BurudaniHabari

Mh Temba; ‘Tattoo’ zilifanya atimuliwe jeshini

Mh TembaKumekuwepo na kauli tata ambazo mara zote zimekuwa hazikati kiu ya mashabiki juu ya kwanini msanii wa kundi la TMK Wanaume Family, Amani Temba

NMh Tembaa Ramadhan Kinyonya

 

Kumekuwepo na kauli tata ambazo mara zote zimekuwa hazikati kiu ya mashabiki juu ya kwanini msanii wa kundi la TMK Wanaume Family, Amani Temba ambaye hujulikana kwa jina la Mheshimiwa Temba, aliacha kazi jeshini na kuamua kuyakabidhi maisha yake katika muziki.

 

Wengi wamekuwa wakisikia kutoka kwake kwamba alihitimu mafunzo ya uaskari katika Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) na pia kwa kauli zake Temba, amekuwa akiileza jamii kuwa alikwishahitimu mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).

 

Kumekuwa kukisemwa mengi au yeye mwenyewe amekuwa akitaja kwa ufupi bila ufafanuzi juu ya kwanini alihitimu mafunzo yote hayo na ameishia au ameamua kuwa mwanamuziki na asiikamilishe ndoto yake ya kuwa mwanajeshi.

 

Kwa mujibu wa simulizi za maisha yake kabla na baada ya kuhitimu mafunzo yanayoonesha alikuwa akipenda kuwa mwanajeshi, ukweli ni kwamba Temba, alifanya kila awezalo na kufanikiwa kujiunga na mafunzo ya jeshi zaidi ya mara tatu, na mara zote alifanikiwa kuhitimu mafunzo, lakini mara zingine kabla hajakabidhiwa ajira anajikuta anaachishwa au anaacha na kisha anarudia tena mafunzo.

 

Huu ni ushahidi kwamba alikuwa akilipenda jeshi kutoka moyoni lakini kuna sababu ilikuwa ikimkwamisha, na sababu hii inaweka bayana kwamba kamwe hataweza tena kuwa mwanajeshi kwa mujibu wa sheria za kitaifa na kimataifa.

 

Jambo hili ndio maudhui ya makala hii kwani mbali ya kulitambua lakini itakuwa ni funzo kwa jamii, hususan kwa vijana wa kike na wa kiume wanaopenda kuiga na kufanya mambo wakidai au wakidhani ndio ujana kumbe mengi kati ya hayo yana athari wakati ujao wa maisha yao.

 

Katika mahojiano maalumu na Majira, msanii huyo ambaye tungo zake zimemdhihirisha yuko ‘matawi ya juu’ na mwenye kipaji cha aina yake, Temba anasema alifanya jambo hilo bila kujua kama lingekuja kumkwaza katika kufikia aliyokuwa akiyatamani.

 

Temba anabainisha sababu kuu ya yeye kutoswa jeshini na kulazimika kuachana na ndoto za kuwa askari kunatokana na kujichora chata ‘tattoo’ kochokocho katika mwili wake.

 

‘Tattoo’ ni michoro ambayo mtu hujichora alama ya kitu anachokipenda kwa wino maalumu usiofutika ama unaofutika katika sehemu mbalimbali za mwili na wengi hupendelea zaidi sehemu za kifua, bega, mkono, mgongo na kwa wanawake hupendelea kuweka ‘tattoo’ kiunoni au kwenye mapaja.

 

Uchunguzi unaonesha wanawake wengi hupenda kujichora ‘tattoo’ chini ya kitovu, juu ya matiti na kiunoni chini ya mgongo, wengi huona ni mapambo, lakini moja ya madhara yake ni hayo.

 

Lakini kutokana na kuwepo kwa ugonjwa wa UKIMWI, wataalamu wanasema kujichora huko pia husababisha kwa asilimia 70 maambukizi ya maradhi hayo.

 

Hii inatokana na namna ya kujichora hiyo ‘tattoo’, kwani hutumika sindano katika kuichora picha iliyokusudiwa ambapo huchomwa mpaka eneo husika likatoka damu.

 

Temba anasema ameridhia kuzungumzia suala hilo linalohusu undani wa maisha yake kwa makubaliano maalumu, ili makosa hayo aliyoyafanya bila kujua yawe mfano kwa vijana na vizazi vijavyo.

 

Awali, Temba alikataa kuzungumzia hilo, lakini baada ya kubembelezwa kwamba yeye ni msanii na moja ya kazi zake ni kuelimisha jamii kwa mazuri au mabaya, hatimaye msanii huyo anayetoka kabila la Wachagga, alikubali na kuweka bayana mambo yalivyokuwa.

 

Kwa mtazamo wa juu juu jambo hili la mtu kujichora mwili, linaonekana kama dogo, lakini kumbe madhara yake ni makubwa, na ubaya zaidi inaonekana hivi sasa limekuwa likidandiwa na vijana wengi tena kwa kasi ya kutisha.

 

Temba anasema ‘tattoo’ hizo hazifai kwa jamii kwa vile zinatia hasara katika maisha kama yeye ilivyomtokea hadi kutimuliwa jeshini.

 

‘Tattoo’ hizo ndizo zilimfanya apoteze ajira jeshini licha ya kwamba alikuwa na sifa kochokocho ikiwa ni pamoja na kiwango kizuri cha elimu ya kuanzia na ziada, lakini baada ya kubainika alikuwa na mchoro mmoja tu katika mwili wake, alisimamishwa kazi.

 

Anadokeza kwamba kibaya zaidi ilifikia mahali akataka kushitakiwa kijeshi na anasema maudhui ya kukubali kuanika hadharani ni kutokana na kutaka kuifundisha, kuitahadharisha jamii juu ya kuwa makini katika mambo wanayofanya hususan vijana ambao mengi wanaiga bila kujua madhara yake ni makubwa.

 

Temba anasema tangu akiwa mtoto alikuwa na ndoto ya kupenda au kutamani kuwa mwanajeshi, lakini anasikitika kwamba ndoto yake hiyo iliyeyushwa na ‘tattoo’ aliyojichora mwilini.

 

Baada ya kuhitimu kidato cha sita mwaka 2000, Temba anasema alianza ‘mishemishe’ ya kujiunga na jeshi na hatimaye Oktoba 22, 2001 alifanikiwa kujiunga na mafunzo ya JKT.

 

Alikuwa ni mingoni mwa vijana wapatao 2,000 walioandikishwa na kusajiliwa kuanza mafunzo katika kambi ya JKT Ruvu.

 

Anasema mafunzo yalikuwa magumu na waliyapachika jina la ‘Oporesheni Mkapa’ na anasema zaidi ya robo tatu ya vijana waliohitimu wana kazi zao za uhakika kwa waliojiajiri na walioajiriwa, anadokeza kuwa karibu wote ‘wako njema’.

 

Temba anasema aliendelea na mafunzo, lakini akiwa katika hatua za mwisho za kuhitimu ‘msoto’ huo, alishtukiwa zikiwa zimebakia wiki mbili na hivyo kukosa cheti cha kuhitimu mafunzo hayo.

 

Temba anasema ilimuuma sana, lakini kutokana na jambo hilo kuwa moyoni mwake, alifanya ‘makeke’ na mwaka uliofuata akafanikiwa kupenya mpaka akasajiliwa kuanza mafunzo ya JWTZ.

 

Kwata la safari hii alipangwa katika kambi ya Mafinga mkoani Iringa. Temba anasema alichakarika na wenzake, lakini kama ilivyokuwa Ruvu, akashtukiwa tena zikiwa zimesalia wiki mbili tu kuhitimu na kuchukua ajira.

 

Anasema hiyo ilimuuma zaidi kutokana na jinsi aliyokubalika kwa maafande wenzake hadi akawa mfano kwa wengine, lakini ndio hivyo tena ikabainika kuwa ana ‘tattoo’, ikabidi atoroke.

 

Dalili za kipaji cha muziki alichonacho, zilianza kuonekana tangu akiwa jeshini ambapo alipata wasaa wa kutunga wimbo wake wa kwanza uitwao ‘Masikini Jeuri’.

 

Anasema wiki aliyofukuzwa jeshini alikuwa amekamilisha mashairi ya wimbo wake wa ‘Mpenzi Nakumaindi’ na anasema hizo ndizo ‘silaha’ alizotoka nazo jeshini alizoanza ‘kubangaiza’ nazo Bongo, akiwa kwa shangazi yake mitaa ya Temeke.

 

Katika hali inayoonesha bado alikuwa na mapenzi na Jeshi, mwaka 2003 alijikuta anaingia katika uhusiano na watoto wa kota za JKT Mgulani, ambapo alikuwa ‘akizuga’ kwa kucheza mpira wa kikapu.

 

Likaibuka ‘zali’, la nafasi ya ajira kwa wanamichezo jeshini, akafanya kweli katika kikapu akachaguliwa hadi timu ya taifa, aliporejea moja kwa moja akaingia kambini kuanza mafunzo ya JKT.

 

Safari hii akatupwa kambi ya Makutupora iliyoko Dodoma ambapo kwa vile alikuwa mwanamichezo, akawa hakaguliwi sana, akafanikiwa lakini akashtukiwa mwishoni wakati kambi imekwisha na ameshaanza kazi.

 

Jeshi halina utani, wakatumwa wachunguzi wakampeleleza mpaka wakagundua ni kweli ana ‘tattoo’, taarifa zikaenda makao makuu, ikabidi aachie ajira, kwani angefuatwa angestahili kushitakiwa kijeshi na huenda asingekuwepo katika ulimwengu wa muziki.

 

Baada ya ‘mishemishe’ hizo, akahamishia nguvu katika muziki akiwa na kundi la TMK Wanaume lililompatia mafanikio ambapo anasema ametoka katika kundi la watu wanaopigania usafiri wa daladala, sasa anamiliki gari lake lenye thamani ya sh. milioni 15.

 

Akizungumzia mipango yake katika muziki, anasema yuko katika hatua za mwisho za kumalisha albamu yake binafsi na anasubiri utaratibu wa kundi lake ili atoke.

 
Source: Majira

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents