Habari

Exaud: Mabadiliko ya sera yatasaidia urahisishaji biashara mipakani

MKURUGENZI wa Shirika la Liberty Spark nchini, Evance Exaud amesema uwepo wa mabadiliko ya sera ni njia ya moja kwa moja itakayowasaidia watanzania kuingiza, kuuza au kufanya biashara mbalimbali bila vikwazo vyovyote mipakani.

Akizungumza hayo jijini Dar es Salaam katika mkutano wa majadiliano ya utafiti wa awamu ya pili ya Mradi wa Ujirani Mwema uliowaunganisha wadau mbalimbali ambao wanahusika moja kwa moja na masuala ya biashara ya mipakani.

Alisema endapo serikali ikafanya mabadiliko hayo ya kisera itasaidia kwa kiasi kikubwa mambo ya biashara hasa ya mipakani kufanyika ndani ya utaratibu na watu kupata taarifa sahihi.

Exaud alisema mradi wa ujirani mwema awamu ya pili,unalenga katika kuangalia matatizo au changamoto ambazo wafanyabiashara kutoka nchi moja au nyingine wanazozipata hususan katika biashara za mipakani katika Kilimo,Viwanda na Madini.

” Mradi unataka kuona Tanzania inafanyaje biashara za mipakani na nchi jirani ili kuweza kurahisisha biashara zao,licha ya uwepo wa changamoto mbalimbali ikiwemo utumiaji wa muda mrefu kutuma mizigo au uingizaji wa mizigo,masuala ya kikodi au sio kikodi pamoja na malipo kutokuwa sawa kisheria,”alisema na kuongeza

”Awamu ya kwanza ya mradi huu tuliweza kuangalia changamoto hizo na ndio maana awamu ya pili tumeweza kuangalia upande wa Kilimo,Madini na Viwanda na kuona kuwa kuna haja ya kuangalia masuala ya kikodi,”alisema.

Aidha alisema kilimo,viwanda na madini ni sekta zinazochangia asilimia 50 ya pato la Taifa huku asilimia 40 ya watanzania wanajikita katika kilimo hivyo sekta hizo zimekuwa ni sehemu ya kuchochea uchumi wa nchi.

Exaud alisema ili sekta hizo ziweze kukua ni lazima Watanzania wakawa wanapata masoko ya nje na kuuza na kusiwepo kwa vikwazo vyovyote vinavyozuia mfanyabiashara kushindwa kufanya biashara kwa nchi majirani kama Kenya,Uganda na Rwanda.

”Tangu tumeanza projecti hii tulikuwa tukifanya michanganuo ya mipaka yetu Tanzania na kuweza kuwaunganisha watu wa mipakani kutoka nchi zote na kuwasaidia wafanyabiashara kufanyabiashara katika mifumo isiyorasmi na kuingia rasmi,”alisema.

Kwa Upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Zanzibar (ZNCC), Hamad Hamad alisema vikwazo vya kisera na kikodi vinatakiwa kuhakikisha vinaondolewa ili kutoa fursa kwa wafanyabiashara kufanya biashara bila vikwazo.

”Tunatakiwa kuongeza hamasa ya upelekeji wa bidhaa nje ya Tanzania kwani tunapoingiza zaidi biashara nchini pato tunalopata linakuwa dogo kuliko tunapotoa zaidi biashara nje ya nchi tunakuwa tunaingiza fedha nyingi zaidi,”alisema na kuongeza

”Kupitia kupeleka bidhaa nje ya nchi zaidi ndipo tunaweza kufanya biashara za kikanda na kimataifa na dola kuingia kwa kiwango kikubwa nchini,”alisema.

Naye Mkurugenzi wa Utafiti na Elimu shirika la Liberty, Maiko Kihande alisema wamekuwa wakiwashauri watendaji juu ya kubadilisha sheria,taratibu au sera zilizopo ambazo wafanyabiashara wanazitumia ili kurahisisha watanzania kupata fursa za nje ya nchi kufanya biashara.

Written by Janeth Jovin

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents