Bongo5 MakalaDiamond Platnumz

Makala: Vanessa katuonyesha kitu, vipi kuhusu Diamond na Wakazi

Nyumbani kwao anatambulika kama Vanessa Mdee, pia Bongo Flava inamtambua kwa jina hilo na kuongezea la Vee Money pamoja na Cash Madame. Sauti yake imeburudisha na kukonga nyoyo za wapenzi wa muziki huo kwa miaka kadhaa sasa.

Alianza kusikika katika kolabo, kisha akatoa ngoma yake binafsi, akatoa hit na hit na hadi sasa ana albamu yake, Money Mondays.

Money Mondays iliingia mtaani January 20 mwaka huu ikiwa na nyimbo zipatazo 17, uzinduzi wa albamu hiyo ulifanyika Dar es Salaam December 29 mwaka jana baada ya kusubiriwa kwa zaidi ya miaka mitatu.

Albamu hii imekuja katika Bongo kukiwa na vuguvugu la wasanii kutokutoa albamu kwa sababu ambazo nitazieleza hapo baadaye, hata hivyo Vanessa kuna maeneo mawili ambayo ameweza kupambana nayo kwa asilimia kubwa;

Promotion

Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji Clouds Media Group (CMG), Ruge Mutahaba aliwahi kukuririwa akisema wakati yeye na team yake wanaingia katika Industry ya Bongo Flava walihakikisha wanatoa muziki huo kule ulipokuwa na kuuleta katika platform za kibiashara.

Hivyo basi kwa hapa ilipofika Bongo Flava pasina shaka ni biashara kubwa kwa sasa. Kama ilivyokawaida biashara yoyote ile inahitaji matangazo ili kuweza kuwafikia walaji wa bidhaa husika/wateja.

Vanessa pia analitambua hilo, albamu yake ni bidhaa ambayo anahitaji iwafikie wateja ambao ndio mashabiki wake, ametumia vyombo vya habari, mitandao na njia tofauti tofauti kuhakikisha anafikia malengo yake.

Siku chache baada ya kuachia albamu ‘Money Monday’ alizindua programu ‘App’ yake mpya ya simu ya VEE MONEY ambayo inapatikana bure kupitia ‘Google Play store’ na ‘Apple store’.

Programu hii ambayo imetengenezwa na kampuni ya masuala ya teknolojia ya Marekani ‘Converge Media’ ni sehemu ambayo itawezesha mashabiki wake kupata bidhaa za Vanessa kama vile nyimbo (albamu), video, picha na kuona kurasa zake za kijamii.

Licha ya kuwa na App hiyo Vanessa pia ana tovuti yake, vanessamdee.com kwa ajili ya kuweka kazi za matukio mbali mbali anayoyafanya kila siku, tovuti hii ilifunguliwa mwaka jana na muda wote ipo updates, hivyo basi albamu ilikuwa imeshaandaliwa mazingira mazuri ya kuitangaza toka awali.

Baada ya kuizindua albamu hiyo Dar es Salaam na kuuza nakala kadhaa aliweza kufanya hivyo Nairobi nchini Kenya, pia alienda Nigeria na mara ya mwisho alikuwa Zanzibar, hiyo yote ni kuhakiki kile alichokiandaa kinawakifikia wengi zaidi.

Mauzo

Kwa muda mrefu wasanii wengi wamekuwa wakisita kutoa albamu kwa kuhofia soko limejaa maharamia na walanguzi wa kila namna, kitu hiki kilifanya Bongo Flava kukaa kipindi kirefu bila albamu. Hata hivyo ukuaji wa teknolojia unakuja na fursa zake kama nilivyotangalia kuaeleza.

Vanessa ameweza kupambana na changamoto zilizopo muda wote na kutumia fursa chache kuhakikisha albamu yake inauzika na kumpatia kile anachotaka.

Hadi kufikia February 8 mwaka huu Vanessa alieleza kuwa nakala zaidi ya 4,000 alikuwa ameshaziuza ambapo kila nakala moja anaiuza kwa Tsh. 10,000, hapo kwa hesabu ya haraka haraka ameingiza zaidi ya Tsh. Milioni 40.

Je hayo ni mafanikio kwa Vanessa?, hapana, kwa mujibu wa Vanessa mwenyewe hadi kukamilika kwa albamu hiyo kumemgharimu Tsh. Milioni 100 hivyo bado kuna kitu cha zaidi anahitaji.

Hili ni somo kubwa kwa wasanii kujifunza namna ya kuwekeza ili kuzalisha bidhaa nzuri, albamu ya Vanessa kutokana na ubora wake ina muda mrefu katika soko na pasina shaka itamletea faida kimuziki na kiuchumi pia.

Kwanini Diamond na Wakazi

Hawa ni wasanii ambao wanazo albamu zao mkononi tayari na kwa kipindi kirefu sasa wamekuwa wakitangaza kuzitoa lakini kwa sababu kadhaa wamekuwa wakisita hasa Wakazi.

Diamond ana albamu inayokwenda kwa jina la A Boy From Tandale, huku Wakazi akiwa na albamu aliyoipa jina la Kisimani, hizi zote zimekamilika na zipo tayari kutoka.

Wasanii hawa wote wameshawahi kutoa albamu kipindi cha nyuma, sitegemei iwapo watafanya kwa kiwango cha mwanzo, nategemea hatua kadhaa mbele, kuuanzia upande wa production, promotion na mauzo pia.

Naamini hivyo kwa sababu wasanii wanaoamua kutoa albamu kipindi hiki ni watu wanaotaka kubadili upepo uliozoeleka na kuleta mtazamo mpya. Changamoto zilizokwamisha albamu kutoka wanazijua ila kuna fursa walizoziona kama digital platform na nyinginezo wanataka watu wazijue, hivyo Diamond na Wakazi kazi kwenu.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents