Bongo5 Makala

Wasanii Tanzania wana la kuwaiga wakenya

Katika juhudi za kuhakikisha kuwa kila jasho la msanii linapata haki yake, juzi wasanii wa Kenya walijumuika pamoja na wawakilishi wa chama cha haki miliki cha Kenya MCSK, kujadiliana masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na kurekebisha baadhi ya sheria zinazomkandamiza msanii.
Ni uamuzi uliotokana na ushirikiano wa wasanii wote wa nchini Kenya na kuamua kuingilia kati ili kuleta mabadiliko katika muziki wao.
Katika mapinduzi hayo ya hali ya juu karibu wasanii 500 wakubwa na wa kati walijiunga kwenye kampeni hiyo ya kuwachagua wasanii wanne ambao watawawakilisha wenzao kwenye foundation ya MCSK Foundation itakayokuwa ikijihusisha na masuala ya kijamii na kitamaduni kwa wanachama wake.
Katika mabadiliko hayo wasanii watakuwa na wawakilishi wa moja kwa moja kwenye bodi ya wakurugenzi na uongozi wa chama hicho.
Kampeni hiyo pia ina lengo la kuwaamsha wasanii ambao ni wanachama lakini wasiohusika na shughuli za hapa na pale za MCSK ambao wengi hungojea kulipwa mirahaba yao (royalties) na kulalamika pale wanapolipwa kidogo.
Ufafanuzi hapa ni kwamba MCSK husimamia pesa zote zinazopatikana kutokana na utumiwaji wa kibiashara wa kazi za msanii hususan zile zinazotolewa na vituo vya radio ama TV kwa kupiga kazi ya msanii (kitu ambacho Tanzania bado ni ndoto).
Wasanii hao wamefanya kampeni kubwa mwaka huu kwa kutengeneza matangazo kuwaamsha wasanii waliolala na ndo maana mkutano wa July 5 ulikuwa umejaa wasanii wote wa Kenya unaowahahamu.
Muitikio wa wasanii wakubwa kama Nameless, Wyre, Wahu, Habida, Jaguar, Nonini, Mr Lenny, Ousman, Didge, Frasha, Bon’Eye, Gabu, MOG, Lady B, Mimmo, na wengine wengi umeonesha kuwa sasa kazi ipo.
Wasanii sita waliwania nafasi mbalimbali kwenye foundation hiyo ambapo wale waliowania kuwepo kwenye kamati ya bajeti walikuwa ni Francis Amisi (Frasha wa P-Unit), muimbaji Jane Nyambura na Njamba (James Wahome).

Matokeo ya uchaguzi yakawapitisha Mongolo na Wa Jane Mwalimu kuingia kwenye MCSK Foundation huku Frasha na Jane Nyambura wakiingia kwenye kamati ya bajeti.
Hiyo ikawa ni hatua kubwa mno iliyofikiwa na wasanii ili kutatua matatizo sugu waliyonayo na MCSK.
Hiyo juzi wasanii wengi walijitokeza kwenye mkutano mwingine uliofanyika Bomas of Kenya kupiga kura juu ya sera zinazowaathiri wasanii na muziki wa nchini humo kwa ujumla.
Mapinduzi hayo ya wasanii wa Kenya katika kuhakikisha chombo kinachosimamia haki zao kinawajibika ipasavyo, yanahitajika kuigwa na wasanii wa Tanzania ambao nao kila kukicha wamekuwa wakiilaumu COSOTA yenye dhamana sawa na MCSK ya Kenya.
Bila wao kujiunga na kufanya mikutano ya pamoja na kuweka sifa pembeni kujadili mambo wanayotaka yawepo COSOTA, haki zao za msingi zitaendelea kuwanufaisha wachache.
Jambo la msingi la kuanza nalo sasa, ni kuhakikisha kuwa COSOTA inaharakisha mchakato wa kuzifanya radio na TV zianze kuwalipa wasanii kwa upigaji wa nyimbo zao. Hilo wakenya walilifanikisha mapema na sasa wanachohangaikia ni kuhakikisha kuwa pesa zinazotolewa ziendane na wanachostahili.
Wanamuziki wa Tanzania wajiunge wenyewe kushinikiza kuwa na wawakilishi wenye sauti kwenye COSOTA ili kusimamia masuala muhimu yanayohusu haki zao. Na wale wanaosimamia chama hiki cha haki miliki nchini wasijifungie tu maofisini ama kufanya semina zisizo na kichwa wala miguu, bali wajifunze namna vyama vingine vinavyofanya kazi zake.
Bila msukumo kutoka kwa wasanii wenyewe utakaochangiwa na umoja wao, muziki wa Tanzania utaendelea kutegemea hela za show peke yake huku zipo njia zingine nyingi halali za kuwaingizia hela.
Hata kama TRA ikiingilia katika usimamizi wa kazi zao, hakuna litakalofanikiwa bila kuongeza uwajibikaji wa COSOTA kwa kuwashikirikisha wasanii nchini.Mtoto hatembei kabla ya kutambaa! Hatua lazima zifuatwe.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents