Bongo5 Makala

Makala: Nini maana ya hizi nyimbo? ‘Mkemia Mkuu, Bombardier, Amsha Dude & Kiba_100

Wakati mwaka 2017 ukielekea ukingoni kuna mambo mengi ya kutafakari kiujumla katika maisha ila leo tuanzie katika burudani, tena katika muziki wa Bongo Flava.

Mwaka huu katika Bongo Flava kumefanyika mambo mengi makubwa na mazuri ikiwepo wasanii kama Diamond, Alikiba na Nandy kushinda tuzo za kimataifa, pia wasanii kama Lady Jaydee, Chege, Ben Pol na Navy Kenzo kutoa albam, well done Bongo Flava.

Pia wasanii wameweza kutoa ngoma kubwa ambazo zimeweza kuleta ushindani baina yao kitu kilichoibua shangwe la burudani kwa mashabiki wao, ni vizuri pia.

Karibu Jamvini

Kama umefuatilia kwa makini kwa mwaka huu kuna baadhi ya nyimbo ambazo zimetoka na zimekua na tungo tofauti kidogo na zile ambazo zimekwisha sikika hapo awali.

Tungo hizi ambazo zimejaa mafumbo ndani yake, unaposikiliza unaweza kupata maana fulani na unapotulia unazidi kupata maana nyingine ya ziada.

Baadhi ya mashabiki amekuwa wakishikilia tafsiri yao ambayo ni tofauti na ile iliyokusudiwa na msanii husika. Hapa jamvini nimeleta ngoma kadhaa ambazo tunaweza kuzijadili;

Rostam – Kiba_100

Rostam ni muunganiko wa wasanii wawili, Roma na Stamini na muungano huu umeanza mwaka huu kwa kuachia ngoma yao ya kwanza ‘Hivi Ama Vile’.

Hivi sasa wanatamba na ngoma yao mpya ‘Kiba_100’ ambayo wamemshirikisha Mau Sama aliyeimba chorus. Ingawa wanazungumzia mapenzi ila kona waliyoitumia imekuwa tata kidogo kutokana ni mambo ambayo ni nadra sana kuzungumziwa wazi wazi.

Kutokana na hilo baadi ya watu wameenda mbali zaidi na kudiriki kusema ngoma hiyo imejaa matusi kitu ambacho Stamina amesema si Kweli. Hivi karibuni Stamina alikiambia kipindi cha XXL, Clouds Fm kuwa katika uandishi walifuata maadili na kuwashangaa wale wanaosema ngoma hiyo ifungiwe.

“Sisi wenyewe katika uandishi tulifuata maadili ya kutofikisha vitu vingine kwa sababu ya ukali wa maneno, ukisema wimbo ufungiwe ni sawa na kusema niache kazi yangu ya muziki, halafu kuna kuwa hakuna uhuru” alisema Stamina.

Hata hivyo wasanii hawa wamekuwa wabunifu kwa kuangalia kile ambacho kinazungumzwa lakini hakipiwe jukwaa la kujadiliwa kwa uwazi. Hizi ni baadhi ya line zinasikika katika verse hiyo.

https://www.youtube.com/watch?v=TEGAqqpxrY8

 

Pia ubunifu mwingine walioufanya ni katika video, kitendo cha kumuweka Dkt. Louis Shika ambaye amekuwa maarufu mara baada ya kujitokeza katika mnada wa kuuza nyumba za Lugumi ambapo Dk. Shika aliahidi kununua nyumba hizo kwa thamani ya Sh bilioni 2.3 lakini alishindwa kulipia asilimia 25 ya fedha hizo ambazo ni shilingi milioni 800, ni credit kubwa kwao.

Izzo Bizness ft Quick Rocka – Mkemia Mkuu

Hapa vinakutana vichwa viwili kutoka mkoani Mbeya, hii siyo ngoma ya kwanza kwa Izzo kumshirikisha Quick Rocka, wameshafanya ngoma kama Ball Play ambayo alikuwepo na Marehemu Ngwea.

Mkemia Mkuu ni neno/ jina la kawaida ambalo lipo siku zote na si ngeni masikioni mwa wengi lakini hivi karibuni limekuwa maarufu baada ya baadhi ya viongozi, wafanyabiashara na wasanii kutakiwa kupimwa (mkojo) na huyo Mkemia Mkuu ili kuthibitika iwapo wanatumia dawa za kulevya.

Izzo akaamua kutumia nafasi hiyo kisha kuingia studio na kutoa ngoma hiyo, wewe unaelewa nini hasa hapo?, tujadili.

Weusi – Amsha Dude

Baada ya kufanya vizuri na ngoma ‘Madaraka ya Kulevya’, waliamua kuachia ngoma hii ‘Amsha Dude’. Ngoma ya awali ilikuwa pasua kichwa kwani licha ya kuzungumzia mahusiano ya kimapenzi ilihusishwa na mambo ya kisiasa.

Wakati ngoma hiyo inatoka ni kipindi ambacho wasanii walikuwa wanasita kutoa ngoma zao kwa kuhofia kumezwa na matukio ya kisiasa yalikuwa yakiendelea, hata hivyo ngoma iliweza kufanya vizuri kutoka iliweza kuendana na mazingira, tuachane na hilo.

Amsha Dude ni neno lilokuwa maarufu kwa kipindi kifupi na aliyesababisha hilo ni Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima. Weusi wakachukua hilo na kuitengeneza ngoma.

https://www.youtube.com/watch?v=P4Q2sId04Ls

Hizo ni lines zilizopo katika chorus hiyo ambazo G Nako na Joh Makini wameshirikiana, je mashabiki wanaweza kupambanua kile kilichokusudiwa na wahusika?, tujadili.

Dully Sykes – Bombardier

Baada ya Rais Dkt. John Magufuli kuingia madarakani mwaka 2015 alianza mkakati wa kufufua Shirika la Ndege Tanzania (ATL), moja ya mikakati ilikuwa ni kununua ndege mpya na kweli alifanikiwa kununua ndege aina ya Bombardier.

Mara paap, anajitokeza Dully Sykes na kutoa ngoma inayokwenda kwa jina la Bombardier. Ngoma hii kwa sasa inafanya vizuri na mapokezi yake yamekuwa makubwa.

Watu wengi wanachofurahia katika ngoma hii ni melody kama ilivyokuwa katika nyingi za Dully Sykes ambazo amekuwa akizitoa hivi karibuni, lakini kweli mashabiki wanauelewa na kile kinachoimbwa?, tujadili.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents