Videos

Huzuni baada ya mfanyabiashara kutapeliwa ng’ombe 40 Dar, asimulia (Audio)

Mjini kuna watu wa kila aina na matapeli ni miongoni mwao. Mfanyabiashara wa ng’ombe kutoka Tabora amejikuta akiingizwa mjini na wajanja waliomtapeli ng’ombe arobaini wenye thamani ya shilingi milioni 40.

Akisimulia mkasa wake kwenye Ripoti ya kipindi cha Ubaoni cha EFM, Maganga Malulu ambaye ni mfugaji wa ng’ombe, alipigiwa simu na mtu wa Dar aliyemweleza kuwa angetaka kununua ng’ombe 40 tena kwa shilingi milioni 1 kila mmoja, bei ambayo ilikuwa juu ya bei aliyokuwa akizoea kuuza.

Anadai kutokana na kupewa ofa hiyo ya aina yake, alilazimika kuchukua ng’ombe 10 kutoka kwa shemeji yake na mkwe wake akampa ng’ombe 15 na kuongeza wake 15.

Maganga anasema jamaa huyo aliyempigia simu alijitambulisha kwa jina la John na alionesha kumwelewa vyema hivyo kumtoa ofa.

Maganga alianza safari ya kuwaleta ng’ombe hao na kumpa dereva pesa nusu na kuwasili ubungo, Dar na mwenyeji wake akamuambia aende Buguruni. Anasema walifikia kwenye kituo cha mafuta na watu watatu kuwafuata ili wamalize biashara yao.

Akisimulia huku akilia kwa uchungu, Maganga anasema watu hao walimchangamkia mno na huku aliyempigia simu akiendelea kumpa story nyingi na kumuuliza habari za kijijini kuonesha anamfahamu vyema ikiwemo kumuuliza kuhusu kama ana mpango wa kuongeza mtoto.

Anasema baada ya dana dana za hapa na pale na upigwaji simu wa dakika kadhaa kupanga mipango ya kumliza, walikubaliana waelekee machinjioni Pugu huku yeye akiambiwa apande kwenye gari ndogo. Anasema kidogo apate wasiwasi lakini kuna kitu kilimpa ujasiri na kutulia.

Anadai walifika sehemu jamaa wakamuita mtu aliyekuwa anauza juice ili wanunue na zikaletwa nne. “Lakini yule jamaa alipoleta juice ni kama alizichagua, mimi nikapewa juice ya rangi rangi nyeusi wengine wakapewa juice kama ya Mirinda,” anasimulia Maganga.

“Mimi kweli huku tunaendelea kupiga story tunacheka kwenye gari mimi nikawa nakunywa ile juice, mimi nakumbuka niliimaliza. Tulipomaliza pale jamaa akawa anacheka, ananikumbusha nyumbani huko, ananikumbusha mashamba yangu na hivyo akaniambia anataka shamba la viazi nikamuambia nitakusaidia mimi kulima nitakuwa kama kibarua wako huku tunaenda akinitania eti ‘ongeza mtoto wa pili mmoja hatoshi,” anakumbushia Maganga kwa uchungu.

“Sasa mimi nafurahi, mimi sijui chochote anavyonitania basi mimi najua nitapata tu haki yangu bila kujua kitu chochote lakini leo ndio naamini matapeli wakiamua kufanya yao… lakini baada ya hapo mimi nikawa nimepoteza fahamu, yaani sikujua hata nilipokuwepo, sijui tukio la mwisho lilikuwa wapi.”

“Mimi nimejikuta nipo pembeni ya reli watu wamenizunguka kwahiyo sikujua kama mimi nilitupwa kwenye reli, watu walionizunguka pale sijui ndio hao walioniokoa mimi sijajua kabisa mimi nikawa nashangaa tu,” amesimulia.

Anasema baada ya hapo alibaki akitangatanga huku wasamaria wema wakimchukua na akawasimulia yaliyo msimu. Hata hivyo Maganga amesema hajakubali kuingizwa mjini kirahisi hivyo huku akiahidi kulipiza kisasi.

“Mimi nasema sikubali, yaani kama wao ni wajanja wa mjini na mimi nitawaonesha na mimi ni mjanja wa kijijini nitatumia hata miti shamba lakini mimi najua mali yangu itarudi.”

Anadai kuwa hata hela aliyokuwa nayo mfukoni, shilingi laki 3 na simu vilichukuliwa. Maganga bado yupo Dar kwa msamaria mwema kwa takriban wiki ya pili sasa tangu alizwe na mbaya zaidi nyumbani hawajui chochote.

“Kule nyumbani wananisubiria mimi nirudi niwape hela kwasababu ng’ombe wote wale sio wote wangu. Kwahiyo mimi hapa nipo sijui nafanya nini na nyumbani hawajui. Hicho kitu ndio kinaniumiza kichwa muda mwingi hata kurudi nyumbani nashindwa,” Maganga anasema huku akilia kwa uchungu.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents