Bongo5 Makala

Makala: Ukimya wa Darassa si wakuchukuliwa poa (+Audio)

Ni zaidi ya miezi 11 sasa mashabiki wa Darassa hawajui utamu wa ngoma mpya kutoka kwa rapper huyo, ukimya wake umekuwa mkubwa zaidi.

Mara ya mwisho Darassa kutoa ngoma ilikuwa May 05, 2017 ambapo alitoa wimbo unaokwenda kwa jina la Hasara Roho. Baada ya hapo aliweza kufanya show mbali mbali za ndani na nje ya nchini lakini kuanzia August mwaka jana amekuwa kimya kwani haonekani kwenye media na mitandao ya kijamii.

Mashabiki wamekuwa wakiuliza wapi alipo Darassa na nini anafanya kwa sasa, pia wasanii wenzake nao wanataka kujua ukimya wa Darassa unasababishwa na nini. Hapo juzi msanii Belle 9 kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Twitter alihoji wapi alipo rapper huyo. Tumjadili Darasa kidogo.

Kivuli cha Muziki

Wakati Darassa anatoa ngoma yake ya mwisho Hasara Roho mashabiki walikuwa wakiilinganisha na ngoma ‘Muziki’ ambayo ilifanya vizuri kuliko ngoma zake alizozitoa hapo awali.

Licha ya Darassa kuikingia kifua Hasara Roho kwa kueleza kila ngoma ina nafasi yake ni wazi ngoma hiyo imezidiwa na Muziki kimafanikio. Tukitazama kwa upande mmoja wa YouTube wimbo Hasara Roho umezidiwa na Muziki.

Ngoma Hasara Roho iliyopandishwa YouTube May 05, 2017 ina views Milioni 3 wakati ngoma Muziki iliyopandishwa November 23, 2016 ina views Milioni 11.5, ukiangalia tofauti ya muda utangundua Hasara Roho inahitaji miaka zaidi mitatu kuifikia muziki endapo itafikisha idadi hiyo ya views kwa kipindi cha kila mwaka mmoja.

Hapo kwa akili ya kawaida utaelewa kuwa katika wimbo wa Muziki Darassa amejipa deni kubwa katika maisha yake ya kimuziki, kila ngoma anayotoa mashabiki wanataka kuilinganisha na Muziki na kwa vile anachokitoa hakifiki hapo pengine inaweza kuwa sababu ya ukimya wake ili kujipanga zaidi ila usichukulie poa.

Ukimya Mtandaoni

Darassa amekuwa kimya si kwenye muziki bali hata kwenye mitandao ya kijamii haonekani, si mtu tena wa ku-like, ku-share wala ku-comment.

Mara ya ya mwisho kuposti katika ukurasa wake wa Instagram ni August 12, 2017, mara ya mwisho katika mtandao wa twitter ni March 17, 2017, katika mtandao wa Facebook ni December 6, 207.

https://www.instagram.com/p/BXtBV2ejjyo/?taken-by=darassacmg

Darasa amekuwa kimya mtandaoni licha ya kuwa wasanii wengi kwa sasa anatumia mitandao ya kijamii zaidi kama sehemu ya kujitangaza na ku-brand bidhaa wanayouza ambayo ni muziki.

Hivyo ukimya huo katika mitandao nao unaweka mashabiki wake njia panda, kama amekaa kimya kimuziki na ameachia kufanya interview na vyombo vya habari, mashabiki wake wana haki ya kupata taarifa kupitia mitandao hiyo.

Alikiba kwa sasa yupo kimya tangu alipotoa ngoma yake ‘Seduce Me’ August 25, 207, amekuwa hafanyi interview na media lakini yupo active kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii ili mashabiki wake kujua kipi kinaendelea kwa upande wake.

Kwa Darassa ni tofauti na hilo kwani amekuwa kimya pande zote mbili. Kukaa kimya katika mitandao kunafanya kurasa zake za mitandao hiyo kutokua (kuongeza idadi ya watu) kwani hakuna anayetembea.

Tetesi Mbaya

Kutokana na ukimya wa Darassa katika muziki na kwenye mitandao miezi kadhaa iliyopita kulizuka taaarifa zilizodai kuwa msanii huyo ametumbukia katika matumizi ya dawa za kulevya na ndio chanzo hasa cha ukimya wake.

Siku kadhaa baada ya taarifa hizo Darassa aliibuka na kukanusha taarifa hizo. Kupitia Clouds FM Darassa alisema hakuna ukweli wowote na kueleza kutokana amefanya vitu vikubwa watu wanataka kuona akifanya makeke katika mitandao, akiwa na wanawake, mitoko ya mara kwa mara club lakini yeye si mtu wa maisha hayo.

“Sasa kwa sababu sifanyi hivyo na nilikuwa nimefanya kazi kubwa sana basi nitakuwa nimechanganyikiwa kama sio nimechanganyikiwa nitakuwa navuta unga lakini sio kitu ninachofanya,” alisema Darassa.

Baada ya interview hiyo iliyoruka January 28, 2018 sijamsikia tena katika interview na chombo chochote cha habari na ndio ukawa mwisho wa tetesi hizo ambazo si nzuri kuzisikia hasa kwa msanii aina Darassa ambaye amekomaa na muziki kwa kipindi kirefu hadi kufika alipo sasa ambapo anapata show nyingi kubwa na dili kadhaa za matangazo.

Watu wa Karibu

Kwa kuwa Darassa yupo kimya na kupatikana ni vigumu, watu wa karibu ambao amekuwa akifanya nao kazi wamekuwa akijihojiwa ili kueleza rapper huyu yupo wapi na anafanya nini. Miongoni mwao ni pamoja na Producer Abba na Director Hascana.

Hanscana ambaye ameongoza video kadhaa za Darassa kama Muziki, Too Much, Kama Utanipenda na nyinginezo alikiambia kipindi cha Chill na Sky kupitia Dizzim Online kuwa msanii huyo yupo poa na yeye mwenyewe ndio anajua kuhusu biashara yake ya muziki labda anajipanga ili kufanya vizuri zaidi.

“Naamini mtu mwenyewe ndio anajua kazi yake na mfumo wa biashara yake kuliko mtu yeyote yule. Mimi naamini vizuri Darassa anajua biashara yake na anajua muziki wake na kila kitu chake. Nadhani kila kitu anachokifanya kipo ndani ya mipango yake na anakiona zaidi hata ya sisi tunavyoona. Labda kuna kitu anakifanya muhimu, akija kuachia ‘Waooo’ ndio maana,” ameongeza.

Mwanzo mwa March mwaka huu, Producer Abba aliiambia E-Newz ya EATV kuwa taarifa za Darassa kutumia dawa za kulevya hazina ukweli wowote na anawashangaa wanaoeneza taarifa hizo kwa kueleza kuwa iwapo Darassa haonekani mitandaoni, katika muziki na mtaani kaonekana vipi akitumia dawa za kulezwa?.

Mwisho; Twende mbele twende nyuma, baada ya kufafanua mambo kadhaa kuhusu ukimya wa Darassa itoshe kusema kuwa ukimya wa Darassa katika hayo niliyoeleza hayapaswi kuchukuliwa poa hata kidogo. Asante.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents