Afya

Taarifa kuhusu ugonjwa wa pumu

Leo ni siku ya kuadhimisha ugonjwa wa pumu duniani. Tangu mwaka 2012, kauli mbiu ya siku ya pumu duniani imekua “Unaweza kudhibiti Pumu yako”.Ugonjwa wa pumu ni ugonjwa ambao huathiri sehemu ya kupitisha hewa kwenda kwenye mapafu ya binadamu zinazojulikana kitaalamu kama bronchioles.

Mtu mwenye pumu huwa na mcharuko mwili sugu (chronic Inflammation) kwenye mirija yake ya kupitishia hewa (bronchioles tubes) hali ambayo husababisha kuvimba kwa kuta za mirija hii, kujaa kwa ute mzito (mucus) na kupungua kwa njia ya kupitishia hewa, hali ambayo humfanya muathirika kushindwa kuvuta na kutoa hewa.

Pumu inaweza kugawanywa katika makundi mawili;

⦁ Pumu ya ghafla (Acute asthma): Wagonjwa wanaopatwa na kundi hili la pumu huwa na hali ya kawaida katika njia zao za hewa isiyobadilika kati ya shambulizi moja na jingine.
⦁ Pumu sugu (Chronic Asthma): Kundi hili la pumu huwa na tabia ya kuwa na njia nyembamba za kupitisha hewa na kadiri jinsi mgonjwa anavyoendelea kupata matukio zaidi ya pumu, njia za hewa huzidi kuwa nyembamba zaidi.

Dalili za ugonjwa wa pumu ni pamoja na

a. Kuishiwa na pumzi na kupumua kwa shida (shortness of breath)
b. Kutoa sauti kama mtu anayepiga miluzi wakati wa kupumua (wheezing)
c. Kukohoa sana (chronic cough) hasa nyakati za usiku au asubuhi. Aidha kikohozi huambatana na kutoa makohozi mazito, yasiyo na rangi au yenye rangi ya njano.
d. Kubana kwa kifua.
e. Kwa mtu aliyepata shambulizi kubwa la pumu (severe asthmatic attack) anaweza kushindwa kuzungumza na pia kuwa na hali kama ya kuchanganyikiwa.

Tafiti kadhaa zimeonesha kuwa takribani theluthi moja ya wajawazito wenye pumu hupata nafuu kipindi cha ujauzito, theluthi nyingine hupata matatizo kipindi hiki na theluthi iliyobakia huwa na hali ya kawaida kama kabla ya ujauzito.

Kwa kawaida dalili za pumu hujirudia kama awali miezi mitatu baada ya kujifungua. Dalili za pumu kwa mjamzito zinaweza kuwa mbaya zaidi kuanzia wiki ya 24-36 (mwezi wa sita mpaka wa nane). Ni mara chache sana mjamzito

anapata shambulizi la pumu wakati wa kujifungua. Inakisiwa kuwa, ni asilimia 10 tu ya wajawazito wenye pumu wanaopata shambulizi la pumu wakati wa kujifungua. Baadhi ya dawa zinazotumika wakati wa ujauzito na baada ya

kujifungua huongeza madhara ya pumu, hivyo ni vizuri kumueleza daktari kwamba una pumu kabla ya kupewa dawa. Aidha na si vyema kunywa dawa kwa mazoea. Wanawake wenye pumu isiyoweza kuthibitiwa kipindi cha ujauzito

hupata madhara ya kuzaa mtoto njiti (premature baby), kuzaa mtoto mwenye uzito mdogo, kifafa cha mimba, shinikizo la damu (Hypertension), na iwapo atapata shambulizi hatari wakati wa ujauzito mtoto anaweza kufa kwa kukosa hewa ya oksijeni.

MATIBABU

Kwa ujumla matibabu ya pumu hujumuisha kuepuka visababishi vya ugonjwa huu na matumizi ya madawa kwa walio na hali mbaya. Aidha, kwa wanaopata ugonjwa huu kwa sababu ya msongo wa mawazo hupewa ushauri nasaha kwa ajili ya
kusaidia kutatua matatizo yanayowakabili. Vilevile inashauriwa kwa wenye tatizo hili, kuwa na dawa karibu muda wote kwa ajili ya matumizi pindi shambulizi litakapotokea.

Pia inashauriwa sana kuepuka mazingira na hali za baridi ambazohuweza kuchochea kutokea kwa shambulio la ugonjwa huu. Matibabu ya kutumia dawa hujumuisha matumizi ya dawa za kusaidia kupunguza na kuondoa makohozi (expectorants), dawa zinazosaidia kutanua mirija ya hewa (bronchodilators), dawa za kuondoa mcharuko mwili kama vile cortisone ya drip (hasa wakati wa dharura) au nebulizer, na dawa za kuzuiamzio (antihistamine drugs).

Hata hivyo, kuna matibabu ya ziada kulingana na hali ya mgonjwa pamoja na kundi na aina ya pumu inayomuathiri mgonjwa. Kwa wagonjwa wenye pumu ya ghafla na wenye hali mbaya (acute asthma) matibabu hujumuisha matumizi ya dawa za kutanua mirija ya hewa (bronchodilators) pamoja na kuongezewa hewa yaoksijeni, dawa za kutuliza mcharuko mwili (steroids) pamoja na dawa za kutuliza kukakamaa kwa misuli ya mwili (intravenous muscle relaxants).

Aidha kwa vile mara nyingi shambulizi hili laweza kuwa la hatari sana, mgonjwa hulazwa hospitali na huongezewa hewa ya oksijeni, na kwa wagonjwa wasioweza kupumua kabisa, husaidiwa kufanya hivyo kwa kutumia mashine maalum iitwayo (mechanical ventilator). Kwa wagonjwa wenye pumu sugu, jambo la muhimu nikuepuka visababishi vya pumu na kuendelea na matumizi ya dawa zinazosaidia katika kutanua mirija ya hewa.

Kwa wagonjwa wanaopata mashambulzi ya mara kwa mara wanaweza kushauriwa na daktari kutumia dawa kadhaa zikiwemo zile zinazopunguza mcharuko mwili (mast cell inhibitors, inhaled steroids au oral steroids), pamoja na dawa za kutuliza kukakamaa kwa misuli ya mwili (muscle relaxants). Aidha ni vema pia kutibiwa na kuthibiti kutokea kwa magonjwa yote yahusuyo mfumo wa hewa. Matumizi ya chanjo ya magonjwa kama influenza na pneumococcal pneumonia nayo husaidia sana katika uthibiti wa kutokea kwa pumu. Ni vema pia kuepuka matumizi ya dawa za jamii ya beta-blockers kwa wagonjwa wenye shinikizo la damu na ambao pia wana pumu.

Na Laila Sued

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents