Siasa

Bajeti yazidi kuliza wengi

BAADHI ya wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam, wameilalamikia bajeti ya serikali iliyotangazwa Alhamisi wiki iliyopita na Waziri wa Fedha, Zakia Hamdani Meghji kuwa inawakandamiza na kuwazidishia umasikini

na Mwandishi Happy Joseph, Happiness Katabazi, Shaaban Matutu, Asha Bani Na Irene Mark


BAADHI ya wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam, wameilalamikia bajeti ya serikali iliyotangazwa Alhamisi wiki iliyopita na Waziri wa Fedha, Zakia Hamdani Meghji kuwa inawakandamiza na kuwazidishia umasikini, kinyume na ahadi ya kuboresha maisha, ambayo imekuwa ikitolewa kila mara na Rais Jakaya Kikwete.


Wakizungumza na Tanzania Daima katika kutoa maoni yao juu ya bajeti hiyo, walisema bajeti hiyo imelenga kuumiza kwa kuwazidishia ukali wa maisha.


Baadhi ya waliotoa maoni yao, ni wafanyabiashara wadogo wadogo (wamachinga) ambao walieleza kuwa, bajeti ya mwaka huu imejaa vikwazo katika biashara zao.


Abdallah Magongo wa soko la Mchikichini, wilayani Ilala, Dar es Salaam, alisema kupanda kwa mafuta ya petroli ni chanzo cha kupanda kwa bidhaa zote muhimu, kwa sababu gharama za usafirishaji bidhaa zitakuwa juu.


Alisema serikali katika bajeti hiyo haikuzingatia kipato cha kila siku cha wananchi wake, bali imeangalia zaidi kuinufaisha serikali yenyewe.


“Rais wetu wa sasa alituahidi katika kampeni za mwaka 2005 kwenye kaulimbiu yake kuwa, kutakuwa na maisha bora kwa kila Mtanzania, lakini kwa bajeti hii, imekuwa kinyume, ni sawa na kusema maisha magumu kwa kila Mtanzania,” alisema mmoja wa wafanyabiashara hao.


Baadhi ya wanasheria wameeleza kuwa, bajeti imewafanya waamini maneno ya viongozi wa vyama vya upinzani, ambao kila kukicha wamekuwa wakisema ahadi ya Rais Kikwete ya kuleta maisha bora kwa kila Mtanzania ni usanii.


“Kama umesikiliza na kuichanganua hii bajeti, utakubaliana na mimi kwamba, wananchi masikini tutaendelea kuwa masikini, kwani bajeti inamkandamiza mwananchi kwa ari, nguvu na kasi mpya,” alisema mwanasheria wa kujitegemea, Theophil Rwegoshora.


Hata hivyo, baadhi ya wanachama wa chama tawala CCM, ambao walikataa kutaja majina yao, walisema bajeti hiyo ni lazima itasababisha mfumuko wa bei siku za usoni, hali itakayowafanya wananchi kushindwa kumudu gharama za manunuzi ya bidhaa na usafiri.


Yusuph Mnyenye, mfanyabiashara wa vinywaji jijini Dar es Salaam, alisema kwamba kupanda kwa kinywaji kama bia kutaathiri watu wa chini, kwa sababu wengi wao wanakitegemea kwa ajili ya kuwaburudisha siku za mapumziko ya mwisho wa wiki na sikukuu.


“Serikali imepandisha bia kwa sababu inajua fika machungu hayo hayatawapata viongozi, wao watakuwa wanakwenda kununua za jeshi kwa bei rahisi, lakini sisi wananchi wa hali ya chini tutaishia kunywa gongo,” alisema Mnyenye.


Aliongeza kuwa, iwapo bajeti hiyo itapitishwa, Watanzania wengi watarudi katika kinywaji cha gongo.


Kwa upande wa nishati ya mafuta, alieleza kuwa kupanda kwa bidhaa hiyo kutasababisha wananchi wengi waliokuwa wakitumia nishati hiyo kuanza kukata miti hovyo kwa ajili ya matumizi ya mkaa na kuni.


“Sasa iwapo mafuta yanapanda tena, matumizi ya kuni na mkaa yatakuwa maradufu na kusababisha vita dhidi ya ukataji wa miti kuendelea kushamiri,” alilalama Mnyenye.


Askari polisi mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini alisema anaiona bajeti kuwa ni sawa kutokana na kuwalenga watu wote na kuwa kila bidhaa au vitu ni lazima viwekewe kodi ili kulinda hali ya viwanda nchini kuporomoka.


“Si vizuri ukinitaja jina langu kwa kuwa silisemei Jeshi la Polisi, lakini naona ni sawa tu katika ulipaji wa kodi ya mapato kwa kuwa inatakiwa kulinda hali ya viwanda vya nchi yetu,” alisema askari huyo.


Mkurugenzi wa Youth Auction Volunteers (YAV), Irene Kiria, alieleza kuwa, fedha zilizotengwa kwa ajili ya elimu ni kidogo na serikali inaonyesha wazi kuwa haina nia ya dhati ya kupambana na adui ujinga.


Alisema, asilimia 18 ni fedha nyingi, lakini hazitoshelezi katika elimu kwa kuwa sekta hiyo ni muhimu, ina matatizo mengi yanayochangiwa na kutokuwepo kwa sera madhubuti za matumizi sahihi ya fedha za umma.


Katika fedha hizo, alisema zinahitajika zaidi ya sh bilioni 140 kwa ajili ya mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu, mishahara na stahili mbalimbali za watumishi wa wizara na walimu, ikiwa ni pamoja na kuajiri walimu kwenye shule za sekondari za kata.


“Kuzitaja fedha hizo ni nyingi, lakini matumizi yake hayatakuwa kama tunavyodhani, kwa sababu hakuna nidhamu ya matumizi ya fedha hizo,” alisema na kuongeza kwamba malipo ya safari na matumizi ya ziada yataongezeka.


“Hiyo asilimia 18 itawanufaisha wachache wizarani… watakaolipana posho za vikao, fedha za kuwapeleka walimu wapya kwenye vituo vya kazi na fedha kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi,” alisema Kiria.


Aidha, alisema mustakabali wa elimu hapa nchini hautakuwa bora kwa kuwa kiasi kilichotengwa hakitalingana na ugumu wa maisha utakaowakumba wananchi.


Bajeti iliyosomwa na Waziri Meghji yenye makadirio ya sh trilioni 6 imeongeza kodi katika bidhaa nyingi, lakini kubwa inayowagusa wengi imeonekana kuwa mafuta, kwani licha ya kupandisha gharama za maisha katika nauli, inaaminika hata bidhaa zitapanda kutokana na ongezeko hilo.


Habari hii imeandaliwa Na Happy Joseph, Happiness Katabazi, Shaaban Matutu, Asha Bani Na Irene Mark.


Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents