Bongo5 Makala

Wasanii walioiweka Tanzania kwenye ramani ya kimataifa mwaka 2015

Tupo kwenye robo ya tatu ya mwaka 2015, mengi yamekwishatokea na yanaendelea kutokea. Macho na masikio ya watanzania wengi kwa sasa yapo kwenye masuala ya kampeni za uchaguzi na pengine hiyo inafanya baadhi ya mambo kutomulikwa ipasavyo.

moja

Kiburudani pamoja na matatizo sugu yaliyopo kwenye kiwanda chetu, nchi yetu imefanikiwa kujipenyeza kwenye majukwaa mengi ya kimataifa. Pamoja na kuwepo vipaji mbalimbali vilivyotumia jitihada zao kujaribu na vingine kufanikiwa kuipeperusha, vipo vingi vilivyoonesha spidi kubwa zaidi. Ifuatayo ni orodha ya baadhi ya vipaji hivyo.

Diamond Platnumz

11373921_1172758619407770_1677646560_n

Hakuna ubishi kuwa 2015 huenda ukawa ni mwaka wenye mafanikio makubwa zaidi kikazi na katika maisha binafsi kwa Diamond. Huu ni mwaka ambao binti yake aliyegeuka kuwa kichanga maarufu zaidi barani Afrika alizaliwa.

Wengi tunafahamu ni kwa kiasi gani staa huyu alikuwa na hamu kubwa ya kuitwa baba na Tiffah amekuwa mtoto wa kwanza kuitimiza ndoto yake hiyo.

Kinachompa furaha zaidi ni kuzaa na mwanamke aliyemzungumzia kumpenda zaidi ya anavyoweza kuuelezea umma. Tofauti na mastaa wengine waliopata watoto, Diamond, mchumba wake Zari na mtoto wao Tiffah wameteka vichwa vya habari vya magazeti na blogs za Afrika kwa kipindi kirefu.

Tuseme tu kuwa ujio wa mwanae hata kipindi alikuwa bado hajazaliwa, umekuja na neema nyingi.

Huu ni mwaka ambao Diamond amefanya mambo makubwa zaidi yaliyotambulika katika bara zima. Ameshinda tuzo kibao kuanzia ile kubwa zaidi ya MTV MAMA na zingine za nchi kama Nigeria, Uganda na kwingineko huku zikiwepo zingine kibao zinazomngoja.

Mwaka huu amefanikiwa kufanya collabo na wasanii wakubwa duniani akiwemo Ne-Yo wa Marekani, P-Square, KCEE, Flavour na Iyanya wa Nigeria, Donald wa Afrika Kusini na wengine. Kuna tetesi zinasambaa pia ambazo binafsi sijaweza kuzithibitisha kuwa huenda akawa na collabo na Nicki Minaj.

Ngoma yake Nana imeshika chart kubwa za TV na redio barani kote na hadi Uingereza (BBA Radio 1 Extra). Ameshiriki kwenye kampeni za kimataifa zikiwemo One Campaign, The Global Goals na zingine.

Ni msanii wa Afrika Mashariki mwenye show nyingi za kimataifa na amekuwa akichukua pipa baada ya pipa kuvuka bahari kwenda kutumbuiza. Mpaka naandika makala hii show yake ya mwisho ilikuwa ni Jumamosi hii huko Mauritius.

Ndio msanii aliyeingiza fedha nyingi zaidi Tanzania kupitia show, mauzo ya ringback tones, mirahaba, mikataba ya matangazo na mishe zingine. Kwa makadirio ya haraka, mpaka mwaka huu unaisha, Diamond anaweza kuwa ameingiza takriban shilingi bilioni 3???!

Alikiba

11925805_1125419824152198_1767121933_n

Alikiba ataukumbuka sana mwaka 2015 kwa mambo mengi. Kubwa zaidi ni mvutano kati ya mashabiki wake na wale wa hasimu yake Diamond. Pamoja na mvutano huo kutengeneza nguvu fulani hasi kwenye kiwanda cha muziki wetu, tofauti hiyo imemtengenezea Alikiba fursa nyingi za kimaitaifa.

Kwa mara ya kwanza muimbaji huyo wa Chekecha Cheketua ameshiriki kwenye kipindi cha Coke Studio Afrika na kupata shavu kubwa zaidi la kuteuliwa miongoni mwa wasanii wachache wa msimu huu kushiriki kwenye wimbo mmoja na Ne-Yo. Fursa hiyo na kwa msaada wa Jokate Mwegelo, Kiba atafanya ngoma na rapper wa Nigeria, Ice Prince.

Habari njema zaidi kwa mashabiki wake mwaka huu ni pale Davido alipotangaza ujio wa ngoma aliyoshirikishwa na msanii huyo.

Wimbo wake Chekecha Cheketua umefanikiwa pia kupenya hadi kushika chart za redio kadhaa za Nigeria. Mwaka huu ametajwa pia kuwania tuzo kibao za kimataifa. Kwa upande wake naye ameshiriki kwenye kampeni za kimataifa ikiwemo ile ya kupinga matumizi ya bidhaa zitokanazo na pembe za ndovu ya Wild Aid.

Vanessa Mdee

11887067_668142586653783_1095353857_n

Vanessa Mdee kwa sasa anachukua nafasi ya mwanamuziki wa kike kutoka Afrika Mashariki mwenye mafanikio makubwa zaidi kimuziki. Nobody But Me aliyomshirikisha rapper K.O. wa Afrika Kusini iliyashawishi masikio ya wahariri wa jarida maarufu zaidi la masuala ya burudani la Marekani, Essence na kumjumuisha kwenye toleo lao la kimataifa. Wimbo huo pia ulishika chart za vituo vikubwa vya runinga vikiwemo MTV Base na Trace TV.

Pamoja na TV, wimbo huo uliingia kwenye Top 10 za redio za Nigeria, Afrika Kusini na kwingine.

Naye pia ameshirikishwa kwenye collabo kibao za kimataifa ukiwemo wimbo aliofanya na Pantoraking wa Nigeria, Sayi Shay, Shaydee na wengine. Ukiachilia mbali kutajwa kuwania tuzo za MTV MAMA mwaka huu, Vee Money pia ametajwa kuwania tuzo takriban nne zingine za kimataifa. Mwaka huu alishiriki kwenye wimbo ‘Strong Girls’ wa One Campaign.

Millen Magese

11821239_832695633495952_1270586772_n

Millen Magese ni mwanamke jasiri na shujaa ambaye tatizo lake la endometriosis halijamzuia kutoyafurahia maisha yake na kusaidia wanawake wengine wenye tatizo hilo. Kutokana na kujitangaza hadharani na kuanzisha taasisi ya kusaidia na kukuza uelewa wa tatizo hilo barani Afrika, Millen amegeuka kuwa mwanaharakati muhimu barani Afrika.

Harakati hizo mwaka huu zilimfanya atunukiwe tuzo ya kwanza na heshima ya BET Global Good. Harakati zake pamoja na kutambuliwa hadi kupewa tuzo, zimemsaidia kwa kiasi kikubwa kuitangaza Tanzania.

Mwaka huu pia Millen alishirikishwa kwenye video ya ngoma ya msanii wa Nigeria, Banky W.

AY

11667385_10155977768870413_4222696183537478644_n

AY ni miongoni mwa wasanii wakongwe ambao kila mwaka huwa na kitu kikubwa na hata kama wasipohit sana kama wengine. Asipokuwa na hit single basi lazima atakuwa amepata shavu kubwa la kimataifa analofanya au kuwa nyuma ya utengenezaji wa kipindi cha TV kilichoshinda mara mbili kwenye Tuzo za Watu, Mkasi.

Mwaka 2015 umekuwa mzuri sana kwa AY na kwa sababu nyingi tu, AY bado anaendelea kulitetea jina lake la ‘Mzee wa Commercial.’

Video ya wimbo wake ‘Touch Me’ aliomshirikisha Sean Kingston, ilitoka December 9 mwaka jana lakini Ilipata airtime zaidi mwaka huu. Video hiyo ilipata mashavu kwenye vituo vikubwa pia vya Afrika ikiwemo MTV Base na Sound City ambako iliingia kwenye Top 10. Lakini kikubwa zaidi ngoma hiyo iliingia kwenye charts za redio na TV kadhaa nchini Jamaica.

Video ya wimbo wake ‘It’s Going Down’ aliowashirikisha Lamyia Good wa Marekani na Ms Triniti nayo ilipata airtime za hapa na pale barani Afrika.

Mwaka huu AY alikuwa mmoja wa wasanii wa Afrika Mashariki walioshiriki kama mentors kwenye shindano la Maisha Superstar la Maisha Magic. Akiwa na rookie, Damian Soul, AY aliongeza kutilia wino wa umaarufu wake barani Afrika.

Kubwa zaidi ni kuwa AY ni miongoni mwa wasanii waliofanikiwa kuachia hit single mwaka huu. Zigo iliyotengenezwa na Nahreel haijafanya vizuri Tanzania tu bali Afrika Mashariki nzima na hadi Nigeria kiasi cha Wizkid kudaiwa kuwa na mpango wa kufanya remix yake. Jose Chameleone ni msanii mwingine aliyeonesha nia ya kutaka kuufanyia kitu mdundo wa ngoma hiyo. Inasubiriwa video yake tu kwa sasa.

Katika kampeni AY ameendelea kushiriki kwenye mambo ya kijamii ikiwa ni pamoja na kuwa balozi wa kujitolea wa UNICEF.


Navy Kenzo

11821173_1616470928638727_970177548_n

Navy Kenzo ni kundi linaloelekea kuwa miongoni mwa makundi muhimu ya muziki Afrika. Kundi hilo mwaka huu limefanikiwa kutoa miongoni mwa video bora za mwaka 2015 ya wimbo wake Game ambao tayari umeshika chart za redio za Afrika na vituo vikubwa vya runinga.

Lakini hata hivyo ndani ya Navy Kenzo, kuna brand nyingine inayojitegemea – Nahreel.

Nahreel ni producer aliyetengeneza moja ya nyimbo kubwa zilizotoka mwaka huu, Nana ya Diamond. Tayari producer huyo amekwishafanya kazi za rappers wa Afrika Kusini, AKA na K.O. pamoja na kundi maarufu la Kenya, Elani. Mwaka huu alichukuliwa miongoni mwa watayarishaji wa muziki waliotumika kwenye kipindi cha Coke Studio Africa.

Joh Makini

11821960_519745881512514_1862012346_n

Joh Makini ni rapper pekee wa Tanzania mwenye video kubwa barani Afrika, Nusu Nusu. Video ya wimbo huo ilishika hadi nafasi ya kwanza kwenye chart ya video za Afrika kwenye MTV Base. Haonekani kubweteka na mafanikio ya video hiyo na ndio maana hivi karibuni alienda tena Afrika Kusini kushoot video ya collabo aliyofanya na rapper AKA.

Shaa

11117172_1612410262314972_908474675_n

Miezi ya hivi karibuni Shaa amekuwa kimya kiaina lakini unajua kuwa ndiye msanii ambaye video yake imeangaliwa zaidi Youtube nchini Tanzania kama sio Afrika Mashariki?

Sugu Gaga iliyotoka mwaka jana imeangaliwa kwa zaidi ya milioni 19.9 hadi sasa. Mwaka huu Shaa amefanya vizuri na wimbo wake ‘Njoo’ aliomshirikisha Redsan. Video ya wimbo huo ilienda hadi kushika kwenye Top 10 ya nyimbo za Afrika kwenye kituo cha Nigeria, Sound City. Naye pia mwaka huu alikuwa mentor kwenye shindano la Maisha Superstar akiwa nyuma ya rookie, Myra.

Lady Jaydee

11235446_10152752400990025_6513769256416713091_n

Mwaka huu Lady Jaydee aliibuka na tuzo ya mwimbaji wa kike anayependwa kwenye tuzo za watu. Kimaisha na kibiashara, mambo yake mwaka huu yameendelea kuwa poa hasa kwakuwa aliwahi kusema kwenye kipindi chake cha TV ‘Diary of Lady Jaydee’ kuwa ana mpango wa kujenga nyumba tano mwaka huu.

Kimataifa, mwaka huu Jide alifanikiwa kuingiza video ya wimbo wake ‘Give Me Love’ kwenye chart za MTV Base. Wimbo huo aliwashirikisha wasanii wa Afrika Kusini, Mazet na Dj Maphorisa wa Uhuru. Mwaka huu pia Jide alishirikishwa kwenye ngoma mbili na wasanii wa Kenya, Sasa ya Jaya na Moyo ya Atemi. January mwaka huu alishinda tuzo za Bingwa za Kenya ambazo ametajwa pia kuwania mwakani.

Wengine?

Sitoacha kuzitambua pia harakati za kimataifa mastaa wengine kama Shettah ambaye ngoma yake Shikorobo aliyomshirikisha Kcee wa Nigeria imemweka pazuri, Hanscana ambaye video alizoongoza ikiwemo Nasema Nawe ya Diamond zimeitangaza Tanzania, Idris Sultan ambaye ushindi wake wa Big Brother Africa ameendelea kuutumia vyema kimataifa na Ommy Dimpoz ambaye video yake ya Wanjera ilishika chart mbalimbali zikiwemo za MTV Base na Sound City.

Wengine ni Yamoto Band ambao video yao mpya ya ‘Cheza Kwa Madoido’ inaelekea kuwapa jina barani Afrika, Sheddy Clever aliyetayarisha wimbo wa Diamond na Ne-Yo, Jux ambaye wimbo wake Looking For You aliomshirikisha Joh Makini umeingia kwenye chart za MTV Base, Ben Pol ambaye mwaka huu ameshiriki kwa mara ya kwanza kwenye Coke Studio Afrika na ambaye amesharekodi ngoma na Nameless pamoja na msanii mkubwa Nigeria, DJ D-Ommy wa Clouds FM aliyechaguliwa kuwa DJ pekee kutoka Afrika Mashariki kutumbuiza kwenye pre-party ya NBA AllStars jijini Johannesburg na wengine.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents