Diamond Platnumz

Diamond kufanya tamasha kubwa la watoto Leaders Club siku ya Chrismas

Diamond Platnumz, anatarajia kufanya tamasha kubwa na la kihistoria kwa watoto katika viwanja vya Leaders Club jijini Dar es Salaam siku ya Chrismas, December 25.

Diamond Platnumz akiwa na akina Mama wa Tushikamane Pamoja Foundation Mrs.Rose Mwapachu na Bikhis Sherally Mwana Chama
Diamond Platnumz akiwa na akina Mama wa Tushikamane Pamoja Foundation Mrs Rose Mwapachu na Bikhis Sherally Mwanachama

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa Habari Maelezo leo, Diamond amesema lengo kuu la tamasha hilo ni kuonyesha upendo wake kwa watoto lakini pia kuwashukuru kwa kumuunga mkono kwa kipindi chote cha uimbaji wake.

“Nimekuwa na bahati kwa mziki wangu kupendwa na watu wa rika zote, na kwa bahati nzuri watu wa marika mengine wamekuwa na bahati ya kuhudhuria matamasha yangu tofauti, ambayo watoto hawawezi kufika na ndio maana nikaona nao kuna haja niwafanyie kitu cha pekee yao,” alisema Diamond.

Diamond ambaye kwa wiki mbili zilizopita amekuwa akizunguka kwenye vituo tofauti vya watoto yatima kuwapa misaada mbalimbali, amesema tamasha hilo ambalo litakuwa ni mara ya kwanza kwa msanii mkubwa kufanya na watoto litaweka historia nchini.

Akielezea zaidi kuhusu tamasha hilo, Diamond amesema anataka kuwapa watoto nafasi ya kuifurahia siku hiyo, kwa kuwaandalia michezo mbalimbali, burudani maalum kutoka kwake, pamoja na nafasi ya kuzungumza nao mambo mambo mbalimbali pia.

Tamasha hilo ambalo litaanza saa nne kamili asubuhi hadi saa kumi na mbili jioni, litawapa fursa watoto kumsikia Diamond akiwaelezea kuhusu maisha na namna wanavyoweza kuamini ndoto zao na kuzifikia.

“Naamini mimi ni mfano kwa watoto wengi (role model), na hivyo pia nitatumia nafasi hiyo kuwapa moyo kukazana kuhakikisha wanazifikia ndoto zao,” alisisitiza Diamond.

Naye Mratibu wa Tamasha hilo, Babu Tale, alisema maandalizi ya tamasha mpaka sasa yanaenda vizuri, na hivyo watoto wajitokeze kwa wingi siku hiyo.

“Michezo mbalimbali ya watoto itakuwepo siku hiyo, lakini pia kutakuwa na zawadi mbalimbali zitatolewa kwa watoto watakaoonyesha vipaji vya kipekee,” alisema Tale.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents