Burudani

Video: Serikali yaufungia wimbo wa Snura ‘Chura’

Wizara ya Habari,Utamaduni, Sanaa na Michezo leo imetangaza kuufungia wimbo wa Snura, Chura kuchezwa kwenye redio na TV.

Picjha 2
Mkuu wa Kitengo cha mawasiliano wa Wizara ya Habari,Utamaduni, Sanaa na Michezo, Zawadi Msalla akiongea na waandishi wa habari

Taarifa hiyo imetolewa na wizara hiyo kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika kwenye ukumbi wake wa mikutano wizarani hapo jijini Dar. Uamuzi wa kumfungia umekuja kutokana msanii huyo kutojisajili kwenye Baraza la Sanaa la Taifa, BASATA.

Picha

“Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja taasisi zake ambazo zinashughulikia mambo ya sanaa, nikimaanisha BASATA, Baraza la Sanaa Taifa, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) pamoja na Bodi ya Filamu, tulipata nafasi ya kukaa pamoja na msanii wa nyimbo za kizazi kipya, Snura Mushi ili tuweze kuangalia kwa pamoja wimbo wake mpya alioutoa hivi karibuni unajulikana kwa jina la Chura, kuangalia maudhui ya huo wimbo na kumuuliza baadhi ya maswali mawili matatu kuhusu kazi hiyo,” alisema Mkuu wa Kitengo cha mawasiliano wa wizara hiyo, Zawadi Msalla.

“Baada ya majadiliano ya muda mrefu kidogo, serikali ilifikia katika maamuzi yafuatayo. Kwanza kabisa serikali imesitisha wimbo na video ya muziki wa Chura kupigwa katika vyombo vyote vya habari, runinga na redio pamoja na katika maeneo ya wazi. Hii tunamaanisha siyo video peke yake, ila na wimbo wake wa Chura.”

Aliongeza, “Lengo la kusitisha limetokana na miondoko iliyotumika katika utengenezaji wa video ile, kwanza ni ya udhalilishaji, pili haina maadili ya Mtanzania, tatu ni ukiukaji wa haki za binadamu kwa jinsi alivyotengeneza video yake. Lakini mbali hapo pia, serikali iligundua licha ya bibi Snura Mushi kuwa ni mwanamuziki wa muda mrefu lakini hana kibali chochote kile cha kumafanya kuwa ni msanii anayetambulika na serikali pamoja Baraza la Sanaa Taifa,” alisisitiza.

“Ili msanii yeyote aweze kutambulika anatakiwa kufuata taratibu fulani za kujisajili lakini Snura Mushi hajajisajiri popote na BASATA hawamtambui. Hivyo basi siyo tu tumezuia wimbo wake, Snura Mushi amesitishiwa kufanya maonyesho yoyote na popote pale, mpaka atakapoweza kutimiza masharti yote yanayotakiwa na BASATA ili kuweza kujisajili na kutambulika kama msanii au mwanamuziki halali anayetokea nchini Tanzania.”

Pia Snura alipewa siku mbili (jana na leo) kuhakikisha anaondoa video hiyo katika mitandao ya kijamii na asipofanya hivyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

“Katika kuzingatia hayo, tumeangalia na jinsi video yake ilivyosambaa katika mitandao ya kijamii na kuwekwa katika YouTube. Bi Snura Mushi ametakiwa kuhakikisha anatoa ile video aliyoiweka kwenye YouTube, na atafanya hivyo akishirikiana TCRA. Kwahiyo hilo ni agizo la mara moja ile video iondolewe na tulimpa siku mbili, jana na leo,” alieleza.

Alisema serikali imewataka Watanzania kuacha kusambaza video hiyo katika mitandao ya kijamii, kwani watakaobainika wanaendelea kufanya hivyo, TCRA itawachukulia hatua kali za kisheria kupitia sheria yake mpya ya makosa ya kwenye mitandao.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents