Uncategorized

Akabiliwa na kifungo cha miaka miwili kwa kosa la kumuita aliyekuwa mke mwenza ‘Farasi’

Mwanamke mmoja raia wa Uingereza anakabiliwa na kifungo cha miaka miwili gerezani mjini Dubai kwa kumuita mke wa mtalaka wake ‘farasi’ katika mtandao wa kijamii wa Facebook.

Kwa mujibu wa shirika la habari la BBC, Laleh Shahravesh mwenye umri wa miaka 55, alikamatwa mara baada ya kutua katika uwanja wa ndege wa Dubai kuhudhuria mazishi ya mume wake wa zamani.

Ameshitakiwa kutokana na maneno aliyoyachapisha katika mtandao huo baada ya mtalaka wake huyo ambaye aliwahi kuwa mumewe kuoa tena mwaka 2016.

Bi. Shahravesh alikua kwenye ndoa kwa miaka 18 na aliwahi kuishi Dubai kwa miezi 18, kwa mujibu wa mamlaka ya mji huo.

Baada ya kurejea nchini Uingereza na binti yake mwanaume wake huyo alisalia Dubai na kuoa mke mwingine.

Sharavesh alifahamu kuhusu hatua ya mtalaka aliyewahi kuwa mumewe kuoa tena baada ya kuona picha ya wanandoa hao katika mtandao wa kijamii wa Facebook.

Aliandika maneno ya matusi kwa lugha ya Kiajemi, na kuongeza kuwa mtalaka wake ni ”mjinga na kumuita farasi mke wake mpya”.

Chini ya sheria ya mtandao ya Falme za Kiarabu, mtu anaweza kufungwa jela au kutozwa faini kwa kutoa kauli za chuki mtandaoni.

Maafisa mjini Dubai wanasema kuwa Bi Shahravesh huenda akafungwa jela miaka miwili au kutozwa faini ya pauni 50,000, licha ya kuchapisha maneno hayo akiwa nchini UIngereza.

Shirika la kutetea haki la Detained in Dubai, linalofuatilia kisa hicho, linasema kuwa mke mpya wa mtalaka wa Shahravesh anayeishi Dubai ndiye aliyepiga ripoti polisi.

Inasemekana kuwa Bi Shahravesh na binti yake waliingia mjini Dubai Machi 10 kuhudhuria mazishi ya mtalaka wake, aliyefariki dunia kutokana na mshtuko wa moyo.

Wakati wa kukamatwa kwake binti yake wa miaka 14, alilazimika kurudi peke yake nyumbani Uingereza, liliongeza shirika hilo.

Afisa mtendaji mkuu wa shirika la Detained in Dubai, Radha Stirling, ameiambia BBC kuwa shirika hilo kwa ushirikiano na ofisi ya uhamiaji zilimuomba mlalamishi kuondoa madai hayo, lakini amekataa kufanya hivyo.

Bi Stirling amesema kuwa mteja wake ameachiliwa kwa dhamana lakini pasipoti yake imechukuliwa na kwamba kwa sasa anaishi katika hoteli.

Ameongeza kuwa Bi. Shahravesh, “amepata usumbufu wa kiakili” na kwamba itamchukua mda mrefu kabla ya kusahau kisanga hicho.

Binti yake pia ametatizika kimawazo na kile anachotaka kwa sasa ni kuungana tena na mama yake, alisema Bi. Stirling.

Aliongeza kuwa watu huenda hawana ufahamu kuhusu sheria kali za uhalifu wa mtandaoni katika Falme za Kiarabu na idara ya uhamaji ya nchi hiyo haijatoa onyo kwa watalii.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents