Habari

Get 2 Know: Historia ya J’odie aliyeimba ‘KUCHI KUCHI’, ni kiongozi wa kwaya Nigeria (Audio)

Mwishoni mwa mwezi uliopita (January 29) mwenzangu Skywalker wa hapa BONGO5 aliandika makala kuhusu jinsi wimbo wa msanii wa Nigeria J’odie unaofahamika kama ‘Kuchi kuchi’ (Oh baby) unavyohit sana kwa sasa hapa kwetu Tanzania huku ulitoka takribani miaka 3 iliyopita.

Jodie-2
J’odie

Ila mimi binafsi kuna maswali yakanijia, kwamba kwa wimbo kama huo kupenya na kuwafikia watu wa vijijini ambao wengi wao utawasikia zaidi wakiimba ile sehemu ya kiitikio ‘kuchi kuchi aaaah, oh baby oh baby’ sababu ofcourse ndio rahisi zaidi kuweza kuishika hata kwa mtu ambaye hajui vizuri kiingereza inawezekana akaushika hiyo sehemu.

Yawezekana ukiwauliza aliyeimba ni nani wakakosa jibu, au yawezekana wakawa na jibu la swali hilo lakini ukiwapa picha za watu watatu wasichana na kuwauliza ni yupi kati ya hawa ni J’odie wanaweza wasimtambue, kwa maana nyingine ni wimbo ambao umemzidi hata umaarufu umaarufu mwenye wimbo mwenyewe , hasa huku kwetu tanzania. So nikaona si vibaya sana kama tukimchimba na kumfahamu zaidi J’odie.

Jodie-55

Mimi binafsi wakati wimbo huu unafanya vizuri sana kwa hapa Tanzania nilijaribu kutafuta kazi za J’odie mtandaoni japo iliniwia vigumu kwa muda, sababu kila nilipokuwa niki-google nilikutana na muigizaji wa marekani ambaye pia anafahamika kama Jodie Foster ambaye jina lake kamili ni Alicia Christian Foster.

DF-05136
Jodie Foster

Hivyo nikawa nakwama kumpata na kilichokuwa kinanikwamisha nilikuja kugundua baadaye sana nilikuwa nikikosea kuandika jina lake ambalo linaandikwa J’ODIE huku yule wa Marekani anaandikwa JODIE. Kwahiyo mimi ni mmoja kati ya watu ambao walipata shida pia kuweza kumfahamu na kufahamu undani wake sababu kila nilipojaribu kutafuta undani nikawa nakutana na kikwazo hicho, kwahiyo nikawa nataka kujua ana nini ana wimbo gani anatokea wapi na vitu kama hivyo.

HISTORIA YA J’ODIE:

Historia ya J’odie inaonesha kwamba kwanza jina lake la J’odie linatokana na jina lake halisi ambalo ni JOY ODIETE, kwahiyo kuna uwezekano hii J’odie ameunganisha ‘J’ ambayo imetokana na jina la kwanza la Joy halafu ndio sababu basi kuna kile kimkato pale juu halafu ‘Odie’ inatokana na jina lake la pili ambayo ukiiunganisha unapata J’odie.
Amezaliwa June 22, ni mwimbaji na mwandishi wa nyimbo kutoka Nigeria.

Safari yake ya muziki imeanzia mbali kidogo, ameshawahi kushiriki na kufika fainali katika mashindano mbalimbali ya kusaka vipaji AFRIKA MAGHARIBI , IKIWEMO Nigeria Idols na alifanikiwa kufika fainali lakini hakubahatika kushinda, na pia ameanzia kanisani, unajua kila msanii anakuwaga na ana mwanzo wake J’odie alianzia kanisani lakini hii utakuja kuipata kwa urefu zaidi baadae kidogo.

ELIMU YAKE:

Upande wa elimu yake mbali na muziki J’odie ni msomi mwenye Bachelor of Science (BSc) in Mass Communication ambayo aliipatia katika chuo kikuu cha Lagos Nigeria, pia ana cheti cha Entrepreneurial Management (CEM) alichopatia The Pan African University pamoja na Basic Leadership Certificate.

Jodie-10

SINGLE ZAKE:
Single za mwanzo kabisa za J’odie ni pamoja na single iliyofahamika kwa jina la ‘Fighter’ pamoja na ‘Kuchi Kuchi’ ambayo ndio ilifungua milango ya mafanikio kwa J’odie, zote zilitoka mwaka 2010, huku Kuchi kuchi ilikuja kupata umaarufu mkubwa zaidi barani Afrika na wimbo huo kwa Tanzania umeanza kuhit mwanzoni mwanzoni hivi mwa mwaka 2012. Single zake nyingine ni pamoja na ‘Under The Mango Tree’, Sugar Coconut’ , na ‘African Woman’ na zingine.

TUZO:

Licha ya kuwa jina lake bado halijakuwa na ukubwa wa kuweza kuwekwa katika ile orodha ya wasanii wakubwa wa bara la Afrika, lakini Kuchi Kuchi ni ni wimbo uliomletea kila aina ya furaha na mafanikio, mbali ya kumpa shows ilimuwezesha pia kuwa nominated katika tuzo mbalimbali.

Jodie-7 akiwa na tuzo

Alikuwa nominated katika tuzo za Nigerian Entertainment Awards (NEA), New York – September 2011 katika kipengele cha the Indigenous Artiste of the year.

Video ya Kuchi Kuchi iliyotoka mwezi February 2011, nayo ilimuwezesha kuwa nominated tena safari hii ilikuwa ni mara nne katika tuzo za Nigerian Music Video Awards, 2011 katika vipengele vya Best Indigenous Concept; Best Use Of Costumes; Best Highlife Video na Video Of The Year, na alifanikiwa kuondoka na tuzo mbili kati ya hizo ambazo ni video bora ya mwaka na best highlife video.

SABABU ZINAZOTHIBITISHA KUWA WIMBO WAKE WA KUCHI KUCHI NI MAARUFU KUMZIDI J’ODIE:

Kama nilivyosema pale mwanzoni, jina la J’odie bado halijawa kwenye vichwa vya watu wengi zaidi ya nyimbo zake hasa hasa kuchi kuchi. Moja ya sababu zinazonishawishi kuamini hivyo hata ukiangalia ukurasa wake wa facebook una likes 4784 tu mpaka sasa, na sio kwamba Una likes chache sababu ni mpya, hapana Umefunguliwa toka mwaka 2010 hivyo inathibitisha kwamba bado hajawa na umaarufu sana ukIlinganisha na umaarufu wa wimbo wake. Upande wa Twitter ana followers 3600, upande wa Instagram kwabahati mbaya sijafanikiwa kumpata kwa jina la J’odie otherwise labda kama anatumia jina tofauti na hilo.

Jodie-8 kuchi video

Kithibitisho kingine cha kwanini naamini umaarufu wa wimbo wake ni mkubwa zaidi ya yeye mwenyewe, video yake ya kuchi kuchi ambayo iliwekwa youtube miaka mitatu iliyopita katika channel ya Joy Odiete, imetazamwa mara 1,217,308 ukilinganisha na video za nyimbo zake zilizofata mfano ‘African woman’ imetazamwa mara 10,911 toka imewekwa miezi 11 iliyopita, huku ‘Sugar Coconut’ ndio kidogo imejikongoja kwa kutazamwa mara 28,025 na ina miezi mitano toka imewekwa youtube.

Nimezitaja hizi figure za youtube nikimaanisha wimbo ambao ndio maarufu sana ndio huo wa Kuchi Kuchi ambao umetazamwa zaidi ya mara milioni moja na zaidi wakati hizi zingine zote hazijafikisha hata elfu 30 kwa maana kwamba huo ndio wimbo ambao umekuwa ni maarufu kuliko yeye.

Jodie-4
J’odie alipozungumza na waandishi wakati akitambulisha album yake

MAANA YA ‘KUCHI KUCHI’:

J’odie ameshafanya mahojiano mara kwa mara na vyombo mbalimbali vya habari, na katika moja ya mkutano na waandishi wa habari ambao alifanya kipindi anataka kutoa album yake ya kwanza alikutana na swali la maana ya Kuchi Kuchi. Yawezekana kuna watu wengi pia hawafahamu maana ya Kuchi Kuchi:

“Watu wengi wamekuwa wakiniuliza kuchi kuchi ni nini, kuchi kuchi ni sauti, ni sauti iliyochangamka,iliyotengenezwa na mtu anayecheza na mtoto..kwahiyo ni wimbo unaoelezea mapenzi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto…kwahiyo watu wengine wamekuwa wakiutumia katika harusi zao na ni sawa, mapenzi yanaweza kuelezewa kwa njia nyingi sio lazima yawe mapenzi ya mama na mtoto”. Alisema J’odie alipokuwa katika mkutano na vyombo vya habari wakati akitambulisha ujio wa album yake ya ‘African Woman’ mwezi may mwaka juzi 2012.

Jodie-3 akiperform mbele ya waandishi

Katika mkutano huo J’odie alipitia wimbo mmoja baada ya mwingine huku akiuelezea kwa ufupi kisha kuuimba live huku akisindikizwa na kinanda (Utasikia katika audio mwisho wa story hii).

Jodie-5 album cover

ALBUM YA J’ODIE ‘AFRICAN WOMAN’:

Album hiyo yenye jumla ya nyimbo kumi ambazo ni pamoja na zile single zake zilizoishatoka iliachiwa mwezi September mwaka huo huo 2012 na pia inapatikana iTunes.

Back-Cover-JPEG
Naamini kwamba ukipata bahati ya kuisikiliza album yake, mapenzi yako juu ya J’odie yanaweza kuongezeka mara dufu. Hebu nikuskilizishe baadhi ya nyimbo ambazo zipo katika album yake ya African Woman, na ofcoz ambazo ziliwahi kutoka kama singles.

Wimbo huu unaitwa ‘Sugar Coconut’ ni wimbo ambao ulitoka, ukitazama video za J’odie utagundua kitu flani , hebu mtazame vizuri usoni, anaimba kwa hisia sna mpaka mara nyingine anafunga macho wakati anaimba sababu anachokitoa kinatoka ndani yake, yaani akauwa na feeling kitu ambacho wasanii wengi huwa wanakikosa especially wanapokuwa wanawasilisha messages za mapenzi tena yale mapenzi ya hisia. Msanii wa bongo ambaye hua anatoa feelings kama hizo kwenye nyimbo zake Ben Pol hua anaimba kwa hsia sana.

Wimbo huu unaitwa ‘Under The Mango Tree’, katika wimbo huu anamwambia mpenzi wake wakutane chini ya mwembe.

SABABU ZA KUCHELEWA KUTOA ALBUM:

Licha ya single ya kuchi kuchi kufanya vizuri sana Nigeria na kwingine barani Afrika toka ilipoachiwa mwishoni mwa 2010, lakini J’odie hakukurupuka kutoa album yake, zipo sababu za kuchelewa kutoka kwa album hiyo mpaka mwishoni mwa 2012.

“Mwaka 2007 Idols za Afrika Magharibi zilifanyika na baada ya hapo nilienda chuoni kwaajili ya masomo yangu. Naamini muda huu (2012) ndio muda muafaka wa album yangu ya kwanza kutoka, na sijutii mwaka wowote uliopita badala yake miaka hiyo imenijenga kufika hapa nilipo sasa.

Nimekuwa nikirekodi nyimbo kipindi chote hicho kutokana na sababu mbalimbali sikuridhishwa nazo. Marafiki zangu wengi walinihimiza kuitoa album lakini moyo wangu haukunihimiza kuitoa mpaka niliopokuja kukutana na meneja wangu, na aliniambia kile kilichokuwa kwenye akili yangu kuwa nyimbo hizi hazifai kwa album na kwa mara ya kwanza nilifurahi kuambiwa kitu ambacho kilikuwa kwenye akili yangu, kwasababu nilikua nitoe nyimbo ambazo sikuwa nafurahishwa kuzitoa…nilijua kuna siku muda wangu utafika na nafurahi kuwa muda huo ni sasa”. Alisema J’odie wakati akiitambulisha album yake kwa waandishi wa habari (Utaisikia sauti yake kwenye audio mwisho wa story hii).

Jodie-6
J’odie

MWISHONI MWA MWAKA JANA J’ODIE ALIFANYIWA EXCLUSIVE INTERVIEW NA MTANDAO WA FUNTAQA, AMBAPO ALIFUNGUKA MAMBO MBALIMBALI IKIWEMO HISTORIA YAKE, MAFANIKIO, NA MAMBO AMBAYO HUENDA YAKAFANYA UKAMFAHAMU ZAIDI:

-Je unaweza kushare na sisi baadhi ya story za mafanikio yaliyotokana na hit single yako ‘Kuchi Kuchi?

“Hadithi nyingi zenye kutia msukumo zimekuwa zikitolewa na mashabiki marafiki na familia kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii na vyombo vya habari au wengine wamekuwa wakiniambia wenyewe kuhusu jinsi wimbo ulivyosuluhisha mahusiano yaliyokuwa yameharibika, jinsi ulivyotumika kama tumbuizo kwa watoto, kuwanyamazisha au kusaidia kuwalaza watoto kwa kuwaimbia, Jinsi wazee vijijini walivyokuwa wakiuimba kwa furaha, jinsi ulivyokuwa ukileta furaha kila wakati usikikapo. Hadithi ni nyingi hazihesabiki za ni nzuri. mimi najiona kama mlinzi wa zawadi hii, na wakati mwingine huwa nashangaa na KUJIULIZA ‘Kwa nini mimi’?”. Alisema J’odie wakati akielezea mafanikio yaliyoletwa na wimbo huo.

-Baba yako ni Askofu, na wewe ni kiongozi wa kwaya katika kanisa lenu, uliwezaje kuishawishi familia yako kuwa unajihusishana aina ya muziki tofauti na gospel?

“Aina ya muziki ninaoufanya ni wa kupendwa na na kila mtu. Kuchi kuchi, kwa mfano, ni wimbo unaoonesha upendo wa mama na mtoto. Naamini kuwa watu wa dini nyingine, au hata wale ambao hawana dini , wana watoto pia.
Kwa kusema hayo, mimi ninazifuata kanuni za mungu….Wakristo wanaoana, wana watoto, wanakutana na matatizo ya kiuchumi kama wanayokutana nayo wengine. Albamu yangu inaelezea baadhi ya mambo ambayo binadamu hukutana nayo”.

-Umaarufu wako umeathiri kiasi gani utendaji wako wa shughuli za kanisani?

“Kama sina kazi ya kufanya nje ya mji, kwa kawaida huwa naenda kanisani na kushiriki katika idara yangu ambayo ni ya muziki”.

-Nini kinachokuhamasisha wewe kuandika nyimbo au kuna yeyote anayekuandikia?

“Maisha yananihamasiha.- kuna mengi ya kuandika. Kwa mfano, watu wamekuwa wakiandika nyimbo za mapenzi kwa miaka: watu bado wanaendelea kuandika sasa:
Watu bado wataendelea kuandika kuhusu mapenzi. Hiyo ni moja tu kati ya dhana zisizohesabika zinazoweza kutumika kuandika nyimbo. Inspiration zimejaa, fungueni tu macho yenu, masikio na mioyo. Nyimbo zote ambazo nimeshatoa zimeandikwa na mimi”.

-Nini ambacho hupendela kufanya usipokuwa na show au na kazi yoyote ya muziki?

“napenda sana kutengeneza shanga, hata hivyo kipindi hiki nimekuwa nikipendelea zaidi kusoma. Dr. Seuss alisema ‘Unavyojua vitu zaidi, ndivyo utakavyofika sehemu nyingi”.

-Kuna wimbo wowote katika album yako ambao ungependa kuubadilisha?

“Hapana, sio kwasababu nazipenda zote kwa kiwango sawa, lakini kwasababu nyimbo zingine nilizodhani sio nzuri sana, ndio zinazopendwa na watu wengine.”

Huyo ndiye J’odie au Joy Odiete msanii kutoka Nigeria ambaye kwasasa ni maarufu sana kwa hapa Tanzania si kwa jina lakini kwa wimbo wake wa Kuchi Kuchi.

Sikiliza makala hii hapo chini katika mfumo wa sauti ili uweze kumsikia J’odie mwenyewe akiongea pamoja na nyimbo zake.

SOURCES: Youtube, www.facebook.com/Jodie, funtaqa.wordpress.com

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents