Habari

Fisi aua watoto watatu wa familia moja

KATIKA Kitongoji cha Gengeni kilichopo Kata ya Kambikatoto, Tarafa ya Kipembawe, Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya, Mnyama Pori aina ya Fisi alivamia nyumba ya Shigela Ngasa [45] Mkazi wa Gengeni na kuwauwa kwa kuwang’ata watoto watatu wa familia hiyo ambao ni Samweli Shigela [05], Kasunzu Shigela [03] na Ngasa Shigela mwaka mmoja wote wakazi wa Gengeni.

Aidha, katika tukio hilo mnyama huyo aliwajeruhi wazazi wa watoto hao ambao ni Shigela Ngasa [baba] na mke wake aitwaye Limi Masanja [38] wote wakazi wa Gengeni. Baada ya tukio hilo Fisi huyo aliua kondoo wawili na kisha akakimbia uelekeo wa Hifadhi ya Rungwa eneo la Kambikatoto. Fisi huyo aliweza kuingia ndani ya nyumba hiyo kutokana na nyumba hiyo kutokuwa na mlango na iko porini karibu na Hifadhi hiyo.

Hayo yamesemwa na Kaimu Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Mbeya, Abdi Issango – SACP Aprili 07, 2024 jijini humo amesema kuwa Majeruhi wamelazwa Hospitali ya Mtakatifu Gasper – Itigi, Wilaya ya Manyoni, Mkoa wa Singida kwa matibabu zaidi. Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Askari wa wanyama pori kutoka pori la akiba la Rungwa na Wananchi wa Gengeni limefanikiwa kumuua Fisi huyo ambaye alikimbilia Porini na baadae kurudi tena Kijijini hapo.

Wakati huo huo, Mnamo Aprili 07, 2024 katika Kitongoji cha Katagho kilichopo Kijiji cha Ngeleka, Kata ya Makwale, Tarafa ya Ntebela, Wilaya ya Kyela, Mkoa wa Mbeya, watoto watano walifariki dunia wakati wanapatiwa matibabu katika Zahanati ya Uhai Baptist baada ya kuzama ndani ya dimbwi la maji lililopo kwenye shamba la kakao lenye ukubwa wa ekari nne.

Watoto waliofariki katika tukio hilo wametambulika kwa majina ya Rahel Christopher Mwaikale [05] Mwanafunzi darasa la kwanza Shule ya Msingi Ngeleka, Carolina Anosisye Mwamkamba [kulwa] [06] Mwanafunzi darasa la kwanza Shule ya Msingi Makwale, Catherine Anosisye Mwamkamba [doto] [06] Mwanafunzi darasa la kwanza Shule ya Msingi Makwale, Lightness Ephraim Kakenda [05] Mwanafunzi wa Chekechea Shule ya Msingi Ngeleka na Kalebu Atufigwege Mwaikombe [05] Mwanafunzi wa Chekechea Shule ya Msingi Ngeleka.

Uchunguzi wa awali umebaini kuwa watoto hao walienda kuogelea kwenye dimbwi lililojaa maji kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha ndipo walizidiwa na maji na kuzama, walipiga kelele kuomba msaada wa kuokolewa na wananchi lakini tayari walikuwa katika hali mbaya. Watoto hao walikimbizwa katika Zahanati ya Uhai Baptist hata hivyo walifariki dunia wakiwa wanaendelea kupatiwa matibabu.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea kutoa wito kwa wazazi na walezi kuchukua tahadhari kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha kwa kuhakikisha wanaweka uangalizi mzuri kwa watoto wao ili kuwalinda dhidi ya maafa yatokanayo na mvua.

Written by Janeth Jovin

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents