeza waandishi wa vitabu, inajali muziki na filamu tu

Mwandishi mkongwe wa vitabu vya riwaya hapa nchini, Shafi Adam Shafi, amesema kwa muda mrefu, serikali imewageuzia mgongo waandishi wa vitabu na kwamba wizara husika imekuwa ikiwajali waimbaji na waigizaji wa filamu tu.

Shafi
Adam Shafi (wa pili kutoka kulia) akiwa kwenye picha ya pamoja baada ya uzinduzi wa Umoja wa Waandishi wa Riwaya wenye Dira (Uwaridi), Alhamis hii jijini Dar es Salaam

Mzee Shafi alisema sekta ya uandishi wa vitabu imekuwa na uharamia mkubwa na kuwaacha waandishi wakiwa na dhiki kuu huku serikali ikishindwa kabisa kutetea maslahi yao.

“Vitabu vingi vinaibiwa, hawa maharamia wamekaa chini wamesubiri tu kitabu gani kitapitishwa ili kitumike mashuleni kikishapitishwa tu haraka wanachukua nakala moja au mbili wanakwenda zao Nairobi, au wanakwenda Dubai, India au Mauritius, wanakwenda wanarudufu hivi vitabu, wanavichapa, vinakuja nchini kwa makontena, vinaingia katika soko la vitabu,” alisema Shafi wakati akizungumza kwenye hafla ya ufunguzi wa Umoja wa Waandishi wa Riwaya wenye Dira (Uwaridi), Alhamis hii jijini Dar es Salaam.

“Na jinsi walivyokuwa mahodari wanaweza kuwalaghai wale wanaohusika na ununuzi wa vitabu katika ngazi za wilaya huko, manispaa na nini wachukue vitabu kutoka kwao. Kwa uharamia huu, waandishi wanakosa mrabaha, wachapishaji wanapata hasara, vinauzwa vile vilivyochapishwa na maharamia,” aliendelea.

Pamoja na hivyo, Mzee Shafi alisema mara nyingi anapokuwa akimsikia waziri wa habari, utamaduni, sanaa na michezo akiongelea vita dhidi ya uharamia, amekuwa akimaanisha ule unaofanyika kwenye muziki na filamu pekee.

“Kwake yeye waandishi hawapo, sijawahi hata siku moja kumsikia waziri wetu, au waziri yeyote, au rais wa nchi hii akizungumzia waandishi. Siku moja rais wetu mstaafu aliyepita hivi juzi, alitoa speech akawataja wasanii wote, akakava sekta zote, akazungumzia kila mtu aliyetoa mchango katika jamii lakini bahati mbaya waandishi hata mara moja hakumtaja. Yaani kwao wao waandishi hawapo, wao kuna wacheza filamu, waimbaji.”

Aliikumbusha serikali kuwa kabla ya muziki na filamu havijaingia sokoni, ni lazima mwandishi awe amehusika kuandika ikimaanisha kuwa ni watu muhimu. Pia aliongelea jinsi chama cha haki miliki nchini, COSOTA akidai kuwa nacho kimekuwa kikiongelea zaidi muziki na filamu.

Aliitaka serikali sasa kuwaangalia waandishi kama wasanii wengine na kuwasaidia katika matatizo yanayowakabili kwenye kazi zao.

Shafi Adam Shafi ni miongoni mwa waandishi nguli wa riwaya Tanzania na mshindi wa tuzo kubwa za uandishi duniani. Vitabu vyake maarufu ni pamoja na Kasri ya Mwinyi Fuad, Kuli, Vuta N’Kuvute, Haini, Mbali na Nyumbani.

Mgeni rasmi kwenye hafla hiyo alikuwa Mkurugezi Msaidizi Lugha Bibi Hajjat Shani Kitogo kutoka Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo aliyemwakilisha Waziri Nape Nnauye.

Umoja wa Waandishi wa Riwaya wenye Dira Tanzania (UWARIDI) umeanzishwa kwa lengo la kuwatetea waandishi wa riwaya nchini ili waweze kunufaika na kazi zao.

Viongozi wa UWARIDI ni pamoja na Hussein Tuwa (Rais), Ibrahim Marijani Gama (Katibu Mkuu) na Suleiman Kijogoo (Katibu Mwenezi).

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents